Kazi ya Mahakama pia kulinda haki zisivunjwe na Bunge, Serikali

18Jul 2021
Nipashe Jumapili
SIASA
Kazi ya Mahakama pia kulinda haki zisivunjwe na Bunge, Serikali

​​​​​​LEO naendelea na hizi makala zangu elimishi kuhusu changamoto za utoaji wa haki Tanzania, kwa mujibu wa katiba yetu, imeeleza tena kwa maandishi makubwa, “UTOAJI HAKI KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO, UTASIMAMIWA NA MAHAKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO, MAHAKAMA YA RUFANI YA JAMHURI YA MUUNGANO”.

Ibara ya 107A ya Katiba yetu, imetoa mamlaka yote ya utoaji haki kwa mhimili wa mahakama. .-(1) Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge, kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.

Ibara hii ina maana kubwa sana, inamaanisha japo nchi inaendeshwa kwa mihimili mitatu ya Serikali, Bunge na Mahakama, lakini katika suala zima za utoaji haki, Mahakama ndio chombo chenye mamlaka ya mwisho, sio Bunge, wala serikali. Tanzania tumeshuhudia Bunge likijiinua na kujigeuza mahakama, huku likiita watu kuwahoji kupitia ile kamati yake ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, ambayo ina kaa kama Quasi Judicial body, na uamuzi wa kamati hizi unaelezwa kuwa ni wa mwisho, kitu ambacho kiukweli ni kinyume cha katiba!.

Pia serikali, kupitia mamlaka zake mbalimbali, zinazokaa kama Quasi Judicial bodies, zinatoa maamuzi yanayoelezwa kuwa ni  ya mwisho, chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa maamuzi ya mwisho kwenye masuala yote ya haki, ambayo ni final na conclusive, ni mahakama pekee, hayo engine yote ya vyombo hivyo, yanayojiita ni ya mwisho, ni kujiinua tu.

Tena Katiba yetu, imeweka mwongozo kwa mhimili wa mahakama, ibara ya 107 2 “Katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo, yaani: (a) kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kiuchumi; (b) kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi; (c) kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine, na kwa mujibu wa sheria mahususi iliyotungwa na Bunge; (d) kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro; Uhuru wa Mahakama Sheria ya 2000 Na.3 ib.17 107B. Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano na mamlaka yake.

Tukizama zaidi ndani ya mahakama, kuna “MAHAKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO na MAHAKAMA KUU YA RUFANI”

Ibara ya 108 inaeleza.-(1) Kutakuwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano (itakayojulikana kwa kifupi kama "Mahakama Kuu") ambayo mamlaka yake yatakuwa kama ilivyoelezwa katika Katiba hii au katika sheria nyingine yoyote. (2) Iwapo Katiba hii au sheria nyingine yoyote haikutamka wazi kwamba shauri la aina iliyotajwa mahususi litasikilizwa kwanza katika Mahakama ya ngazi iliyotajwa mahsusi kwa ajili hiyo, basi Mahakama Kuu itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kila shauri la aina hiyo. Hali kadhalika Mahakama Kuu itakuwa na uwezo wa kutekeleza shughuli yoyote ambayo kwa mujibu wa mila za kisheria zinazotumika Tanzania shughuli ya aina hiyo kwa kawaida hutekelezwa na Mahakama Kuu. Isipokuwa kwamba masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila ya kuathiri mamlaka ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kama ilivyoelezwa katika Katiba hii au katika sheria nyingine yoyote.

Mahakama Kuu, inaongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu (ambaye katika ibara zifuatazo kwenye Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Kiongozi"). Jaji Kiongozi atakuwa ndiye msaidizi maalum wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake, na katika madaraka hayo Jaji Kiongozi atatekeleza kazi na shughuli atakazoagizwa au kuelekezwa mara kwa mara na Jaji Mkuu, na kwa madhumuni ya ibara hii, Jaji Kiongozi atajulikana pia kama Mkuu wa Mahakama Kuu.

Mfumo wa utoaji haki nchini kwetu Tanzania, ni kunapofanyika kosa, hatua ya kwanza ni kuripotiwa kwa kosa husika, kisha uchunguzi unafanyika, kisha mtuhumiwa anashtakiwa mahakamani. Hivyo mahakama zetu, zinasubiri mashauri yaletwe mahakamani yasikilizwe na mahakama kutoa uamuzi.

Huu ndio utamaduni wa kimahakama kwa mahakama kusubiri kupelekewa mashauri. Kazi za mahakama sio kusikiliza tuu mashauri, bali kazi ya kutafsiri sheria, ni moja ya majukumu muhimu sana ya mahakama, na kazi ya kulinda haki, ni jukumu kubwa kuliko yote lililotukuka la mhimili wa mahakama.

Tanzania tumeshuhudi kelele nyingi za tuhuma za uvunjwaji wa katiba, sheria, taratibu na kanuni, mamlaka pekee yenye kusema kama Katiba imekiukwa au la, ni mhimili wa mahakama!, kwa vile mahakama yetu inasubiri shauri lifunguliwe, ndipo inatoa ufafanuzi, hakuna shauri lolote lililofunguliwa mahakama yoyote kuitaka mahakama kutoa ufafanuzi wa ukiukwaji wa Katiba, hivyo katiba inakiukwa, na maisha yanaendelea ‘as if nothing happened’.

Kafuatia Watanzania wengi kutojua haki zao, hivyo wanavunjiwa haki zao bila kujua, na maisha yanaendelea, sasa ni wakati muafaka, kutapotokea suala la ukiukwaji wa haki zozote za mzingi zilizoainishwa kwenye Katiba yetu kukiukwa,  mhimili wa mahakama, usisubiri shauri lifunguliwe, bali ujiongeze kwa kujitokeza wazi wazi kulinda na kutetea haki zinazokiukwa na Bunge na Serikali, kupitia kitu kinachoitwa “Suo Motto”, na pale mahahama inapoona wazi kabisa, Katiba imekiukwa, serikali au Bunge limekiuka haki ya msingi, mahakama ina act on its own volition, bila mtu yeyote kufungua shauri na kuilinda haki hiyo ya msingi.

Mfano mzuri ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, haki hii imetolewa na Katiba, kukatokea kiongozi, akaifuta kwa kauli tu! Mahakama haikupaswa kukaa chini na kunyamaza kimya ikisubiri kufunguliwa kwa shauri, ilipaswa kuinuka na kulinda haki hii ya msingi. Hivyo katika utetezi wa haki, mhimili wa mahakama usikae tu kusubiri mashauri, itende haki ya kulinda haki hata bila ya kufunguliwa shauri.

Wasalaam

075427003

[email protected]