Kengele ya hatari kwa wachezaji wa Kibongo

22Jul 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kengele ya hatari kwa wachezaji wa Kibongo

ILIKUWA inakwenda taratibu, lakini sasa ni dhahiri kuwa klabu nyingi zimeanza kupenda kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi.

Zamani ilionekana kwa Simba, Yanga na Azam tu, lakini taratibu kwa sasa imeanza kuvuka mipaka, klabu hata Biashara ya Mara, Kagera Sugar, Stand United, Mwadui FC, Alliance FC zimeanza kuvutika na wachezaji wa kigeni.

 

Hata Namungo FC, ambayo imepanda daraja msimu huu imeonekana kufukuzia pia wachezaji wa kigeni. Kwa mara ya kwanza kabisa msimu huu, sijaona zile pilikapilika za Simba, Yanga na Azam kugombea wachezaji wa Kibongo waliowika kama ilivyokuwa huko nyuma.

 

Nina uhakika kabisa kama ingekuwa miaka ya nyuma, Simba na Yanga zilipokuwa zikipigana vikumbo kugombea wachezaji waliovama vema, basi wachezaji kama Salum Aiyee aliyekuwa Mwadui FC na kuwa wa pili kwenye nafasi ya ufungaji bora nyuma ya Meddie Kagere wa Simba, angezua zogo kubwa la kugombewa na klabu hizi kubwa.

 

Kulikuwa na wachezaji waliotia fora kama Ramadhani Kapera na Kassim Khamisi wa Kagera Sugar, Raidhin Khafidh wa Coastal Union na wengine wengi, ingekuwa ile enzi ya zamani ingekuwa balaa.

 

Na hii ilikuwa inasababisha wachezaji hao kujiwekea gharama kubwa usajili kutokana na kuhitajika kwa udi na uvumba na klabu hizo.

 

Msimu huu haiko hivyo. Pamoja na kupata mafanikio makubwa, lakini Simba, Yanga na wala Azam haikuwa na mpango kabisa na wachezaji hao.

 

Badala yake zimesajili wachezaji wachache tu wa ndani, na wengi wa nje ya nchi.

Pamoja kwamba kumekuwa kama kuna mpango hivi wa kutaka kuwafanyia wepesi kwa kuwapunguza wageni wawekewe idadi ndogo tu ya kucheza uwanjani, lakini hii haiwezi kuwasaidia bali kuwapoteza zaidi.

 

Tatizo kubwa la wachezaji wa Kitanzania kwanza kabisa gharama zao wa usajili ni kubwa kuliko uhalisia wa uwezo wao wa kawaida.

 

Pili ni kwamba wachezaji wengi wa Kibongo hawana mwendelezo wa uwezo wao. Leo anaweza kucheza vizuri, kesho akawa vingine kabisa isivyotarajiwa.

 

Lakini pia mara nyingi ni wachezaji wa msimu. Yaani msimu huu anaweza kufunga magoli 19, lakini msimu ujao akashindwa kufikisha japo magoli 10 tu, akafunga manne au matano.

 

Wengi wao wanabweteka mapema na sifa za mashabiki mitaani na kushindwa kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii baada ya hapo.

 

Kingine ni kwamba wachezaji wa Kitanzania wanakosa nguvu, stamina na pumzi, na hii inatokana na kutopenda mazoezi magumu, badala yake huetegemea zaidi vipaji vyao tu.

 

Kwa sasa soka duniani limebadilika sana, nguvu hutumika zaidi na mifumo kuliko vipaji binafsi, hivyo klabu kubwa kama za Simba, Yanga na Azam zinapenda kusajili wachezaji wa nje ya nchi kwa ajili ya kufanya vema kwenye mechi za kimataifa.

Klabu hizo tayari zimeshagundua kuwa ili ziweze kufanya vema kwenye michuano hiyo ni lazima ziwe zaidi na wachezaji wa nje na wachache tu wa ndani.

 

Hii ndiyo imesababisha msimu huu wa usajili usiwe mzuri sana kwa wachezaji wa Kitanzania.

 

Kilichobaki sasa kwa wachezaji hao inafaa kukaa na kujitafakari na kuangalia udhaifu wao ambao nimejaribu kuuelezea.

 

Kingine ni kuondoka nchini kwa kwenda kucheza soka nje ya nchi kwenye klabu mbalimbali na kukutana na changamoto ili kujijengea uwezo wa kupambana.

 

Na hata wale ambao watakaobaki, wajaribu kubadilika, kwani ukiona hata Biashara ya Mara na Namungo FC wanatafuta wachezaji wa kigeni, hii si dalili nzuri kwa mustakabali wao wa baadaye na nchi nzima.

 

Ikumbukwe kuwa klabu hazilazimishwi kusajili wachezaji wa nje, bali wanafanya hivyo kutokana na mahitaji na kama siku wakijirekebisha, tutaanza kuona klabu hizo hizo zikipunguza kusajili wachezaji kutoka nje.