Kero ya foleni Dar hadi lini?

14Apr 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Mjadala
Kero ya foleni Dar hadi lini?

“TUMEZOEA…. ni sehemu ya maisha yetu sasa.Ukitaka kwenda sehemu ni lazima uondoke nyumbani lisaa limoja kabda ili ufike kwa wakati unakokwenda,”

Hizo ni baadhi ya kauli za wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambazo husikika mara kwa mara wakizungumzia shida na kero ya foleni inavyowatesa siku hadi siku au mara kwa mara.

Wengine nimewahi kuwasikia wakisema kwa namna ya mshangao kidogo kwamba “ Du! leo Ubungo hakuna foleni maajabu haya ya karne ya 21 hapa Tanzania….”

Wengineo nao kwa mtazamo wao wanaamrishana kwamba“ .Chukua bodaboda uende, ukipanda daladala utachelewa kuna foleni sana katika barabara fulani na fulani za hapa jijini…”

Ndizo kauli za baadhi ya wakazi wa Jiji hilo, ambalo ni kitovu cha nchi kiuchumi.Ndilo Jiji kubwa zaidi nchini lenye watu wengi na shughuli nyingi za maendeleo zinatekelezwa hapa.

Ofisi karibu zote muhimu hasa za serikali na nyinginezo ambazo mapato yake ni makubwa kwa maendeleo ya uchumi wa watu na nchi kwa ujumla lakini kero kubwa inayojitokeza na kuathiri mwenendo wa maisha ya watu ni foleni zisizokwisha ambazo hazitabiriki.

Ni kawaida mtu kukaa barabarani kwa zaidi ya mbili hadi tatu hivi katika eneo moja ambalo lina umbali wa kuweza kusafiri kwa dakika 30.

Ndilo Jiji ambalo mvua ikinyesha kwa dakika kadhaa tu, magari yanafungana barabarani kwa saa kadhaa utadhani kuna ajali imetokea, kumbe ni foleni.

Jiji hilo mvua ikinyesha ni kawaida kusota kwenye foleni kwa saa tano hadi sita hivi. Hali hiyo ni kwamba, kwa aliyetoka kazini mathalani katika eneo la Posta saa 12 jioni na unaishi Mbezi mwisho, ni lazima ufike nyumbani kwenye majira ya saa nne usiku.

Ni umbali ambao katika hali ya kawaida kabisa ungetumia saa moja tu kufika kisha ukaendelea na shughuli nyinginezo.

Ki ukweli kwa sasa Jiji limezidiwa na uwingi wa magari barabarani, hata taa zilizowekwa kuongozea magari hayo ni kama zimeshindwa na ndiyo sababu askari wa usalama barabarani utawakuta wakiongoza magari katika baadhi ya maeneo kwa muda mwingi.

Serikali inajitahidi kujinasua katika suala hili, lakini ni kama inashindwa kwa sababu idadi ya magari yanayoingia nchini kwa mwaka ni kubwa kulinganisha na uwezo wa miundombinu iliyopo kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo aliwahi kueleza kuwa mwaka 2015 yaliingia magari madogo 53,927, na wastani kwa mwezi huingia magari 4,493 nchini.

Hivyo utaona idadi kubwa ya magari yanayoingia nchini kwa mwaka na kwa mwezi, lakini miundombinu haiongezwi kwa kasi hiyo wala njia nyingi za mzunguko hazikarabatiwi ili kuchangia kupunguza foleni katika njia kuu za Jiji la Dar es Salaam hata kusababisha matatizo yanayojitokeza sasa.

Rais Dk. John Magufuli katika siku zijazo natarajia makubwa na mazuri katika uongozi wako, naomba uingilie kati kero hii na anza mipango ya kiutekelezaji ya kuongeza miundombinu na kuiboresha iliyopo pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa wakandarasi wote wanaojenga barabara chini ya viwango hata kusababisha inaponyesha mvua kwa muda mfupi tu zinaharibika vibaya sana.

Katika hili, siyo Rais Magufuli peke yake mwenye dhamana ya kutatua kero hii, hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anawajibu wa kuhakikisha kuwa kero hiyo ambayo kadri miaka inavyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo tatizo hilo linazidi kuwa sugu.

Ni kweli Mkuu wa mkoa una majukumu mengi yaliyo chini ya dhamana yako, lakini ninakuomba inasue Dar es Salaam kutoka kwenye dhahama hii ya ubovu wa miundombinu, mathalani barabara za mitaani ambazo zinaweza kusaidia kupunguza foleni lakini nyingi ni mbovu sana.Na kipindi cha mvua ndiyo hali huwa mbaya zaidi.

Ndiyo maana nakuomba Rais, Waziri mwenye dhamana na Mkuu wa mkoa mtuondolee kero hii, ili uchumi uzidi kupaa kwani huwezi kuzungumzia maendeleo ya uchumi wakati kuna kikwazo kikubwa cha miundombinu inayosababisha foleni hivyo watu kuchelewa kufika katika shughuli za uzalishaji.

Ni jambo lisiloingia akilini kwa karne ya sasa, nchi imetimiza miaka 50 na zaidi tangu kupata Uhuru, lakini kero ya foleni ishindwe kutatuliwa kwa kiwango ambacho hakielezeki.

Kama serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutumbua majipu basi tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam nalo ni jipu sugu ambalo linatakiwa kupatiwa dawa halisi ya kulitibu haraka na kwa uhakika zaidi.Linalowezekana leo lisingoje kesho.