Kero za wamachinga sokoni, barabarani zimalizike sasa

09Jun 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kero za wamachinga sokoni, barabarani zimalizike sasa

HIVI karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, alilizuru soko la Kariakoo jijini Dar –Es- Salaam na kuahidi kushughulikia kero za soko hilo maarufu barani Afrika, lakini akatoa neno kwa wafanyabiashara ambalo ni muhimu kulizingatia.

Rais aliwakumbusha kwa kusema; 'abebwaye hujikaza na ninyi jitahidini kufuata sheria zinazowekwa katika maeneo mlipo maana nimeona njia zote zimezingirwa, ni vibanda kila kona'.

Kauli hiyo ya Rais inawakumbusha wafanyabiashara kuwa wakati serikali inawabeba, nao wanatakiwa kufuata sheria ili kuepusha msoguano na malumbano kati yao na serikali au watu na mamalaka nyingine hasa majiji na wilaya.

Akiwa Kariakoo, Rais alishuhudia kitu alichokiita 'vurugumechi', kutokana na wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila kuzingatia utaratibu hadi 'kuvamia kila eneo na kusababisha watu wengine kushindwa kutumia barabara.

Ufanyaji biashara wa aina  hiyo haupo Kariakoo tu, bali karibu maeneo yote ya masoko ya Tanzania kuanzia jijini Dar es Salaam hadi Makoroboi Mwanza mpaka Mwanjelwa Mbeya hali ambayo inaonyesha wazi kwamba kuna haja viongozi wa hamashauri kuwaweka kwenye maeneo rasmi ya biashara.

Kwa sasa wapo wanaopanga biashara kwenye vituo vya daladala na kusababisha usumbufu kwa madereva na abiria, kwa kuwa wakati mwingine magari yanakosa sehemu ya kupita kwa sababu yao.

Wengine wanapanga bidhaa kwenye barabara zinazoendelea kujengwa, huku mama na babalishe, wachoma mahindi, viazi na wakaanga chipsi na ndizi kwa upande wao, wanawasha moto kwenye vituo vya mabasi na popote penye upenyo.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye baadhi ya vituo vya daladala, mabasi na kwenye njia za wanotembea, madaraja, juu ya mitaro ni kama wanaozimiliki wao hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji.

Kwa mazingira hayo ni kama 'vurugumechi' aliyosema Rais Samia alipotembelea soko la Kariakoo, kwani kinachoendelea sasa ni kama wamejimilikisha baadhi ya barabara.

Ikitokea bahati mbaya mpita njia akakanyaga bidhaa za mmachinga, anaweza kujikuta katika wakati mgumu kwa kutukanwa matusi ya nguoni, kana kwamba hana haki ya kutumia njia au barabara.

Njia bora itakayoondoa mkanganyiko huo, ni kuwapeleka katika masoko yao kama yapo, au kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya usalama wao na wa watu wengine ambao ni watumiaji wa barabara na vituo vya daladala.

Vilevile jiji la Dar- es- Salaam linaweza kuweka utaratibu bora ambao makundi yote hayo yatanufaika nao na ikibidi, itengwe hata mitaa maalum kwa ajili yao, ambayo haiingiliani na shughuli nyingine.

Kuendelea kufanya biashara katika mazingira ya sasa ni sawa na vurugumechi au ‘mchafukoge' ambazo zinaweza kusababisha watu wakaumizana au wakaungua kwa moto wa kupikia vyakula unaowashwa vituoni.

Kwa mfano, abiria ni wengi kituoni, usafiri ni wa shida, halafu inakuja daladala wanaanza kukimbizana kuwawahi kupanda na bahati mbaya mmoja wao akajigonga kwenye jiko lenye maji yanayochemka. Hilo linaweza kusababisha ajali watu wakaungua, hivyo umuhimu wa kuepusha abiria na wafanyabiashara wenyewe katika hatari, ni kila upande kuwa na eneo lake, kuliko kujichanganya pamoja huku wengine wakifanyabiashara hatarishi.

Itapendeza iwapo vituo vya daladala vitabaki kuwa vya abiria na maeneo ya kupika na kuuza vyakula yake kwa ajili ya mama lishe, baba lishe na wengine wanaojishughulisha na biashara hiyo.

Lakini pia, itapendeza iwapo barabara zitaachwa kwa ajili ya magari na zile za waenda kwa miguu zikabaki kwa ajili yao, kuliko kuvamiwa na wamachinga na kuzigeuza kuwa eneo la biashara tena zinazotandazwa chini na kusababisha usumbufu kwa wengine na uchafu wa mazingira na vyakula.