Kidato sita, wanavyuo mcheni Mungu kivitendo vita corona

29May 2020
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kidato sita, wanavyuo mcheni Mungu kivitendo vita corona

HATUANGAMII kwa neema ya Mungu tu, wala si kwamba sisi Watanzania ni wajanja sana ikilinganishwa na wenzetu, bali kwa kuamua kumlilia Muumba ametuhurumia.

Ni wazi tunapaswa kuendelea kumuomba na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya katika kudhibiti maambukizo ya homa kali ya mapafu Covid 19.

Hivi karibuni serikali ilitangaza wanafunzi wa kidato cha sita na vyuo warejee kuendelea na masomo. Ni uamuzi baada ya kufungwa shule na vyuo tangu Machi 17 mwaka huu, hatua inayolenga kudhibiti maambukizo ya ugonjwa unaoendelea kuitikisa dunia.

Ni wakati ambao wanafunzi wa kidato cha sita wanatakiwa kuonyesha uelewa wao kama wasomi, kwa kuzingatia taratibu za kujikinga na maambukizo hayo.

Korona imevuruga ratiba kwenye sekta nyingi, ikiwamo ya elimu. Vijana wa kidato cha sita walipaswa wawe wameshamaliza Mtihani wa Taifa sasa, wakihamia mchakato wa mengine kama vile kusubiri matokeo yao ya mitihani na kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), kwa mujibu wa sheria, kwa wale wateule.

Hali hiyo imesababisha maumivu fulani miongoni mwa vijana hao, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba ni janga la kimataifa. Hakuna aliyeliomba lituue, bali ndiyo mambo ya dunia yanavyoenda, kuna uzima, magonjwa na mauti.

Tayari serikali imeshatangaza ratiba mpya ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita, inayotarajiwa kuanza Juni 29 mwaka huu nchini kote na kumalizika Julai 16.

Nachukua fursa hii kuwasisitiza vijana hao, wahakikishe wanaendelea kumuomba Mungu kwa bidii, kama mamlaka za nchi na kiimani, pia wazazi wao wanandeleza.

Vivyo hivyo, pamoja washiriki kikamilifu katika kuzingatia taratibu na miongozo ya kudhibiti maambukizo, ili ratiba zao zikamilike kama ilivyopangwa na kukusudiwa.

Nawakumbusha kwamba, serikali imewaamini kwamba tayari wanauelewa wa kutosha, tofauti na wanafunzi wengine. Ndiyo maana, serikali imeruhusu warejee kumalizia ngwe yao, ili waendelee na ratiba za maisha mengine.

Ninukuu kidogo maneno ya kiimani yanavyotamka “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”

Katika huu ugonjwa wa corona unaosababisha vifo vya mamilioni ya watu, kuna mengi yasiyojulikana.

Tumeshuhudia vifo vya maelfu na mateso kwa wananchi hadi kwa nchi zilizoendelea kama vile Marekani , China na Italia hali licha ya juhudi kubwa na uwezo wa vifaa na ujuzi wavyotumia kudhibiti maambukizo hayo.

Rais Dk. John Magufuli, kwa kuwa na uhakika na nguvu na Mungu, ndipo alipoamua kuhamasisha wananchi kumuomba muumba huyo kwa bidii zikatengwa siku tatu maalumu za maombi, huku akikataa kuwekea vizuizi (lockdown) kwenye miji hasa Dar es Salaam, kwa kubainisha kuwa ni hatua itakayowazuia wananchi kujitafutia kipato.

Baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa waliinuka na kulaani hatua hiyo ya Rais Magufuli, aliyeamua kuchunguza uwezo wa vipimo vinavyotumika nchini kupima virusi vinavyosababisha ugonjwa huo na matokeo yameshaanikwa.

Ni wakati huu ambao wanafunzi wa kidato cha sita na vyuo wanapaswa kushiriki kikamilifu kudhibiti maambukizo hayo ili kuwezesha serikali kuruhusu wanafunzi wa madarasa ya chini, zikiwamo shule za awali na msingi kurejea darasani.

Miongoni mwa wanavyuo, wapo wanaopenda anasa, hivyo wanajisahaulisha kuwapo kwa ugonjwa huo, hivyo wanaendelea na maisha yao waliyozoea wakitumia uhuru pasopo mipaka waliowekewa, jambo linalohatarisha maisha yao na wengine kwa ujumla.

Baadhi ya wanajamii wamekuwa hawazingatii taratibu zilizowekwa katika kudhibiti ugonjwa huu. Inawezekana hiyo ikasababishwa na uelewa mdogo wa mambo, hasa yanayohusu afya na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Muhimu kila wanafunzi wa kidato cha sita na chuo, ahakikishe barakoa inakuwa miongoni mwa vazi muhimu kwa kila siku, kukumbuka kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kutumia vitakasa mikono(sanitizer).

Uwepo wa corona, umebadili taratibu za maisha, kama vile kusalimiana kwa kushikana mikono. Jamii iepuke kukumbatia na kushikana mikono wakati kuasalimiana marafiki ambao hamjaonana muda mrefu, furahieni kivingine, kukumbatiana marufuku.

Kidato cha sita na wanavyuo, dhihirisheni kuwa ni wacha Mungu na watu makini, kwa kushiriki kikamilifu kudhibiti maambukizo haya, hivyo kuwa mfano kwa jamii na kuonyesha tofauti ya uelewa mambo mlionayo.