Kigoda cha Mwalimu Nyerere kitumike kukuza Kiswahili

30May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kigoda cha Mwalimu Nyerere kitumike kukuza Kiswahili

TAMASHA la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, ni jukwaa la aina yake linalotumiwa na wasomi kutoa hoja na kujadili mada zinazohusu mambo ya Afrika na vikwazo vinavyoikabili.

Katika tamasha hilo la 11, pamoja na wasomi wengine kadhaa kuwasilisha mada zao, Profesa Patrick Lumumba kutoka nchini Kenya, alikuwa ni miongoni mwa wawasilishaji mada.

 

Anasema, kuna yanayoonekana kuwavutia wengi, kutokana na uwezo wake wa kuchambua mada kwa ufasaha.

Profesa Lumumba, mbobezi wa taaluma ya sheria, anaeleza kuwa Afrika imekuwa dhaifu, hivyo inakwama kushindana na mataifa mengine, kwa sababu imegawanywa na wakoloni.

Anabainisha kuwa Wachina ndiyo wanaojenga viwanja vya michezo Afrika. Je, hapa Dar es Salaam imejengwa na nani? Wamejenga kule Nairobi, Kenya, hata Uganda na nchi nyingi za Afrika wanaendelea kujenga?

“Hakuna chakula cha bure, Wachina wameshajua udhaifu uliopo Afrika, ndiyo maana wanaona njia nyepesi ya kushika ufahamu wetu ni kuwekeza hata katika taasisi za elimu ya juu,” anasema.

Profesa Lumumba anasema, hivi sasa China imeanza kupandikiza utamaduni wake, kwa kutumia lugha yake inayoweza kumeza utamaduni wa Afrika.

Anasema Kiswahili ni miongoni mwa zana zinazoweza kutumika katika mawasiliano ya Waafrika, katika masuala ya biashara na elimu, hivyo kuunganisha nguvu ya kuimarisha umoja kama ilivyo, kwa nchi za Ulaya zinavyotumia Kiingereza.

Ni vyema ifike wakati sasa, waandaaji wa Kigoda cha Mwalimu, wawe mfano wa kuendeleza nadharia za Mwalimu Nyerere kwa vitendo, kwa kuiwezesha lugha ya Kiswahili iwe ndiyo lugha kuu.

Nasema hivyo, kwa sababu lugha kuu inayotumiwa kwenye tamasha hilo ambalo mwaka huu limedhaminiwa na Uongozi Institute, taasisi ya Haki Elimu na Benki ya CRDB inatawaliwa katika lugha ya Kingereza.

Wazungumzaji wengine katika tamasha hilo, ni pamoja na mfanyabiashara mahiri, Ali Mufuruki, aliyezungumzia kuhusu mustakabali wa soko huria na dola.

Profesa Georges Ntalaja, raia wa Kongo anayeishi Marekani, alizungumzia dhana ya utawala bora na siasa, huku Profesa Paul Zeleza kutoka Malawi, Dk. Suzan Kavuma Uganda aliwasilisha mada kuhusu hali ya Uganda katika kuendeleza viwanda.

Watoa mada wote walitumia lugha ya Kiingereza kuwasilisha mada zao na kwa nadra miongoni mwao, ndio walidokeza Kiswahili.

Profesa Lumumba anataja methali ya Kiswahili kuwa ni “Vita vya panzi furaha ya kunguru.” Alitumia methali hiyo kuonyesha jinsi mgawanyo au migogoro kwa mataifa ya Waafrika, inavyoutumiwa vyema na mataifa ya kigeni kujinufaisha na rasilimali za Afrika.

Inatimu miaka 20 sasa, tangu kufariki Mwalimu Julius Nyerere, Oktoba 14, 1999. Miongoni mwa maono yake, ni kuona Afrika inakuwa na maendeleo na kumudu kujitegemea kiuchumi na kukuza lugha ya Kiswahili aliyoiamini inaweza kutumiwa vyema kuliunganisha bara la Afrika.

Hivi karibuni, vyombo vya habari kadhaa na mitandao ya kijamii, imebainisha kuwa Afrika Kusini  iliidhinisha lugha ya Kiswahili kufundishwa katika shule za nchi hiyo Septemba 2018, utekelezaji wake utaanza mwaka 2020.

Hatua hiyo ni fursa kwa walimu wa lugha ya Kiswahili kutoka Afrika Mashariki, hasa nchi za Tanzania na Kenya ambako lugha hiyo ni rasmi.

Ni wazi kuna wataalamu wa kutosha na wana sifa inayojitosheleza kwenda katika nchi hiyo kufundisha lugha hiyo maridhawa.

Kwa hiyo naamini, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu, Profesa Rwekaza Mukandala, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wakati fulani, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano  wa Umma, ataona umuhimu wa kutumia jukwaa hilo kukuza Kiswahili barani Afrika, iwe lugha kuu zaidi.

Natambua kwamba ni jukwaa linalokusanya wasomi kutoka mataifa mbalimbali, wakiwamo wasiojua lugha ya Kiswahili. Ni vyema wakawekewa watafsiri wa lugha, ili nao waanze kuona umuhimu wa kujifunza Kiswahili.