Kiini macho cha upungufu wa sukari kisirudi tena

13May 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kiini macho cha upungufu wa sukari kisirudi tena

TANGU kuadimika kwa sukari baadhi ya Watanzania ni kama wamesahau utamu wa chai.Wameshindwa kunywa chai kwa sababu ya kuadimika kwa bidhaa hiyo muhimu katika maisha yao.

Tabia hujenga mazoea.Watanzania wengi wana mazoea ya kunywa chai kama kifungua kinywa chao.

Matamshi mbalimbali yamekuwa yakitolewa yakilenga kuwatia matumaini watu kuwa bidhaa hiyo muda si mrefu itapatikana kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali, ikiwemo hivi karibuni kutangaziwa kuingizwa nchini zaidi ya tani 10,000 za sukari.

Hakuna mtanzania anayependa kunywa chai bila sukari, au mtoto wake aende shule bila ya kunywa chai, wakati kuna watu wachache wameifungia sukari kwenye magodauni kwa makusudi wakilenga kupata faida kubwa.

Baada ya sukari kuadimika mtaani Rais Dk. John Magufuli alitangaza ‘kiama’ kwa wafanyabiashara walioficha sukari kuwa atawanyang’anya na kuigawa bure.

Tamko hilo lililiamsha Jeshi la polisi na Takukuru kuanza kuwasaka watu hao,ili kuhakikisha kuwa wanachukuliwa hatua muafaka za kuwaezesha wananchi wanaendelea kunywa chai. Kinachoshangaza ni kwa nini Jeshi la polisi liamke baada ya kusikia tanko la mkuu wa nchi, hivi hawawezi kuchukua huku wakishuhudia wananchi wanaendelea kutesema siku hadi siku sukari ikiwa imefichwa?

Wwalikuwa wapi wakati sukari inafichwa na kusababisha uhaba mkubwa kwa wananchi, wanazinduka baada ya wananchi kuteseka kwa kiwango kikubwa? .

Nchi kama ya Uingereza ambayo ni gwiji wa uchumi wa soko wana sheria kali kwa wafanyabiashara au kampuni ikibainika kujihusisha na kuhujumu uchumi.

Mfanyabiashara au kampuni nchini Uingereza itakayofanya kile ambacho kinafanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa sukari nchini kwa kuficha sukari ili kulibadili soko la sukari au kupunguza/kuzuia ugavi (supply) kwa lengo la kupunguza ushindani wa soko, watakuwa wanakaribisha adhabu kali ya kifungo cha miaka mitano gerezani na/au faini isiyo na kiwango cha mwisho kwa mujibu wa sheria ya ushindani wa soko nchini humo..

Tanzania tuliona tatizo hili mapema na mwaka 1984 ikatunga sheria ya uhujumu uchumi.

Kuna wengine kwa kutofahamu au kutaka kupotosha umma wameanza kusema katika dunia ya uchumi wa soko, serikali haina madaraka ya kuingilia mwendo wa soko Kwa Tanzania, anachokifanya Rais Magufuli kiko ndani ya sheria ya uhujumu uchumi.

Tofauti ya Rais Magufuli ni kwamba, baadhi ya wananchi hawakuzoea kumuona Rais anayesimamia bila kutetereka sheria za nchi.

Kwa wale watakaopatikana na hatia ya kuficha bidhaa nchini kama sukari, sheria inasema kifungo chao ni miaka 15 gerezani.

Mwandishi mmoja wa Marekani aitwaye Neale Donald Walsch aliwa kusema, ‘’New life begins at the end of your comfort zone’’. Akiwa na maana kuwa ‘Maisha mapya huanza pale unapoamua kuondoka ulipozoea’

Rais Magufuli anawaondoa watanzania katika comfort zone iliyokuwa imejaa uzembe, wizi, ubabaishaji, ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma. Kwa sababu hii ndiyo maana kwa sasa tunasikia baadhi wanapiga kelele.

Mageuzi yoyote yana kipindi cha mpito ambacho kinakuwa ni kigumu sana, kutokana na mazoea ya kuishi kwa muda mrefu katika mfumo uliowafanya wananchi wakauzoea pamoja na kwamba umewafanya wapige hatua za kimaendeleo kwa kasi ndogo sana, zikilinganishwa na fursa zilizopo nchini.

Ombi langu kwa serikali ni kutowaonea huruma wafanyabiashara wa ana hiyo, ambao wanataka kuneemeka huku maelfu ya Watanzania wakitaabika kwa kusababishiwa matatizo kibao.

Hii ni haki kila bidhaa ipatikane kwa shida hapa nchini? Mafuta yawe ya shida, saruji iwe ya shida, vifaa vya ujenzi viwe vya shida, hata sukari nayo ipatikane kwa shida! Hapana sitaki kuamini kuwa serikali imeshindwa.