Kikulacho ki nguoni mwako'

30May 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kikulacho ki nguoni mwako'

“KIKULACHO huwa ndani ya nguo iliyo mwilini mwako.” Twakumbushwa kuwa mtu anayeweza kutudhuru ni yule anayetufahamu vizuri.

Aidha husemwa “Adui wa mtu ni mtu.” Kwamba binadamu huathiriwa na binadamu mwenzake. Hii ni methali ya kutukumbusha kuwa aghalabu matatizo tuyapatayo husababishwa na watu tunaoishi nao kila siku.

Damka/rauka kisha nenda kakae mkabala (tazamana) na klabu ya Simba au Yanga. Hapa utaona watu wa makundi mawili. Moja ni la muuza kahawa na la pili wanaelezana na kubishana kuhusu ubora na udhaifu wa timu.

Kundi hili ambalo hakuna yeyote aliyecheza kandanda, husimama mduara wakimzingira msemaji anayezungumza mithili ya chiriku!

Yanayozungumzwa hapo ni kuwasifu baadhi ya wachezaji na kuwasema vibaya wengine. Aidha huwasema viongozi wasiofaa na kuwasifu wengine wanaojali masilahi ya vilabu na wachezaji.

Kati ya pande zote mbili, wapo wanachama na wasio wanachama, yaani wanaofuata upepo. Watu wa aina hii huwa upande wa timu yenye mafanikio dhidi ya timu zingine, hasa hizi ziitwazo ‘watani wa jadi’ ingawa si watani ila ni mahasimu!

Idadi kubwa ya kundi hilo ni wale wanaofuata timu inayoshinda mara kwa mara na kuikimbia inayoshindwa. Hawa si wanachama ila ni mashabiki wanaofuata upepo kama bendera. Miongoni mwao hupenda timu kwa kuvutiwa na wachezaji fulani, kocha, wafadhili na baadhi ya viongozi.

Wanaowafuata viongozi ni wale wanaopewa nafasi za kuwa walinzi na kuitwa ‘makomando.’ Katika hali halisi komando ni kundi la askari wa jeshi kwa kazi maalum.

Eti wao hujiona bora kuliko wanachama wanaojitoa kwa hali na mali! Kwa hali hiyo, vilabu vitakuwa vikiwaneemesha baadhi ya viongozi na ‘makomando’ wao na kuvifanya kuwa tegemezi kwa miaka kadhaa.

‘Mfadhili’ ni mtu anayemfanyia wema mtu mwingine; mtu au taasisi inayosaidia mtu au jamii kwa fedha au vifaa kwa ajili ya kuendeshea mradi.

Yanga na Simba zimekuwa na wafadhili mbalimbali lakini ziko vilevile bila maendeleo ya maana. Zimebaki kuwa ‘omba omba’ mwaka hata mwaka kiasi cha kuwachosha wafadhili wao.

Kungekuwa na uangalizi makini, wallahi leo Yanga na Simba zingekuwa na maendeleo makubwa ya kuigwa na nchi jirani, kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Malawi lakini wajanja (nadhani tuwaite wezi) ndio wanaojinufaisha!

Baadhi ya wanachama hugombea nafasi za uongozi ili kujinufaisha badala ya kuzijenga Simba na Yanga zilizoundwa miaka kadhaa iliyopita. Yanga ilizaliwa mwaka 1935 ilhali Simba mwaka 1936 baada ya kutengana.

Nani aliyesikia mchezaji wa Azam FC akilalamika kwa kucheleweshewa fedha za usajili au kutolipwa mshahara wake kila mwezi? Ni timu pekee yenye viwanja vyake, gymnasium/gym yaani ukumbi wa michezo ya mazoezi ya viungo, zahanati na mambo muhimu yanayohusu afya ya wachezaji.

Tujiulize: Asingetokea MO Dewji, leo Simba ingekuwa hali gani? Hata huyu naye kuna wakati alitangaza kujitoa lakini baada ya kuombwa sana na baadhi ya viongozi wa ... (nachelea kuweka wazi) akakubali kurejea kundini.

Sasa alhamdulillahi (tamko la kuonesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu) mambo yanakwenda kisasa.

Kadhalika Yanga isingekuwa na udhamini wa GSM ingekuwaje? Kumbuka jinsi ilivyoitwa ‘omba omba’ iliposaidiwa na aliyekuwa kocha wao Mkongomani Mwinyi Zahera! Sasa Yanga wanapumua baada ya kampuni ya GSM kuingia ‘kundini’ na kuwafanya wawe na sauti mbele ya wale jamaa ... (msomaji nakuachia ujaze mwenyewe.)

Kuna mtu aliyeona mbele akataka kuifanya Yanga iwe ya kimataifa na kujitegemea, lakini alipoona haielekei na hata kutumiwa ‘makomando’ wamtukane yeye na familia yake, akawaachia klabu yao.

Mtu huyo hayupo nasi sasa kwani ametutangulia mbele ya haki. Mungu amrehemu.

Wahenga walisema: “Ushikwapo shikamana (ukichwewa na jua lala).” Maana yake unaposhikwa na mtu shikamana au nawe jitahidi. Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu aliyepatwa na tatizo kisha akapata mtu wa kumsaidia. Humhimiza ajikakamue au ajitahidi ili ajinasue.

Kadhalika yasemwa: “Usione kwenda mbele, kurudi nyuma si kazi.” Maana yake usijivune kwa kwenda mbele, unaweza kurudi nyuma wakati wowote.

Ngoja niwapooze: “Kujikwaa si kuanguka bali ni kwenda mbele.” Mtu anapojikwaa huwa si kwamba ameanguka ila huenda mbele. Hii ni methali ya kutumiwa katika muktadha ambapo mtu amekabiliana na tatizo fulani anapotenda jambo. Huweza kumhimiza asikate tamaa au asife moyo bali aendelee.

Yanga, Simba mpo?

Methali: Kukataa kwa chungu ni kuvuja.

[email protected]
0784 334 096