Kila king’aacho si, dhahabu

21Dec 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kila king’aacho si, dhahabu

KIGAE cha chupa kikiwa juani hung’aa. Hivyo isidhaniwe ni dhahabu inayochimbwa ardhini baada ya utafiti na kugundua uwapo wa madini hayo.

Hakuna madini yanayopatikana kirahisi. Mpaka kupata madini ya aina yoyote, watu hutoka jasho na wengine kupoteza maisha mpaka kuyapata.

Hata yanapopatikana huwa na kazi ya kuyasafisha na kuyatayarisha ili kuyapeleka sokoni.

Wahenga walisema: “Sihadaike na rangi, sifa ya chai ni sukari.” Maana yake usidanganyike kutokana na rangi ya chai, utamu wake hutokana na sukari. Methali hii hutumiwa kumkanya mtu asipumbazike au asivutwe na sifa za nje za kitu ila akichunguze kwa ndani.

Dirisha dogo la usajili wa wacheza kandanda lilifunguliwa rasmi nchini wakati nikiandaa makala haya. Kila timu, Simba imekuwa mbioni kufanya usajili wakati watani zao, Yanga tayari washasajili, lengo likiwa ni kujaza nafasi za wachezaji walioachwa, majeruhi au walioomba kuondoka baada ya kuona hawapati nafasi ya kucheza.

Halahala Simba na Yanga kukurupukia usajili mdogo au mkubwa. Mara nyingi imeonekana kuwa mwafanya hivyo kupimana uwezo wa fedha na umaarufu badala ya kuwapata wachezaji mahiri.

Matokeo yake, baadhi ya wachezaji hukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza na kuwekwa benchi kwa muda mrefu! Usajili haufanywi kwa papara (ukosefu wa umakini katika kufanya jambo) au kushindana na timu nyingine.

Hapa ndipo pa kujiuliza: Hao wanaowasajili wachezaji kisha kukosa nafasi za kucheza, kilichowavutia hata kuwasajili ni kitu gani? Timu zinazosajili wachezaji kuanzia wanne mpaka kumi maana yake ni kuwa wachezaji wote waliopo nchini hawafai! Si kweli.

Tatizo ni baadhi ya viongozi wa Simba na Yanga kuingilia kazi ya makocha (walimu) katika usajili. Hufanya hivyo ili wasajiliwe wachezaji watakaokubaliana nao kugawana sehemu ya fedha wanazotaka kabla ya kusajiliwa! Wahenga hawakukosea waliposema “Fedha fedheha.” Maana yake pesa huweza kuleta mambo ya aibu baina ya binadamu.

Hutumiwa kutuonya kuhusu maovu yanayoweza kusababishwa na pesa. Usajili ni kazi ya mwalimu baada ya kuona eneo fulani linahitaji mchezaji mbadala au msaidizi wa aliyepo. Endapo mchezaji aliyependekezwa na mwalimu ili asajiliwe kisha kutompanga kwa kutokuwa na sifa zitakiwazo, ni wajibu wa uongozi kumhoji kwa nini imekuwa hivyo.

Wachezaji hawatafutwi haraka haraka kama watu wachaguavyo nguo za mitumba. Wanaweza kufuatiliwa hata kwa mwaka mzima na zaidi, hasa wale wenye umri mdogo.

Hili laweza kufanyika kwa mafanikio kama klabu zitakuwa na timu za vijana watakaoandaliwa kuchukua nafasi za wakubwa watakaohitajika na timu zingine za ndani au nje ya nchi.

Tofauti na hili, klabu zetu zitakuwa zikitegemea wachezaji wa kigeni zaidi na kusababisha nchi kutokuwa na timu nzuri za taifa. Jambo lingine ni klabu kuwa na viwanja vyao vya mazoezi na mashindano.

Viwanja hivyo viwe na mahitaji yote muhimu kwa wachezaji: ukumbi wa michezo ya mazoezi ya viungo (gym), bwawa la kuogelea, zahanati, bwalo la kulia chakula, chumba maalum cha mafunzo ya ubaoni n.k.

Kadhalika, kuwe na vyumba vya kulala timu zitakapokuwa kambini kujiandaa na michezo ya mashindano badala ya kupanga kwenye hoteli kubwa na kulipa hela nyingi.

Ikumbukwe kuwa kupanga ni kuchagua. Yasikitisha kuwa viwanja vingi humu nchini vyaitwa ‘viwanja’ lakini kiukweli havistahiki kuitwa hivyo kwa jinsi vilivyochakaa.

Chama Cha Mapinduzi kimetwaa takriban viwanya vyote vikubwa vya kandanda nchini, lakini kimeshidwa kabisa kuviendeleza ila huvipamba kwa rangi zake tu!

Kama kimeshindwa kuviendeleza na kuvitunza, basi vikabidhiwe kwa mamlaka za miji na majiji. Wakati hayo yakifanyika, timu zinazoshiriki Ligi Kuu zishauriwe kuwa na viwanja vyao badala ya kutegemea vya wenzao au vya taifa. Azam FC imeweza hilo na sasa Simba nayo imefikia hatua hiyo.

Wale jamaa wa Jangwani (Yanga) walipewa uwanja kule Kigamboni jijini Dar es Salaam. Aliyewapa ni mpenzi kindakindaki (halisi) wa Simba, Paulo Makonda aliye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Yanga wasilaze damu kwani muda haumsubiri mtu. Ilisemwa na wahenga kuwa “Ngoja ngoja huumiza matumbo.” Maana yake kuambiwa “ngoja ngoja” kwa kuwa chakula kinaletwa huishia kuyaumiza matumbo kwa njaa.

Methali hii huweza kutumiwa na mtu anayeonesha kucheleachelea (-wa na hofu ya; -wa na wasiwasi wa) katika kufanya jambo kwani ni tabia inayoweza kumletea madhara baadaye. Methali hii inamhimiza mtu kutenda jambo alilokusudia.

Viongozi wa Yanga watambue kuwa wametwaa madaraka ya kuiongoza klabu hiyo wakati usio rafiki si kwao tu bali hata kwa wanachama na mashabiki wake. Wanapaswa kufanya kazi ya ziada kuitoa Yanga hapo ilipo na kuipeleka kwenye maendeleo.

Ninaposema maendeleo nina maana ya maendeleo ya kweli na ya kisasa. Klabu iondokane na ‘ombaomba’ kwa ‘kutembeza bakuli’ na badala yake iwe na wadau watakaoitoa kwenye ufukara uliokithiri ili ijitegemee yenyewe.

Wakumbuke kuwa penye nia pana njia. Kile kibanda kilicho makutano ya barabara za Mafia na Nyamwezi kivunjwe ili kujenga jengo refu la ghorofa 10 au zaidi.

Jengo hilo laweza kutumiwa kuwa hoteli na ofisi za mashirika na kampuni mbalimbali. Kama viongozi wamesahau, sasa nawazindua ili waufanyie kazi ushauri wangu.

“Penye nia pana njia.” Ikiwa mtu ana dhamira ya kufanya jambo fulani hawezi kuikosa njia. Hii ni methali ya kutumiwa kutukumbusha kwamba tuwapo na nia ya kufanya jambo lazima tutafanikiwa. Kazi kwenu viongozi wa Yanga.

[email protected] 0784 334 096