Kila la heri uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar

22Mar 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Kila la heri uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar

KWA mara nyingine uchaguzi wa kumpata Meya na Naibu wa jiji la Dar es Salaam unatarajiwa kufanyika leo baada ya kuahirishwa Jumamosi ya Februari 27, mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni zuio la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa zuio hilo lilikuwa feki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, akaagiza uchaguzi huo ufanyike kabla ya Machi 25 na kutaja sifa za wapigakura.

Uamuzi huo wa kutangaza tarehe na sifa za wapigakura unaweza kuwa ahueni kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo vilifurahia hatua kama hiyo.

Simbachawene aliwahi kuagiza uchaguzi huo ufanyike kabla ya Februari 29, lakini ukakwama mara tatu na sasa ameshasema kuwa utafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 13 (1) cha Kanuni za Kudumu za Jiji.

Waziri ameshatoa maelekezo kuwa mbali na madiwani, wapigakura wengine watakuwa ni wabunge wa kuteuliwa na Rais, ambao ni Dk. Philip Mpango, Balozi Agustine Mahiga, Dk. Ackson Tulia, Prof. Joyce Ndalichako, Dk. Abdallah Possi na Prof. Makame Mbarawa ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Tayari waziri Simbachawene alishawaagiza wakurugenzi wa manispaa za Kinondoni, Temeke na Ilala kuwasilisha kwa mkuruhenzi wa jiji la Dar es Salaam wajumbe halali watakaoshiriki katika uchaguzi.

Binafsi sina budi kuutakia heri uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam ili ufanyike kwa vyama kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kukubali matokeo ili visiendelee kusimamisha maendeleo ya jiji.

Maelekezo yameshatolewa na waziri mwenye dhamana kwamba watakaopiga kura katika uchaguzi huo ni madiwani wote wa halmashauri za jiji la Dar es Salaam ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni, wabunge wa kuchaguliwa na wabunge wa viti maalumu ambao mchakato wa kuwapata ulianzia kwenye mamlaka za halmashauri hizo.

Kwa maana hiyo hatutarajii kusikia ama kushuhudia mizengwe tena na badala yake apatikane Meya ili wawakilishi wa wananchi katika ngazi za maamuzi katika jiji la Dar es Salaam waweze kufanya kazi.

Tatizo kubwa la kuahirishwa mara kwa mara kwa uchaguzi huo ni mvutano baina ya CCM na Ukawa, hasa wa uhalali wa wajumbe halali wanaotakiwa kupiga kura.

Bahati nzuri waziri ameshautolea ufafanuzi, kwa maana hiyo kinatotakiwa kufanyika leo ni uchaguzi na sio tena zuio kama ambavyo imekuwa ikitokea hadi kufikia kuwapo kwa zuio feki!

Kuendelea kuzuia uchaguzi wa Meya ni kuchelewesha mipango mbalimbali ya maendeleo kwa jiji la Dar es Salaam na pia ni kuwapotezea muda wajumbe ambao wamekuwa wakitokeza kushiriki uchaguzi, lakini mwisho wake haufanyiki.

Mfano mojawapo ni kuahirishwa kwa uchaguzi wa Februari 27 kwa zuio ambalo baadaye mahakama ililikana kwamba halikuwa halali na kusababisha usumbufu kwa wapigakura.

Inasikitisha kuona wapo baadhi wanafikia kuisingizia mahakama kwa jambo ambalo halina ukweli ili mradi tu wafanikishe mambo yao. Nadhani kwa muda ambao wametumia kukwamia uchaguzi huo sasa unatosha, waruhusu ufanyike.

Ikumbukwe kuwa kura ni siri ya mtu, hivyo wengi pamoja wingi wao wanaweza kujikuta wakishindwa na pia wachache kwa uchache wao wanaweza kuibuka na ushindi, hasa kwa kuzingatia kwamba kura ni siri ya mtu.

Hivyo wanaokwamisha uchaguzi kwa sababu ya uchache wao, watambue kuwa wanaweza kushinda na pia wanaweza wakabwagwa kutokana na uchache, kwa maana hiyo lolote linaweza kutokea.

Cha msingi ni vyama vya siasa kuacha demokrasia ifanye kazi yake ili wachague viongozi wanaowataka bila kushawishiwa kwa chochote bali kwa tashi wao wenyewe Mimi ninaamini kwamba uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam bila mizengwe inawezekana, kinachotakiwa ni kuzingatia vifungu vya Kanuni za Kudumu za Jiji kama ambavyo waziri Simbachawene anavyoelekeza.

Wanasiasa watii kanuni, taratibu na sheria bila shuruti vinginevyo wataendelea kuyumbisha uchaguzi huo na kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa wananchi ambao tulifanya maamuzi Oktoba 25, mwaka jana.

Uzuiaji wa uchaguzi huo umekuwa ukizua maswali mengi kutoka kwa wananchi na kuhoji sababu za msingi za kukwamisha upatikanaji wa wa Meya kwamba wanasiasa wanaficha kitu gani ndani ya jiji hadi waisingizie uongo mahakama?