Kila la kheri Taifa Stars CHAN kesho

18Jan 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kila la kheri Taifa Stars CHAN kesho

AMEBAKI mchezaji mmoja tu ambaye alikuwa yupo kwenye michuano ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) iliyofanyika nchini Ivory Coast mwaka 2009 kuanzia Februari 22 hadi Machi 8. Si mwingine ni Erasto Nyoni.

Wengine wote 22 hawapo tena kwenye kikosi hicho, ingawa baadhi yao wanaendelea kucheza Ligi Kuu Tanzania, wengine wameshakuwa makocha na baadhi wameshataafu kabisa kucheza soka.

Imekuwa ni rekodi ya aina yake kuwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inarejea tena CHAN baada ya miaka 12, ikiwa na mchezaji ambaye pia alikuwapo kwenye kikosi hicho.

Mara ya kwanza kilikuwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo, lakini safari hii kimekwenda nchini Cameroon kikiongozwa na Mrundi Etienne Ndayiragije. Kesho kikosi hicho kitatupa karata yake ya kwanza kwa kucheza dhidi ya Zambia kesho.

Ikumbukwe kuwa hata mwaka 2009, Stars ilikuwa kundi moja na Zambia na katika mechi yao ya Kundi A zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Stars likifungwa na Shadrack Nsajigwa, hivyo kesho ina sababu zote za kuweza kuifunga Zambia na kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye Kundi lao D zikiwa pamoja na Guinea na Namibia.

Ukiliangalia kundi hili si la kutisha sana kama wachezaji wa timu hiyo wataamua kupambana, tofauti na lile la miaka 12 iliyopita lililokuwa na Zambia, Senegal na Ivory Coast.

Mara nyingi kwenye michuano kama hii ya makundi, ni vizuri zaidi kushinda mechi ya kwanza.

Ni mechi ambayo inawajengea wachezaji kujiamini, lakini pia pointi tatu zinazopatikana zinaifanya timu kuanza mahesabu yake kwenye mechi mbili zilizobaki, kama moja itoke sare yoyote vile, lakini inapopoteza inabidi kupambana ili kushinda mechi zote mbili kwa lazima.

Halafu pia hapo hapo linakuja lile suala la kuanza kuomba timu fulani ipoteze. Kitakachoibeba zaidi Stars kwenye michuano hii ni kwamba ina wachezaji wake wengi ambao ndiyo hao hao wanaunda timu ya jumla ya Taifa Stars ambayo inawajuisha pia wachezaji kutoka nje ya nchi.

Tunajua kuwa baadhi ya nchi zinazoshiriki michuano hiyo, huwa wanaita wachezaji zaidi ya asilimia 90 kama si 100 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, wakati mwingine hata wachezaji wa akiba watakuwa ni wa nje ya nchi.

Linapokuja suala la michuano ya ndani ya nchi wanakuwa na wachezaji ambao viwango vyao havitishi sana. Hii ni tofauti na Taifa Stars, ambayo haina hata wachezaji 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na mara nyingi tegemeo linakuwa kwa Mbwana Samatta na Simon Msuva tu, lakini mara nyingi wengi wanakuwa ni wale wale wanaocheza soka ndani ya nchi.

Kwa maana hiyo nataka kusema kuwa nchi nyingi kwenye CHAN zinaweza kuwa na kisingizio kuwa zilikosa wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi yao ndiyo maana hawakufanya vema kwa sababu hao ndiyo wanawategemea zaidi, lakini si kwa Stars.

Yenyewe hata kwenye kikosi cha jumla cha Stars kinatumia asilimia 90 ya wachezaji wa ndani, na kwa asilimia kubwa ndiyo hao hao ambao wako CHAN.

Huu ni wakati wa kuithibitishia Afrika na dunia kuwa kwa sasa Tanzania kuna vipaji ambavyo vinapaswa kumulikwa. Ni wakati vile vile kwa wachezaji wa Kibongo kujiunza kwani mara nyingi michuano hiyo, inakuwa imejaa mawakala kutoka nchi mbalimbali duniani.

Kuwapo kwa wachezaji wa kigeni wanaocheza soka kwenye Ligi ya Tanzania, pia kumesababisha wachezaji wa Kibongo kutokuwa na hofu sana wanapocheza na timu za kigeni tofauti na zamani ambapo walikuwa wanacheza wenyewe kwa wenyewe na wanakuwa wamezoeana.

Wanapokutana na wachezaji wa kigeni, wachezaji wengi walikuwa wana wasiwasi sana, lakini kwa sasa hilo halipo.

Tunawatakia kila la kheri Taifa Stars kufanya vema kwenye michuano hiyo ya CHAN kuanzia mechi ya kesho dhidi ya Zambia na zinazofuata pia.