Kinara wa darasa la nne anayepaishwa na ‘house girl’

02Feb 2016
Romana Mallya
Nipashe
Tesa
Kinara wa darasa la nne anayepaishwa na ‘house girl’
  • MARTHA BONAVENTURE

"NAMSHUKURU sana msadizi wa ndani wa nyumbani kwetu, Jenina Mdede, amenisaidia mambo mengi katika maisha yangu hususan kwenye masomo. Alinipa msukumo mkubwa wa kusoma na kunitaka kila nitokapo shule nijifungie chumbani nisome. Namuona kama dada yangu wa damu kwa namna alivyochangia maendeleo yangu ya kielimu," anasema Martha Nkwimba Bonaventure.

Martha (10) ni mshindi pekee wa kike kitaifa katika mtihani wa darasa la nne, 2015 katika wanafunzi kumi bora. Ni mwanafunzi ambaye sasa ameingia darasa la tano katika Shule ya Msingi Tusiime ya jijini Dar es Salaam.
Katika orodha ya washindi kitaifa, Martha alikuwa mwanafunzi bora wa tano kwa kupata ufaulu mzuri.
Akizungumzia siri ya mafanikio yake, Martha anasema kuwa anajivunia kupata dada mlezi anayejali elimu yake kwa kiwango kikubwa.
Mwanafunzi huyu ni mkazi wa Mbagala Zakhem anayeishi na wazazi wake anasema, anamchukulia Jenina kama dada yake wa damu kutokana na ukweli kuwa, wakati wote akiwa nyumbani amekuwa mstari wa mbele kumshauri ajisomee.
“Ananipenda na mimi nampenda. Hupenda nijifungie chumbani nisome. Hivi ni nani nitakayeweza kumshukuru zaidi yake? Amenijenga hivyo na nimekuwa nikitekeleza kwa vitendo,” anasema na kuongeza:
“Sasa hivi nimekuwa natimiza wajibu wangu, nikifika nyumbani bila kunishurutisha huwa natumia muda mwingi kujisomea na kujipa mazoezi. Pia napenda kusoma vitabu mbalimbali ambavyo vinaniongezea ujuzi na maarifa. Nina furaha ya ushindi kwa ajili yake,” anasema Martha.
Mwanafunzi huyo kimwonekano anajiamini na mwenye uwezo wa kujenga hoja na kuitetea, anaendelea kusema, “Nimeishi naye sasa ni mwaka wa nne, sitamani aondoke ili aone matunda yangu.”
Kimsingi Martha anaamini kuwa dada huyo ni tofauti na wengine wanaoishi kwa watu wengine, kwa sababu ameitambua thamani ya elimu yake kama wanavyofanya wazazi wake.
Msichana huyo anasema, endapo angebweteka nyumbani bila kufanya mazoezi na kujisomea, haamini kama angefanya vizuri kwenye mtihani huo, kwa sababu ushindani katika shule yake na nyingine ulikuwa mkubwa.
“Unajua hakuna anayetamani kufeli, lakini hutokea kwa sababu ya kupunguza juhudi za kujisomea. Nilikuwa na mpinzani darasani kwetu, ambaye kila nikifika nyumbani nilikuwa nakazana kusoma ili nimshinde, ndoto yangu sasa imetimia,” anasema.
Dada Jenina ambaye amehitimu kidato cha nne, akimzungumzia mtoto huyo anasema kwamba ni mwenye kutambua thamani ya elimu kwa mtoto wa kike na mwenye wivu wa mafanikio yake kielimu.
Miongoni mwa masomo anayoyapenda ni Hisabati, Sayansi na Uraia ambayo mara zote amekuwa akiyasoma ili ufaulu wake uwe kwa kiwango cha juu.
“Natambua wanafunzi wengi wamekuwa wakiyaogopa masomo haya na wamekuwa wakifeli… naamini juhudi binafsi ndizo zitakazotuwezesha kuyafaulu,” anafafanua.

Ratiba yake ya masomo
Martha anasema, kila siku akiamka kabla ya kufanya kitu chochote kile anapiga magoti na kumuomba Mungu ili aweze kumtangulia kimasomo na maisha kwa ujumla.
Baada ya kuamka saa 11:00 alfajiri husali kisha hujiandaa kwenda shule.
Anasema, hupenda kujiandalia kitafunwa mwenyewe, hivyo baada ya maandalizi yake ya shule kukamilika hutumia muda uliobaki kabla ya kuondoka, kunywa maziwa na mkate.
Martha ana utaratibu wa kila siku kuondoka nyumbani kwenda kituoni kusubiri basi la shule saa 11:30 alfajiri. Na hutumia muda wa njiani kulala hadi shuleni, ili kuepuka kusinzia akiwa darasani.
Martha anasema, katika vitu anavyoheshimu ni ratiba ya nyumbani na shuleni, aliyowekewa na wazazi wake ya kuhakikisha kuwa anaamka na kulala mapema ili asichelewe shule.

Maisha ya shuleni
Siri kubwa iliyomfanya afaulu na kushika nafasi ya tano kitaifa akiwa msichana pekee, ni kuhakikisha kuwa anamsikiliza mwalimu kwa makini, na pale anapokuwa hajaelewa anamfuata mwalimu wa somo husika.
Anaongeza kuwa, alianza kuwa na wivu wa kutaka kufaulu kwa kuwa darasani kwao, kulikuwa na mwanafunzi aliyekuwa anachuana naye na alitamani siku moja amshinde.
Kutokana na kupenda kujisomea nyumbani anasema kuwa imemsaidia darasani kuelewa kile kinachofundishwa na walimu wake.
Kuhusu mahusiano na wenzake darasani, Martha anasema anajitahidi kushirikiana nao ili kubadilishana uzoefu kwa kuwa anapata fursa ya kujifunza kutoka kwao.
Ili kupata uelewa zaidi darasani, kila anapopata muda amekuwa akisoma mambo mapya, ambayo hawajayafikia wala hawajafundishwa darasani kwao.
Martha ni mtoto anayejali muda na katika kudhihirisha hilo, wakati tukiendelea na mahojiano, kengele ya darasani ilipolia alinyanyuka na kuniomba arudi darasani ili asikose kipindi.

Wazazi wake
.
Martha akiwazungumzia wazazi wake, Martha anasema kuwa ni watu wanaojali elimu yake kwa kiwango kikubwa, kwa sababu anapotaka vitabu vya kujisomea wamekuwa wakijitahidi kumpatia.
Anasema kila anapofanya vizuri darasani, wazazi wake wamekuwa wakimpa zawadi mbalimbali, zikiwamo vitabu.
Anaongeza licha ya kutambua mchango wa dada yake Jenina, wazazi wake wana mchango mkubwa na wamekuwa wakimhimiza apende masomo wakati wote.
Miongoni mwa watu wa tatu anaowashukuru kwa kumlea na kumfundisha vizuri, ni walimu wake hususani wa masomo ya hesabu, sayansi na uraia.

Nje ya masomo
Martha anasema akiwa nyumbani anapenda kujifunza kupika vyakula mbalimbali na amekuwa akitumia muda mwingi kukaa na msaidizi wao wa ndani, ili ajifunze namna ya kupika vizuri.
Mambo mengine anayopenda ni michezo kama vile kuruka kamba, kukimbia na sarakasi kwa kuwa anaamini kwamba ndiyo yanayomjenga kimwili na kiakili.

Ndoto zake za baadaye

Kimsingi ndoto za Martha ni kusoma kwa bidii ili siku moja afike Chuo Kikuu kisha baadaye afanye kazi kwenye taasisi za fedha kama mhasibu.

Akiwa mkubwa na kuanza kazi anasema kuwa atahakikisha anapambana na suala la rushwa kwa kuwa anaichukia na kwamba hatapokea wala kutoa rushwa.
Anasema anatamani kusoma kwa bidii ili afanye vizuri katika mitihani yake ya darasa la saba mwaka 2018.

Kauli ya mama yake
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Shilwa Mboma, anasema ni mtoto wa pekee ambaye amekuwa akipenda kusoma kuliko vitu vingine na kwamba, muda mwingi amekuwa akiutumia kujisomea hali iliyomsaidia kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu darasani tangu aanze shule.

"Tumekuwa tukimuhimiza mara kwa mara asome. Baba yake amekuwa akimwambia asiposoma hatakuwa rafiki yake. Naona nayo ni moja ya jambo linalomfanya aongeze bidii. Akifanya vizuri darasani ukimwambia unataka zawadi gani, anasema vitabu. Licha ya umri mdogo alionao, lakini hadi sasa amesoma vitabu vingi huwezi amini," anasema.
Kuhusu msadizi wake wa ndani, Shilwa anasema amekuwa kiongozi mzuri kwa watoto wake.
"Kazi zetu unazijua za Newsroom, unatoka saa 3:00 usiku lakini nikirudi nakuta amewasimamia watoto wamefanya kazi zao za shuleni, binafsi namshukuru Mungu kwa hilo," anasema.

Mwalimu wa darasa

Aliyekuwa Mwalimu wake wa darasa la nne katika shule ya msingi Tusiime, Fredy Nkwasibwe, anasema mtoto huyo anapenda kudadisi mambo mbalimbali kwa lengo la kutaka kujifunza.
Anasema napenda kuwa mshindi katika masomo yake na inapotokea mtu akamshinda, huongeza bidii ili aendelee kuwa juu.
Nkwasibwe anasema msichana huyo mara zote hujiamini kwa kile anachofanya na hilo amejengewa na walimu ambao hutaka kila mtoto ajiamini.
"Utaratibu tulionao tunapenda kuwajengea uwezo wa kujiamini watoto kupitia mada ambazo hutayaarishwa na walimu na mwanafunzi anaziwasilisha mbele ya kadamnasi," anafafanua.

Kuhusu siri ya ufaulu anasema, walimu hutumia muda mwingi kutoa mitihani kwa ajili ya kuwapima wanafunzi kabla ya kufanya mitihani ya mwisho wa kumaliza muhula mmoja.

Anaongeza kuwa matokea ya mitihani hiyo hubandikwa na kwamba hatua hiyo huwafanya wanafunzi kutambua uwezo wao na nini wanatakiwa kukifanya ili safari nyingine wasipate alama za chini.

Mwisho