Kinywa jumba la maneno

30Dec 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kinywa jumba la maneno

KINYWA cha binadamu ni kama jumba la maneno. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kuwa binadamu ana uwezo wa kusema maneno yoyote yawe mazuri au mabaya. Hatupaswi kushangaa tusikiapo fulani kasema maneno fulani.

Kabla ya mechi ya leo Jumamosi baina ya Mbao FC ya Mwanza wakiwakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, kwenye uwanja wa Kirumba jijini Mwanza, mechi ilianza ‘kuchezwa’ nnje ya uwanja.

Wachezaji na makocha wa timu hizo walianza ‘kucheza’ nnje ya uwanja kila upande ukijitapa kuuadhibu mwingine. Kiungo wa kimataifa wa Yanga, Mkongomani Pappy Kabamba Tshishimbi amenukuliwa na gazeti moja la michezo akiwaambia Mbao “wajiangalie kwani ana kazi nao.”

Naye kocha wa Mbao FC hakukosa neno la kuwaogofya wapinzani wao kwani alisema haihofii Yanga kwani haoni jipya kwao (Yanga) na kwamba ni timu ya kawaida kama zingine.

Bila shaka huyu anajivunia matokeo ya mechi mbili alizokabiliana na Yanga msimu uliopita jijini Mwanza. Mechi ya kwanza Mbao iliiadhibu Yanga kwa bao 1-0. Na timu hiyo ndio iliyoivua Yanga ubingwa wa Kombe la Azam Federation kwa kuifunga tena bao 1-0 palepale Kirumba, Mwanza.

Timu hizo zilipokutana mara ya pili kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Yanga ililipa kisasi kwa kuifunga Mbao FC mabao 3-0.

Mwishowe Simba ndio iliyotwaa Kombe la Azam Federation mjini Dodoma kwa kuifunga Mbao FC kwa penalti ambao nayo imeondoshwa na timu ya daraja la pili kwa mikwaju ya penalti 4-3. Ndio yale ya ‘mdharau mwiba mguu huota tende!’

Katika hali kama hii, magazeti ya michezo nayo hutumia nafasi hiyo kuandika vichwa visivyoendana na maelezo yake. Lengo ni mradi magazeti yanunuliwe haraka! Wasichoelewa ni kwamba wanavunja hadhi ya machapisho yao kwa wasomaji kutokana na tamaa zao.

Ni kama wauza matunda wanaouza maembe ya kupepea na kuwasifia wanunuzi kuwa “ni maembe ya mdondo tena ya leo leo” kumbe yalianguliwa kabla ya kukomaa, yakafukiwa ardhini na kuwashwa moto juu ili yaonekane yameiva!

Na kweli ukiyaangalia yanavutia kwa wekundu wake kumbe kila king’aacho si dhahabu lakini ndio umeshayanunua. Ukila unakumbana na ugwadu usiotarajia!

Hebu soma kichwa hiki: “Yanga yabadilisha silaha kuiua Mbao.” Hapana shaka mashabiki wa pande zote mbili walikuwa na shauku ya kutaka kujua ‘silaha zilizobadilishwa’ na Yanga ili kuiua Mbao.

Habari hiyo yenye paragrafu 10, hakuna hata moja inayoeleza Yanga kubadilisha silaha ili kuiua Mbao FC! Zaidi ni viongozi wa Yanga kutokuwa na uhakika kama wachezaji wao wangesafirishwa kwa basi lao au eropleni (ndege)!

Tukiachana na hilo la timu kutambiana, sasa tuone jinsi magazeti ya michezo yanavyoandika vichwa tofauti na habari/makala zao ili kuvuta wasomaji.

“Kocha mpya Simba huyu hapa.” Chini ya kichwa hicho imeandikwa hivi: “Simba wamemtimua kocha wao mkuu Joseph Omog na sasa wanataka kushusha kocha mwingine ambaye CV yake wakiiona wapinzani wao, itawatetemesha na kuwakatisha tamaa kabisa ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.”

Habari hiyo ina paragrafu 17 lakini hakuna hata moja kati ya hizo inayomtaja huyo kocha aliyeelezwa na kichwa cha habari kuwa “Kocha mpya wa Simba huyu hapa!” Yu’wapi? Ni nani? Hakuna aliyetajwa rasmi kuwa kocha mpya wa Simba!

Mwisho wa habari hiyo, gazeti linajikanganya lenyewe kwa kuandika: “ … (jina la gazeti) lilijaribu kuwatafuta viongozi wa timu hiyo ili kuzungumzia jambo hilo, lakini simu zao zikawa hazipokelewi na hata alipopatikana msemaji wao, Hajji Manara, hakutoa ushirikiano.”

Gazeti hilo pia lilikuwa na kichwa kisemacho: “Joseph Omog aondoka na faili la siri.”

Maelezo ni kuwa “Wakati kikosi hicho kikitarajiwa kuondoka muda wowote, kocha huyo msaidizi (Djuma) amekiri kwamba haijui Ndanda hata kidogo na alitarajia kupata mbinu za kuwaua wapinzani wao hao kutoka kwa Omog, lakini kabla hawajazungumza lolote akasikia bosi wake huyo ametimuliwa.”

Sasa kocha Omog ameondoka na ‘faili la siri’ au ameondoka na siri ya kuifunga Ndanda FC? Faili ni jalada la kutunza karatasi zenye kumbukumbu ya mambo fulani.

Mara nyingi magazeti ya michezo huzitumia timu za Simba na Yanga ili yanunuliwe kirahisi. Kama nilivyoeleza hapo juu, vichwa vya habari hutofautiana kabisa na habari/makala zinazoandikwa!

Wahenga walisema: “Jawabu wakatiwe, na wakatiwe si zani.” ‘Zani’ ni fujo au ghasia. Maana yake kila jawabu au jibu huwa na wakati wake na ufikapo huwa halisababishi fujo au mabishano yoyote.

Methali hii yatufunza umuhimu wa kuyasema mambo wakati unaofaa na wakati yanapoweza kukubalika bila ya kuleta mabishano.

Kuna baadhi ya wasomaji walionitumia ujumbe mfupi wa simu (sms) kuniambia siku hizi hawasomi magazeti ya michezo kwani ushabiki, porojo na uongo ni mwingi kuliko uhalisia wa mambo yanayoandikwa!

[email protected]

0715 334 096 / 0622 750 243