Kipendacho moyo ni dawa

04Apr 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kipendacho moyo ni dawa

KITU anachokipenda mtu au inachokipenda roho ya mtu huwa kama dawa yake.

Methali hii yaweza kutumiwa kumpigia mfano mtu anayeelekea kukipenda kitu fulani sana ingawa wengine wanakiona kibaya.

Wengine husema “Kipenda roho hula nyama mbichi.” Maana yake roho ikipenda huweza kula hata nyama mbichi. Matumizi yake ni sawa na “Kipendacho moyo ni dawa.”

S.A. Mohamed ameandika hivi kwenye kitabu chake cha Vito vya hekima, Simo na Maneno ya Mshangao: “Pavumapo palilie si kazi kudamirika*.

*Damirika ni kitendo cha kitu au maisha ya mtu kuharibika kabisa; fisidika. ‘Damiri’ ni angamizwa kabisa; haribikiwa.

Duniani kuna vyakula vya aina nyingi lakini si vyote vinavyopendwa na watu wote. Kwa mfano kuna wasiokula nyama ya kondoo, bata, mbuzi wala utumbo. Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwao.

‘Mchezo’ ni jambo ambalo watu au timu hulifanya kwa kushindana ili kupata mshindi. Kwa mfano, mpira wa miguu uliopewa majina mengi: kandanda, kabumbu, soka, dimba n.k., watu huhitilafiana kila mmoja akiwa na sababu zake.

Mfano mzuri ni wale wanaojipaka rangi za bendera za timu zao, kujiandika kwenye miili yao na wengine kuvaa vitu vya ajabu ajabu kuonyesha jinsi wanavyozishabikia timu zao.

Mbali na hayo, kuna wanaopigana uwanjani, wanaong’oa viti wanavyokalia, wanaolia na kutoa machozi, wanaozirai na waliopoteza maisha!

Kadhia (jambo linalojiri; tukio la kuhuzunisha) hii hutokea wakati timu zao zinapofungwa, hasa na wapinzani wao. Hii hutokea mara kwa mara zipambanapo Yanga na Simba.

Hata hivyo yanipa shida kubainisha (kitendo cha kutofautisha miongoni mwa vitu au watu) kama hali hiyo husababishwa na mshituko wa moyo timu zao zinapofungwa au ni kutokana na kupoteza dau (fedha au kitu anachoahidi mtu kutoa kwa timu itakayoshinda).

Ndo maana wahenga walisema: “Tamu ikizidi tamu huwa si tamu tena.” Methali hii hutumiwa kutukumbusha kwamba jambo lolote zuri huwa na mipaka. Linapozidi huwa halivutii tena.

Sasa ni kwa nini baadhi ya watu hupenda sana timu fulani? Mara nyingi, katika mchezo wowote watu humpenda mchezaji anayefanya vizuri kwenye mashindano.

Mchezo wa ngumi, kwa mfano, watu walimpenda mno Mohamed Alli (Mungu amrehemu) wa Marekani aliyekuwa bingwa wa mchezo huo duniani. Hata waliokuwa hawaupendi mchezo huo walijikuta wakiupenda kwa sababu ya Mohamed Alli.

Baada yake alifuatia bondia Mike Tyson pia wa Marekani aliyetikisa ulimwengu wa masumbwi kama alivyokuwa marehemu Mohamed Ali. Kadhalika alipendwa na wengi duniani.

Nchini Tanzania kuna waliopendwa na wengi ila sasa anayezungumzwa na kupendwa na wengi si mwingine ila ni mgosi Hassan Mwakinyo wa Tanga anayeitangaza nchi kwa mchezo huo wa ngumi.

Sababu ya wachezaji au timu kupendwa hutokana na juhudi na ushindi hivyo hupendwa na wengi ingawa katika hao wapo wanaofuata mkondo tu. Mchezaji akishuka au timu ikipoteza mwelekeo, baadhi ya watu huhamia kwingine!

Timu ya Manchester United ya Uingereza ilitikisa ulimwengu wa soka hata mwalimu wao, Alex Ferguson akatunukiwa jina la ‘Sir’ na Malkia Elizabeth wa nchi hiyo.

Humu nchini timu zenye mashabiki (watu wenye mapenzi na hamasa kubwa) wengi ni Yanga na Simba. Wingi wa mashabiki wao ni tofauti na wanachama wenye kadi na waozichangia timu hizo, mbali ya wale wanaozisaidia kwa hali na mali.

Mashabiki wengi wa timu hizi wanapoona hazifanyi vizuri, huzikimbia kwani wanachotaka ni ushindi tu! Hawajui kuwa kuna sare (kufungana idadi sawa), suluhu (kutofungana) kushinda na kushindwa?

Wahenga walirahisisha zaidi waliposema: “Hakuna mume wa waume.” Maana yake hakuna mtu mmoja anayeweza kuwashinda wanaume wenzake wote. Methali hii hutumiwa kwa mtu anayejitia ubabe au anayejidai kuwa na nguvu kama njia ya kumnyamazisha.

Yanga ndio waliozitesa timu zingine, kwa kuwa mabingwa mara nyingi mpaka kuitwa ‘mabingwa wa kihistoria.’ Upepo umebadilika na sasa timu inayotamba nchini ni Simba, wanaoitwa ‘mnyama wa Msimbazi’ kwa mwaka wa tatu mfululizo wakati Yanga wakisota kwa kipindi kama hicho bila kuwa bingwa!

“Kupata kuna Mungu.” Mtu anayetaka kufanya jambo hushajiishwa na msemo huu. Haifai mtu kusitasita katika kuomba jambo au kupigania jambo. Ni bora mtu kuondoa wasiwasi. Woga na ujasiri wa kuona labda hatofuzu. Tukijaribu matendo ya ujasiri, mbele yetu tumweke Mungu. Yeye ndiye atoaye na ndiye anyimaye.

[email protected]
0784 334 096