Kipindupindu kiwe jukumu binafsi, isiachiwe serikali tu

07Aug 2019
Moses Ismail
Nipashe
Mjadala
Kipindupindu kiwe jukumu binafsi, isiachiwe serikali tu

NIANZE kuzungumzia hili kwa kuzitalii takwimu zilizotolewa na Naibu Waziri wa Afya, Faustine Ndugulile, kwamba kufikia Juni 17 mwaka huu watu sita walishafariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine 391 wakiwa wamepata maambukizi ya ugonjwa huo na kupewa tiba.

Nionavyo mie idadi hii ya waliofariki na waliopatwa na maambukizi, inaweza kuonekana ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa na idadi ya watu waliofariki kwa ugonjwa huo kwa takwimu za miaka iliyopita.

Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka jana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, katika kipindi cha mwezi wa Machi tu mwaka jana idadi ya wagonjwa wa kipindupindu ilikuwa ni watu 1,448 huku idadi ya vifo ikiwa ni 27 tu.

Ukilinganisha na idadi hii ya takwimu za Juni 17 mwaka huu, utaona kuna udhibiti mkubwa wa maambukizi ya ugonjwa huo pamoja na vifo vitokanavyo na madhara yake.

Hata hivyo, ugonjwa huo wa mlipuko una tabia ya kujirudia tena katika kila kipindi cha majira ya mvua za mwaka kwa kusababishwa na mifumo mibovu ya udhibiti wa mifumo ya maji machafu ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ugonjwa huo.

Kwa tabia yake ya kujirudiarudia kwa majira hayo ya mvua kila mwaka, nategemea kuwa pengine idadi hii ya wagonjwa 391 na vifo vya watu 17 iliyotolewa sasa na Naibu Waziri, vinaweza kuongezeka na pia naomba Mungu aepushe hilo.

Kwa mujibu wa maelezo ya matabibu ugonjwa huu, unaoweza kuua haraka, husababishwa na bakteria wanaofahamika kwa jina la kitaalamu kama vibrio cholera.

Ni bakteria wanaozaliwa na kuishi kwenye kinyesi cha binadamu na huwa hatari zaidi pindi mtu anapokunywa maji au chakula kilicho na bakteria hao.

Vilevile ugonjwa huu huambukiza kwa mtu kugusa matapishi au kinyesi cha mgonjwa wa kipindupindu bila ya kuwa na kizuizi.

Inashauriwa wenye kuwasaidia watu walioambukizwa ugonjwa huu nao wapatiwe dawa za kuwazuia kupata maambukizi.

Kwa miaka mingi serikali imekuwa ikitoa elimu ya watu kujikinga na ugonjwa huo kupitia wataalamu wake wa afya na kuendesha kampeni za vipindi vya radio, televisheni na hata makala za magazeti kila unapofika msimu wa mvua ili watu wajikinge na balaa la kipindupindu.

Nimeshuhudia tangu nikiwa bado mdogo kampeni za kuudhibiti ugonjwa huu kwa mafunzo maarufu ya kuchemsha maji ya kunywa kabla hujayanywa, kunawa mikono kila unapotoka chooni, kuosha matunda kabla ya kula na mafunzo mengine kadha wa kadhaa ili kuepuka ugonjwa huo.

Lakini hata hivyo, pamoja na kampeni hizo, bado mlipuko wa ugonjwa huo unaendelea kujitokeza mwaka hadi mwaka ingawa athari zake si mbaya kama zile za miaka ya 1978 hadi miaka 1980 ambapo watu wengi waliougua kipindupindu waliweza kuwaambukiza ndugu zao na kusababisha madhara kuwa makubwa zaidi.

Unapowasikiliza watu na kutafuta maoni yao juu ya swali hilo, utagundua wana ufahamu mkubwa tu wa sababu za maambukizi na pia namna ya kuukwepa ugonjwa huo.

Watakuambia ni kwa sababu ya kukosa maji salama ya bomba vijijini na baadhi ya miji, kutokuwa na miundombinu ya maji kupitisha majitaka katika maeneo mengi, kukosa vyoo salama na sababu nyingine nyingi ambazo kimsingi zinaonyesha kuwa tunafahamu sababu za ugonjwa huo.

Katika hali kama hii ndipo Mjadala unapojiuliza, iwapo tunafahamu kuwa maji yasiyo salama ni hatari kwa kuyanywa au hata kuyakanyaga, kujisaidia ovyo vichakani au kwenye mito kunaleta kipindupindu, kwa nini basi tusikabiliane na mambo hayo? Tunasubiri nini?

Kwa vyovyote iwavyo ni kwamba jukumu la kujizuia na maambukizi ya kipindupindu bado lipo mikononi mwa kila mmoja wetu na bahati nzuri serikali kwa upande wake imeshatimiza kwa kiwango kikubwa jukumu lake la kutoa elimu ya kujilinda na ugonjwa huo.

Iwapo tutazingatia mafunzo yaleyale ya msingi ya kujiepusha na kupindupindu kama vile kuchemsha maji kabla ya kuyatumia, kujisaidia ovyo vichakani au kwenye mito, kuosha matunda kabla ya kula na kuwahi hospitalini kila mtu anapopatwa na ugonjwa wa kuhara na kutapika, basi tutaudhibiti ugonjwa huu.

Mjadala unasema ni ukweli uliodhahiri kuwa serikali imeshatimiza wajibu wake wa kutoa elimu juu ya ugonjwa huu na inaendelea kufanya hivyo.

Jukumu kubwa linabaki kwetu sisi wananchi kuamua kupambana na sababu na vyanzo vyote vya maambukizi ya ugonjwa huu ili kulinda afya zetu na kuokoa maisha yetu.