Kipunguni ‘A’ wahoji hatima yao serikalini

02Jul 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Kipunguni ‘A’ wahoji hatima yao serikalini

KWA takriban miaka 22 sasa, wakazi wa Kipunguni ‘A’ wanaopakana na uwanja wa ndege wa kimataifa uliopewa jina la Mwalimu Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam, wanaishi kwa wasiwasi wa kutojua hatima yao.

Wananchi wa Kipunguni ‘A’ wameishi eneo hilo kabla ya ujenzi wa uwanja huo wa ndege (Terminal 1) na sasa kuna Terminal 2, ilhali Terminal 3 yategemewa kuzinduliwa rasmi na Rais Magufuli hivi karibuni.

Waliishi wakitegemea mifugo (ng’ombe, mbuzi, kondoo, mabata na kuku), kilimo cha mpunga, mboga za aina mbalimbali na minazi iliyowapatia madafu na nazi. Kwa wanywa vileo, waliburudika kwa tembo kwa kugema tunda, ua la mnazi kabla halijachanua.

Mwaka 1997 eneo hilo lilithaminiwa na mkadiria thamani binafsi kwa namna iliyowashangaza wakazi wake kwani hakukuwa na tangazo la indhari (tahadhari juu ya jambo) kuhusu wakazi wa eneo hilo kuhamishwa ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege! Hakuna mkadiria thamani aliyeingia ndani ya nyumba za wakazi kujihakikishia thamani yake bali ukadiriaji ulifanywa kwa kuangalia nyumba kwa nje tu!

Vivyo hivyo hakuna aliyeambiwa thamani ya nyumba na mimea iliyokuwa katika eneo lake bali alifahamishwa kwa mdomo tu kuwa angelipwa baada ya miezi sita, bila kutajiwa kiasi atakacholipwa!

Wananchi walishtushwa na kushangazwa kwa tangazo la Serikali Na. 23 ya mwaka 2000 kuwa eneo linalouzunguka uwanja wa ndege wa kimataifa jijini Dar es Salaam ni eneo la mipango miji, ikiwemo Kipunguni ‘A’.

Hali hiyo ilisababisha wakazi 325 wa Kipunguni ‘A’ wafungue kesi mahakamani ili kujua kama hatua iliyochukuliwa na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege ilikuwa sahihi ama la; vilevile hatima yao ya kuishi kwenye maeneo yao itakuwaje kutokana na tangazo lilitolewa na Serikali.

Kesi iliendeshwa na baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote, ikatoa hukumu Novemba 30, 2017 kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

Je, Waliowasilisha madai mahakamani ni wakazi halali wa eneo husika na kama wameyaendeleza, zikiwemo nyumba wanazoishi? Kwa hiyo baada ya mahakama kusikiliza hoja na ushahidi wa pande zote mbili, iliamua kuwa waliowasilisha madai, yaani wananchi wakazi 325 waliofungua kesi mahakamani, wapo kihalali kwenye maeneo yao na pia wameyaendeleza.

Je, utaratibu uliotumika kutwaa eneo hilo la ardhi kwa mujibu wa G.N. 23/2000 ulikuwa halali? Kuhusu hoja hii, mahakama iliangalia kwa kina sheria na taratibu zilizotumika, na kwa kuzingatia hoja na ushahidi wa pande zote mbili, iliamua kuwa utaratibu wa kutwaa eneo husika haukuzingatia sheria, hivyo ni batili.

Je, utaratibu wa kufanya tathmini na kukadiria fidia ulizingatia sheria? Baada ya mahakama kujadili kwa kina hoja hii, mwishowe ilifikia uamuzi kuwa haikuwa sahihi kufanya tathmini ambayo sio ya haki au isiyo na kiuhalisia hivyo ikaelekeza tathmini ifanywe upya kwa kuzingatia bei ya sasa ya soko ya mali za walalamikaji waliowasilisha madai.

Je, wananchi waliowasilisha madai wanastahiki kulipwa fidia kwa hasara wanayoendelea kupata kwa kipindi chote wanachokuwa katika hali ya sitafahamu (hali ya kutoelewana au kusikilizana) ya kuhamishwa au hapana?

Mahakama haikuridhishwa na hoja zilizotolewa na walalamikaji kwani hawakuthibitisha ni kwa kiasi gani walizuiwa kufanya maendeleo katika maeneo yao au kutumia mali walizo nazo kuombea mikopo katika taasisi za fedha ili kuiridhisha Mahakama kuwa ni kweli wanastahiki fidia wanayodai.

Haya yamo kwenye sehemu ya barua ya wananchi wa Kipunguni ‘A’ iliyotumwa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mh. Isaac Kamwelwe kumwomba akutane nao ili kujadili kwa kina masuala yanayohusu mgogoro na mvutano uliopo kati ya wananchi na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kuhusu ardhi ya eneo hilo baada ya kesi ya ardhi namba 18 ya mwaka 2011 kumalizika.

Katika barua hiyo, wananchi wa Kipunguni wamemwomba Waziri Kamwelwe akutane nao siku ya Jumamosi au Jumapili kutokana na wingi wa kazi zinazomkabili, ili wamweleze kwa kina malalamiko yao. Wanasema hawapingi kuhamishwa kwenye maeneo yao ila wanakerwa kwa ukimya na kutokuwa na uwazi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege tangu mwaka 1997!

Wananchi hao wanamwomba Waziri Kamwelwe awasaidie kuwaelekeza wahusika wanaosababisha mvutano huo kumaliza mgogoro huo ili ifanyike tathmini mpya kama ilivyoamuliwa na Mahakama na wananchi wanaohusika walipwe fidia na stahiki zao. Baada ya kupokea malipo yao ya fidia na kupewa viwanja vipya vyenye ukubwa wa maeneo yao, pia wapewe muda wa kukamilisha ujenzi wa makazi yao mapya.

Aidha lipatikane jibu sahihi kuhusu utaratibu uliotumika kuwachagua wananchi hao wachache (59) waliolipwa fidia. Pia kujiridhisha pasipo shaka kuhusu zoezi linaloendelea kimya kimya la kuwapa viwanja baadhi ya wananchi wa Kipunguni ‘A’ zikiwemo athari za kifedha na kisheria endapo zoezi hilo litaendelea.

Kwa kuwa baadhi ya wananchi waliofungua kesi mahakamani, na pia wasiokuwamo kwenye kesi wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu hatima (mwisho wa jambo baada ya kipindi fulani) ya suala hili, wananchi wa Kipunguni ‘A’ wamemwomba Waziri Isaac Kamwelwe ashughulikie maombi yao kabla ya ufunguzi wa jengo jipya la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Terminal 3 waweze kujua hatima yao ili wawe na muda wa kutosha kujiandaa kuhama baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Nakala ya barua hiyo imetumwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kwa taarifa.

Imetumwa pia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, M-bunge wa jimbo la Segerea, M-bunge wa jimbo la Ukonga na wakili wao, Charles wa Lugaila & Associets Advocates kwa taarifa vilevile.

Husemwa “Kikiharibika cha fundi (mwalimu); kikiongoka cha Bwana Suwedi (Suudi).” Maana yake kitu fulani kinapoharibika kinakuwa ni cha fundi lakini kikiwa kizuri ni cha Bwana Suwedi (Suudi). Methali hii huweza kutumiwa pale jambo fulani linapoharibika kisha akalaumiwa mtu mdogo ilhali likitengemaa au likawa sawa, sifa humwendea tajiri au mtu mkubwa.

[email protected]

0784 334 096