Kiswahili chapendwa duniani

08Oct 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Kiswahili chapendwa duniani

“BURA yangu sibadili kwa rehani.” Maana yake langu nalithamini hata kama kwa wengine halina thamani.

Wakati baadhi ya Watanzania hawathamini lugha yetu ya taifa, mataifa kadhaa duniani yanairai* Tanzania iwapelekee walimu wa Kiswahili.*Rai ni kitendo cha kumwambia mtu maneno mazuri au kumtendea mema ili akubali kutekeleza haja fulani.

Marekani ya Kaskazini, nchi kadha wa kadha* za Ulaya Magharibi na Afrika zinaiomba Tanzania iwapelekee walimu wa Kiswahili. Hata hivyo wakalimani* wengi walio nchi za nje wanatoka Kenya, sio Tanzania! Penye miti hapana wajenzi!

*Kadha (nomino) ni tamko linalotumiwa kutaja jambo lisiloainishwa bayana: Watu kadha walihudhuria mkutano. Msemo: Nimejia kadha, sikujia kadha wa kadha. Maana yake nimefika kwa ajili ya masuala fulani mahususi wala si kwa shughuli nyingine.

‘Kadha wa kadha’ ni ibada ya faradhi inayotekelezwa baada ya kupita wakati wake. ‘Kadhaa’ (kivumishi) a kiasi/idadi maalumu; haja aliyokuwa nayo mtu; matakwa, mahitaji.

‘Kadhi’ ni hakimu wa Kiislamu anayehukumu kwa kufuata sheria. ‘Kadhia’ ni jambo linalojiri; tukio la kuhuzunisha. ‘Kadhibisha’ ni kitendo cha kukanusha ukweli wa jambo.

*Wakalimani (mmoja aitwa mkalimani) ni watu wanaofasiri maelezo ya lugha moja kwa lugha nyingine; mtapta/watapta; mtarijumani/watarijumani.

Baadhi ya nchi za Mashariki kama Urusi kuna vitabu vinavyoeleza maana ya maneno ya Kirusi kwa Kiswahili.

Mfano: Panidyelynik/Jumatatu; Ftornik/Jumanne; Srida/Jumatano; Chitvyerk/Alhamisi; Pyatnista/Ijumaa; Subota/Jumamosi na Vaskrisyenye/Jumapili.

Kinachosikitisha ni kwamba wakati lugha ya Kiswahili inathaminiwa na mataifa mengine yaliyoendelea kuliko Tanzania, sisi twatumia maneno ya kihuni yanayozungumzwa mitaani!

Mfano: “Samatta shangwe kama lote.” Hiki ni kichwa cha habari kwenye gazeti la michezo. “Kama lote” maana yake nini?

“Asiyejua maana haambiwi maana.” Maana yake hapana haja ya kujisumbua kumweleza mtu asiyejua faida ya jambo. Methali hii huweza kutumiwa kumpigia mfano mtu anayejisumbua au kujipa taabu za bure kwa unayemweleza faida za jambo linalomhusu yeye lakini anapuuza.

Hata hivyo, “Ukuchapao (ukupigao) ndio ukufunzao.” Maana yake unajifunza jambo baada ya mchapo huo.

Methali hii yaweza kutumiwa kumshauri mtu anayelalamika baada ya kufikwa na jambo fulani. Anapaswa kujua kuwa mtu hujifunza kutokana na shida iliyompata au adhabu aliyopewa.

Ni dhahiri kama walivyosema wahenga kuwa “Chako ni chako, cha mwenzako si chako.” Maana yake kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa na una uhuru nacho kuliko cha mtu mwingine. Twafunzwa kuvitegemea vitu vyetu wala sio vya watu wengine.

Sasa soma baadhi ya maneno yatumiwayo na magazeti ya michezo nchini. “Azam ni mzuka kama wote.” Maana sahihi ya ‘mzuka’ ni kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa kuwa kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo.

Maana nyingine ya ‘pepo’ ni mahali panapoaminiwa kuwa Mungu atawaweka wale waliotenda mema ili waishi milele kwa raha na starehe baada ya kuwafufua na kuwahukumu; paradiso, edeni, janna, firdausi.

‘Kama’ ni kitendo cha kutoa maziwa kutoka kwenye kiwele; ushanga; mfano wa. Maana ya ‘ote’ ni bila ya kubakia. Waandishi wanapoandika “Azam ni mzuka kama wote” wana maana gani?

“Kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ana mambo nyie, jana buana ametamka maneno mazito juu ya straika wake, David Molinga akidai eti kama asipofunga mabao 15 hadi 20, yupo radhi akatwe mkono au kulipa faini ya Dola 1,000 (zaidi ya Sh2 mil).”

Waandishi wanapaswa kutambua na kutofautisha maneno ya mazungumzo na yanayoandikwa. Pia watambue matumizi ya maneno ya wakati uliopita, uliopo na ujao.

“Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ana mambo nyie” ni maneno ya mazungumzo si ya kuandikwa. “Jana (wakati uliopita) “buana ametamka. Ingeandikwa ‘jana alitamka.’ ‘Buana’ ni maneno ya waandishi badala ya ‘bwana’ ambalo ndilo neno halisi na sahihi. Ukiwauliza, wanasema “lugha inakua!”

Kama ndivyo, mbona nchi haiandikwi na kutamkwa ‘inchi?’ ‘Nchi’ ni sehemu ya ardhi ambayo haikufunikwa na maji; bara. Sehemu ya ardhi ambayo imegawanywa kwa mipaka ya kisiasa na inayotambulika kwa jina la taifa lake. ‘Inchi’ ni sehemu moja ya kumi na mbili ya futi moja, urefu unaokaribia sentimeta 2.5.

“Pia kocha huyo kutoka DR Congo ameendelea kukomaliza mavazi yake ya penzi akidai yana thamani kubwa kuliko inavyofikiriwa na anapenda kutinga kwa sababu ya hali ya hewa, hivyo wanatarajia kuyaacha watasubiri sana kwake.”

Ili nisipoteze muda kueleza mtiririko m-baya wa sentensi, nimeamua kuzungumzia maneno ya mwandishi kuhusu ‘kukomaliza,’ ‘penzi’ na ‘kutinga.’

Sipati maana ya ‘kukomaliza’ kwani si neno la Kiswahili nijuacho. Badala ya neno hilo mwandishi angeandika ‘komaa’ lenye maana ya pevuka au iva, kwa mfano matunda, nafaka na mazao mengine. Pia kuwa mtu mzima, fikia umri wa kuzaa.

Maana ya ‘penzi’ ni hisia kubwa ya kupenda; pendo. ‘Tinga’ ni kitendo cha kuning’inia bila kugusa chini; kitendo cha kitu kukwama mahali.

Ujumbe niliotumiwa: “Mzee Maro shikamoo. Mimi ni msomaji wako. Naomba kufahamu kipi sahihi wakati wa kujitambulisha. “Kwa jina naitwa Frank John Kimara” au “Kwa majina naitwa Frank John Kimara?” Natanguliza shukrani.” (0754 378 887).

Jibu langu: Kwa nini kueleza maneno mengi? Sema “naitwa Frank John wa Kimara, inatosha. Wengine hukosea zaidi wanapojitambulisha kwa kusema: ‘naitwa Bwana …’ ilhali wao ni wanaume!”

Akanijibu: “Asante sana.”

Methali: Upishi ni kuni.

[email protected]
0784 334 096