Kiswahili hakiendelezwi, chapotoshwa!

28May 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Kiswahili hakiendelezwi, chapotoshwa!

‘LUGHA’ ni mpangilio wa maneno yanayotumiwa na watu wa jamii fulani katika mawasiliano; ni mtindo anaotumia mtu katika kujieleza.
‘Lughawiya’ ni taaluma inayoshughulikia uchambuzi wa lugha katika nyanja mbalimbali kama vile sarufi, maana, matamshi na matumizi.

Lugha ya Kiswahili ina lahaja mbalimbali. Kati ya hizo, lahaja ya Kiunguja ndiyo iliyoteuliwa kuwa Kiswahili sanifu. Lahaja za Kiswahili ni Kingwana, Kimgao, Kitumbatu, Kimashomvi, Kimrima, Kiunguja, Kihadimu, Kipemba na Kijomvu. Pia Kimtang’ata, Kimvita, Chichifundi, Kivumba, Kingozi, Kipate, Kitikuu, Kishela, Kiamu, Chimiini, Chimbalani, Kingazija na Kinzwani.

Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Utamaduni wa Mzanzibari’ kilichoandikwa na Amour Abdalla Khamis na kupata ithibati ya Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), kuna maswali matatu yanayoulizwa mara kwa mara; 1) Mswahili ni nani? 2) Utamaduni wake ni upi? na 3) Asili yake ni wapi?

Maswali haya, kwa mujibu wa mwandishi, hupata jawabu za kejeli na kumdharau Mswahili kuwa ni mtu aliyetawaliwa na tamaduni za nje na kutokuwa na nasabu (uhusiano wa kizazi baina ya watoto na wazazi au wazee wao) wala watwani mahususi. Kejeli na dharau kama hizi zinafanywa sana na hata baadhi ya Waswahili wenyewe kwa kutoithamini lugha yao ya Kiswahili yenye msingi wa utamaduni wa Mswahili, pale baadhi ya watu wanapohoji kuwa Kiswahili:

Hakijitegemei kwani kimepokea maneno, matamshi na maandishi yenye asili na miundo ya Kiingereza na Kiarabu na kupoteza uasili wake.
Hakina mwenyewe wala pahali mahususi bali kila msemaji na mjuzi ndiye mwenyewe na sasa ni miliki ya Afrika au dunia nzima.

Hakitumiwi kwa usahihi na ufasaha miongoni mwa Waswahili wenyewe na badala yake huona fahari ya kutumia Kiingereza au kuchanganya Kiswahili na Kiingereza.

Waandishi wa sarufi yake hawaafikiani katika uchambuzi wa baadhi ya vipengele kama vile aina za maneno, vitenzi, ngeli za majina na aina za sentensi.

Dhana hizi zinahitaji kutafitiwa kwa kina ili kujua ukweli wake. Inawezekana baadhi ya dhana hizo zikawa na ukweli kutokana na kuathiriwa kwa Waswahili, Kiswahili na Uswahili jambo ambalo ni la kawaida kwa watu wote, lugha zote na tamaduni zote za dunia hii. Lakini upo uhakika kuwa baadhi ya dhana hizo si sahihi kwa Mswahili, Kiswahili na Uswahili wake. (Ukurasa wa 1-2).

Fasili ya Mswahili: Kilugha neno Mswahili lina asili ya Kiarabu kwa maana ya mtu wa pwani. Kiistilahi, kwa mujibu wa Bakhresa, S.K. (1992:256) “Mswahili ni mtu ambaye lugha yake ni ya Kiswahili. Mtu mwenye maneno mengi, mpayukaji, laghai, mdanganyifu.”

TUKI (2004:279) wanasema kuwa Mswahili ni “Mtu asiyekuwa na lugha nyingine yoyote ya jadi yake isipokuwa Kiswahili. Mtu anayeishi mjini ambaye lugha yake ya mwanzo ni Kiswahili au mwenyeji wa mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki na visiwa vilivyo karibu yake. Mtu mwenye maneno mengi, mjanja.”

Fasili hizi zote zinamweka Mswahili kuwa ni mtu matata sana katika eneo la Mwambao wa Afrika Mashariki na kuwahofisha wengine wasio Waswahili ili wam-beze. Awali tulisema kuwa Mswahili anakejeliwa na kudharauliwa katika jamii za Afrika Mashariki.

Naona ukweli ndio huo kwa mwenye macho na masikio ya kuziona au kuzisikia fasili hizo zilizomo katika makamusi yanayotegemewa. Mtu mwenye maneno mengi, laghai, mjanja, mnyang’anyaji katika Afrika Mashariki ndiye Mswahili! Ama kweli asiyekujua hakuthamini na akutukanae hakuchagulii tusi.

Sifa hizi si za Mswahili tu ni sifa za watu wengi zilizoenea kwa baadhi ya jamii tofauti za watu wa Afrika Mashariki na dunia nzima. Leo iweje sifa hizi atwikwe na kubambikizwa Mswahili peke yake? (rejea Fasili na Sifa za Mswahili Uk. 4).

Lugha: Kwa mujibu wa Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977-52 na Nurse, D. & Spear, T. (1985-62), lugha ya Waswahili ni Kiswahili chenye kujumuisha viswahili na lahaja zake 16 zikiwamo:

1.Kiunguja Mjini (Unguja mjini, Magharibi na Kati). 2. Kipate (Kaskazini ya Pate). 3. Kisiu (Mji wa Siu Kenya). 4. Kibajuni au Kitikuu (Kaskazini ya Lamu na Kusini ya Kismayuu-Shungwaya). 5. Kimgao au Kimwani (Kilwa na Kaskazini ya Msumbiji). 6. Kimtang’ata (Tanga mjini na Pangani). 7. Kipemba (Kisiwa cha Pemba).

8. Kimvita (Katikati ya Mombasa). 9. Kijomvu (Kaskazini ya Mombasa). 10. Kiamu (Kisiwa cha Lamu). 11. Kimrima (Mafia, Rufiji na Dar es Salaam). 12. Kimakunduchi (Kusini Unguja). 13. Chimiini au Chimbalazi au Kibarawa (Barawa). 14. Kitumbatu (Tumbatu na Kaskazini Unguja). 15. Kichichifundi au Chifunzi (Kusini ya Gaza hadi Wasin, Kenya) na 16 Kingazija (Komoro). (Uk. 9)

Hata hivyo mwandishi Amour Abdalla Khamis anaandika kuwa usanifu wa Kiswahili umekosea na kuitoa ladha ya ufasaha na usahihi kwa kuyaandika baadhi ya maneno yasivyotamkwa na Waswahili wenyewe. Mfano, badala ya kuandika nnje, mmbwa, arubaini, tafauti, thamanini, dasturi na zunguuka kama yanavyotamkwa huandikwa, nje, mbwa, arobaini, themanini, desturi na zunguka.

Baada ya kueleza yote haya kutoka kitabu cha ‘Utamaduni wa Mzanzibari’ kama ilivyoandikwa na mwandishi Amour Abdalla Khamis, kuna maneno ya Kiswahili yanayotumiwa vibaya na waandishi wa magazeti na kuchanganya Kiswahili na Kiingereza kama ‘straika’, ‘ishu’ wengine huandika ‘inshu’, ‘stop’ n.k.

Pia maneno ya Kiswahili yanayotumiwa vibaya kama ‘mwisho wa siku’, ‘lakini’, ‘kwa niaba yangu’, ‘pokelewa’, ‘wakilisha/wasilisha’, ‘chama lao’, ‘mzuka’ n.k. Tukutane toleo lijalo Inshallah (apendapo Mwenyezi Mungu).

Methali: Anayejidai mjanja ni mjinga.
[email protected]
0784 334 096