Kiswahili kinavyopelekwa arijojo

16Jul 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Kiswahili kinavyopelekwa arijojo

‘ARIJOJO’ ni uendaji usio na mwelekeo mwafaka kwa kukosa kuongozwa au kupangiliwa vizuri; enda ovyo; hali ya kupotea. Ndivyo lugha yetu ya taifa Kiswahili isivyokuwa na thamani miongoni mwetu!

Ndo maana wahenga walisema “Titi la mama li tamu, jingine halishi hamu.” Maana yake titi la mama huwa tamu, jingine halimalizi tamaa au hamu ya maziwa. Ni methali ya kutumiwa kupigia mfano kitu ambacho mtu ana asili nacho na anakithamini. Mbona hatutaki kuthamini lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo lugha rasmi ya taifa?

‘Mazungumzo’ ni maongezi baina ya watu wawili au zaidi; ubadilishanaji wa mawazo baina ya watu, nchi au taasisi kuhusu jambo. ‘Uandishi, pia uandikaji ni shughuli inayohusu masuala ya kuandika kama vile habari, magazeti au kitabu; namna au ujuzi wa kuandika. ‘Uandikishaji’ ni uwekaji wa taarifa za mtu au kitu katika orodha au daftari maalumu kwa kuandika maelezo yake.

Ilivyo sasa (kipindi cha wakati uliopo), waandishi, hasa wa michezo, hushindwa kuandika mtiririko mzuri wa sentensi (tungo yenye kiima na kiarifa na inayojitosheleza kimaana). Kadhalika mara nyingi huandika maneno ya mitaani yasiyo na ufasaha wa Kiswahili na upotoshwaji mwingi wa Kiswahili hivyo sentensi kutoeleweka!

Maneno ya kuzungumza: “Ee bwanae, ngoja nikupashe yaliyotokea mtaani kwetu leo” au “Umesikia yaliyotokea mtaani kwetu leo?” ama “Umekalia nini?” mwingine atajibu: (ashaakum) tamko la kuomba radhi kabla ya kusema neno la karaha: “matako.” Haya yote ni maneno ya mazungumzo kwa hiyo hayastahiki kuandikwa gazetini wala kusomwa kwenye runinga au redio.

“Kama hujui, klabu hizo kongwe hutenga bajeti zao za kila mwaka ikiwamo usajili na Simba kwa miaka miwili iliyopita ilikuwa ikitenga bajeti kubwa kuliko ile ya Yanga ikitajwa kuwa ni Sh1.3 bilioni huku watani wao wasajili kwa kuungaunga.”

Ingeandikwa: “ … ikitajwa kuwa Sh. bilioni 1.3” badala ya Sh1.3 bilioni kama ilivyoandikwa. Kadhalika “huku watani wao wasajili …” Neno la mwisho (wasajili) halikukamilika. Kwa hiyo sentensi haieleweki kwa kutokuwa na mtiririko mzuri.

Mwandishi anapoandika gazetini au kutangaza kwenye runinga ama redioni hufanya hivyo kuwajuza wasomaji wa magazeti, watazamaji wa runinga na wasikilizaji wa redio. Kinachotakiwa ni mwandishi kuwaeleza wasomaji, watazamaji na wasikilizaji kile kilichotokea badala ya kuweka maneno ya kuuliza.

Mwandishi anapoandika au kuuliza “kama hujui …” ni kosa kwani yeye ndiye aliyeona au kusikia kilichotokea/yaliyotokea hivyo anapaswa kuwajuza wasomaji/watazamaji/wasikilizaji hali halisi ilivyokuwa. Huyo anayeambiwa “Kama hujui …” ni kweli hajui ndo maana ananunua gazeti, anaangalia runinga au anasikiliza redio ali ajue kilichotokea.

“Kwa misimu miwili, mashabiki wa Yanga wamejikuta wakinuna, hii ni kutokana na chama lao kutoka kapa Ligi Kuu Bara na michuano mingine.” Maneno nitakayoyatolea maana halisi ni ‘wamejikuta’, ‘chama lao’ na ‘kapa’.

Maana ya ‘jikuta’ ni kuwa mahali bila kukusudia, kuwa katika hali fulani bila kujua. ‘Chama’ ni kikundi cha watu wenye itikadi au lengo moja, kundi lenye kufuata kaida au silka fulani zenye kuegema dini, siasa, misimamo ya jamii, uchumi au jambo lingine lenye maazimio maalumu.

‘Kapa’ ni –topata kitu au alama zozote katika mchezo; shindwa kupata hata fungu moja. Si kweli kuwa Yanga haikupata alama zozote kwenye Ligi Kuu ya misimu miwili iliyopita. Waandishi wasitumie maneno ya mitaani au wasiyojua maana yake kwa undani.

Aidha maana nyingine ya ‘kapa’ ni urefu wa kutoka bega moja hadi lingine wakati wa kupima nguo. Pia ni vazi kama koti lakini fupi lisilo na mikono; kizibao//kizibau. Kadhalika eneo la pwani lenye tope ambapo mikoko husitawi.

“Yanga iliyumba tangu Yusuf Manji, aliyekuwa Mwenyekiti wao kujiuzulu na kukosa pesa za kufanya usajili wa kufuru kama zamani, lakini hali kwa sasa imebadilika na inaonekana mabosi wa Yanga wanakula sahani moja na bilionea wa Simba Mohamed ‘Mo’ Dewji.”

Maana halisi ya ‘kufuru’ ni kitendo cha kusema au kutenda jambo lililo kinyume na dini; kitendo cha kumkana Mungu. Tamko au tendo lililo kinyume na dini au kumkanusha Mungu. Mwandishi anapoandika “ …usajili wa kufuru …” ana maana ya ‘usajili wa kumkana Mungu’ au ana maana gani?

Kuandika au kusema ‘chama lao’ badala ya ‘chama chao’ ni kosa ingawa magazeti ya michezo huandika ‘chama lao’ kila mara. Badala ya kuandika ‘chama lao’ iandikwe ‘chama chao, klabu yao’ au ‘timu yao.’

“Pacha wa Kagere mzuka kama” ni kichwa cha habari ya gazeti la michezo. Kwanza kichwa chenyewe hakikukamilika na kwa hiyo hakina maana yoyote kwa wasomaji. Pili ‘mzuka’ nimelitolea ufafanuzi mara nyingi sana kwenye safu hii kumbe natwanga maji kwenye kinu! Niandikaje ili nieleweke au wenzangu hudhani mimi ndiye nisiyeelewa?

Jamani! (tamko la kuwataka watu wasikilize. Tamko la kuonesha hisia ya kukerwa), ‘mzuka’ ni kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa kuwa kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo. Sijui kwa nini waandishi wa habari za michezo hupenda mno kulitumia neno hilo!

“KADAMSHI Koku wa kapuni ye na Manula tu!” Kama mwandishi anaandika habari au makala kwa kutumia maneno yasiyoeleweka, anafanya kazi bure. Nimeshindwa kupata maana ya ‘kadamshi.’ Nitumiapo maneno ninayohisi hayaeleweki vizuri, huyatolea maana yake. Kwa mfano, ‘kesa’ ni kitendo cha kuondoka wingu la mvua. Kwa maana hii, wasomaji hujua maana ya neno nililotumia.

Methali: Jawabu wakatiwe, na wakatiwe si zani.

[email protected]

0784 334 096