Kitema kuni temato

01Aug 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kitema kuni temato

‘TEMATO’ ni tema vizuri. Maana yake ukiamua kuchanja kuni zichanje vizuri. Methali hii yatufunza kuwa tuamuapo kufanya jambo lazima tufanye vizuri na kwa njia iliyo bora zaidi. Matumizi ya kiisho‘to’ hupatikana katika lugha ya kishairi.

Kadhalika, twakumbushwa na wahenga kuwa “Kilemba hakimfanyi mstaarabu mtu.” Maana yake mtu hawezi kuwa mstaarabu kwa kuwa kavaa kilemba. Heshima au taadhima ya mtu pamoja na thamani yake haitokani na sura zake za nje au anavyoongea mbele za watu bali na tabia zake.

Kocha Mbelgiji Luc Eymael alipokewa kwa shangwe na viongozi, pamwe wana Yanga alipotua klabuni. Viongozi, wanachama na mashabiki walitegemea kumwona akiibadili kabisa timu yao na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliomalizika hivi karibuni lakini alishindwa. Simba ndio iliyotwaa Kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Sikuona mafanikio yoyote kwenye timu ya Yanga iliyokuwa chini ya mwalimu Luc Eymael anayesemekana kuwa na ubaguzi wa rangi na wachezaji, hata kuwatukana! Matokeo yake ikawa haelewani na wasaidizi wake aliowakuta hata kusababisha timu kucheza chini ya kiwango, hivyo kila ilipocheza, ilipata ushindi kiduchu (-enye kuwa na kiwango cha chini) tena wa kubahatisha!

Wanachama na mashabiki wengi wa Yanga walikata tamaa kwenda kuishangilia kila ilipocheza.

Aidha, ilidhaniwa kuwa usajili wa Mghana Bernard Morrison ungeisaidia sana Yanga katika eneo la ushambuliaji, lakini baada ya kusifiwa sana kwa namna alivyolichezea gozi la ng’ombe, alifura kichwa akidhani yeye ni bora zaidi, si kwa wachezaji wenziwe tu bali hata kwa makocha na viongozi! Akawa hajali maonyo aliyopewa. Yasemekana kuwa hata Afrika Kusini haimtaki Morrison kutokana na tabia zake mbaya. Yanga inasubiri nini kumfukuza ili aende anakotaka?

Ndio maana wahenga walisema: “Kijumba cha ufisadi mbele kina sumbuko.” Maana yake mahali panapofanyiwa maovu huwa hapana mwisho mwema. Methali hii hutumiwa kutufunza kuwa tabia mbaya au isiyoelekea huwa haina mwisho mzuri. Mtu mwenye matendo yasiyofungamana na matakwa ya jamii hana mwisho mwema. Hii ni methali ya kuwazindua watu. Methali hii inawahusu viongozi wa Yanga.

Huyo Morrison atambue kuwa wahenga walikuwa na hekima walipotuachia methali isemayo: “Umejigeuza chachandu (aina ya samaki) kujipalia makaa.” Maana yake umejifanya chachandu kuishia kujivutia makaa na kujichoma. Msemo huu hutumiwa kumpigia mfano mtu anayejitosa taabani kutokana na matendo yake mwenyewe.

Hakika kila nilipoiona Yanga ikicheza, iliniwia vigumu kusema ndio timu iliyotwaa Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara mara 27 ikifuatiwa na Simba iliyotwaa ubingwa huo mara 21. Simba, wakati ule ikiitwa Sunderland, ilikuwa ya kwanza kutwaa kombe hilo Ligi ilipoanzishwa mwaka 1965 ikitwaa kombe mara mbili mfululizo, yaani msimu wa mwaka 1965 na 1966 ikifuatiwa na timu iliyokuwa machachari, Cosmopolitan pia ya Dar es Salaam mwaka 1967. Baada ya hapo Yanga ilizinduka na kutwaa kombe hilo mara tano mfululizo, mwaka 1968, 1969, 1970, 1971 na 1972.

Timu ya Mseto kutoka Morogoro ilitwaa ubingwa mwaka 1975 kisha Simba ikaijibu Yanga kwa kutwaa kombe hilo mara tano mfululizo, yaani mwaka 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980. Kunako mwaka 1981 Yanga ikatwaa kombe hilo, lakini kutokana na mgogoro uliozuka klabuni ikapokonywa na Pan Africans mwaka 1982 baada ya mfarakano, lakini Yanga ikajibu mapigo kwa kulitwaa tena mwaka 1983. Simba ikaipokonya Yanga kombe mwaka 1984 na Yanga kulitwaa mwaka 1985.

Mwaka 1986 Tukuyu Stars ya Mbeya ikatwaa kombe hilo kisha Yanga ikalitwaa tena mwaka 1987. Coastal Union ya Tanga ikalitwaa kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1988 kisha Yanga ikalitwaa tena mwaka 1989. Hata hivyo, Simba ikaipokonya Yanga mwaka 1990 lakini Yanga ikalitwaa tena Kombe kwa miaka mitatu mfululizo 1991, 1992 na 1993.

Simba ilitwaa tena kombe hilo kwa misimu miwili, yaani mwaka 1994 na 1995 kisha kupokonywa na Yanga kwa miaka mitatu 1996, 1997 na 1998. Timu ya Mtibwa Sugar ilitwaa kombe hilo misimu miwili ya mwaka 1999 na 2000 na kutwaliwa tena na Simba mwaka 2001 kisha Yanga mwaka 2002 na Simba kuipokonya Yanga mwaka 2003 na 2004.

Mwaka 2005 na 2006 ikawa zamu ya Yanga kulitwaa na kupokonywa na Simba mwaka 2007, lakini mwaka 2008 na 2009 Yanga ikatwaa tena kombe hilo. Kuanzia hapo ikawa ni kupokezana kwani Simba ililitwaa mwaka 2010 kisha Yanga mwaka 2011, Simba mwaka 2012, Yanga mwaka 2013. Azam nayo ikatwaa kombe hilo mwaka 2014 kisha Yanga ikalitwaa mara tatu mfululizo mwaka 2015, 2016 na 2017 kisha Simba nayo imelitwaa Kombe hilo mfululizo tangu mwaka 2018 mpaka sasa 2020.

Mpaka sasa Yanga imetwaa kombe hilo mara 27 ikifuatiwa na Simba mara 21, Mtibwa Sugar mara mbili, Cosmopolitan, Mseto, Pan Africans, Tukuyu Stars, Coastal Union na Azam mara moja moja kila timu. Ni kama Kombe hilo ni kwa ajili ya Yanga na Simba ilhali ni kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni wakati sasa wa timu zingine kuonesha kuwa haziwi wasindikizaji bali ni washindani kama zilivyo Yanga na Simba zilizotwaa ubingwa huo mara nyingi zaidi ya zingine.

[email protected]
0784 334 096