Klabu ziache kulalamika, muhimu kumaliza msimu

25May 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Klabu ziache kulalamika, muhimu kumaliza msimu

MIAKA ya mwanzoni mwa '80, bendi ya Makassy Orchestra ilitoka na kibao chao kilichotokea kuwa maarufu kisemacho 'Binadamu Hatosheki'.

Baadhi ya maneno yaliyomo kwenye wimbo huo yanasema 'binadamu hatosheki, hata ukimpa nini milele hatoridhika. Ukimpa tano leo, kesho atataka kumi. Leo mvua ikinyesha atataka jua, kesho jua likiwaka hachoki kulalamika, atataka tena mvua.'

Nia yangu si kukumbushia nyimbo za zamani, ila nataka kueleza jinsi baadhi ya klabu ambazo zitaanza kulalamika baada ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi yake ya Ligi kuamua mechi zilizosalia za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza Tanzania Bara na la Pili kuchezwa kwa vituo badala ya nyumbani na ugenini kama ilivyozoeleka.

Kupitia kwa waziri mwenye dhamana na michezo nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, alitangaza kuwa Ligi Kuu Tanzania Bara itachezwa kwenye Kituo cha Dar es Salaam, Uwanja wa Taifa, Uhuru na Azam Complex.

Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara na la Pili itachezwa kwenye kituo cha Mwanza, kwenye viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana.

Hii ni baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuruhusu shughuli zote za michezo kuanza Juni Mosi, baada ya kusimama tangu Machi 17, mwaka huu kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi vya corona. Tayari kwa mbali yameshaanza manung'uniko kutoka baadhi ya klabu.

Na kuanzia leo Jumatatu, kwenye vipindi mbalimbali vya michezo, tunaweza kusikia baadhi ya viongozi mbalimbali kila mmoja akiongea lake kuhusiana na hali hiyo.

Wapo ambao walianza kusikika wakitaka Ligi Kuu iendelee vile vile kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, ili mradi tu kila timu ipate faida ya kucheza nyumbani, hasa kipindi hiki ambacho timu nyingi zinapigana kwenye janga la kushuka daraja.

Baadhi ya viongozi watakuja kulalamika kuwa kucheza kwenye kituo kimoja kwao ni gharama licha ya kwamba serikali imejitolea na kutenga pesa za kujikimu, lakini wapo watakaosema kuwa hazitoshi.

Kuna baadhi ya viongozi wanaweza kuanza kulalamikia ratiba baada ya kupangwa na kusema inazipendelea baadhi ya timu.

Kusema kweli kwa hali iliyofikia sasa ni lazima kila klabu na viongozi wake wakubaliane na hali halisi jinsi ilivyo kwani, hata haikutegemewa kama ligi hizo zitachezwa tena.

Najua kuwa baadhi ya viongozi wa klabu hawakutaka kabisa ligi zirudi na walitaka zivunjwe kwa sababu mbalimbali ambazo wenyewe walidhani kuwa wangenufaika nazo kwenye timu walizopo kwa kutoshuka daraja.

Hawa kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaokuja na malalamiko, na wengine wataendelea pia kulalamika.

Ikumbukwe kuwa kila kinachofanywa sasa kinafanywa kwa dharura na si kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

Lengo ni kuunusuru msimu huu wa ligi umalizike na wapatikane mabingwa halali wa kuiwakilisha nchi kwenye mechi za kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Kuliko kulaumulaumu, ilipaswa kuisifia na kuipongeza serikali na wizara zake mbili za Afya na Michezo, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kwa kuhakikisha kuwa msimu huu hafutwi, na badala yake unamalizika ili maisha mengine yaendelee.

Kilichobaki sasa ni viongozi wa klabu zote kuzikusanya timu zao na kucheza mechi za ligi kwa mazingira haya haya mapya ambayo wamewekwa, badala ya kulalamika.