Kocha Stars ni Amunike, wengine mashabiki tu

11Mar 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kocha Stars ni Amunike, wengine mashabiki tu

UKITEMBELEA mitandao ya kijamii na hata wakati mwingine mijadala kwenye uchambuzi wa michezo, unajiuliza hivi Watanzania wote wamekuwa ni makocha?

Halafu ukisoma sana utakuta hata wanacholalamikia chenyewe hakiko kwenye kuijenga timu ya taifa, Taifa Stars, bali ni zile zile siasa za siku zote za Simba na Yanga.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, ameteua kikosi cha wachezaji ambao wataivaa timu ya Uganda Cranes Machi 24, mwaka huu, kwenye mechi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Baada ya uteuzi huo, kama kawaida ya Wabongo, wengi  wamekibeza na sababu wanazotoa wala si za kiufundi, bali za kishabiki zaidi.

Asilimia kubwa wanamlalamikia Amunike eti kwa sababu hajamwita Ibrahim Ajibu. Eti Ajibu angechaguliwa angeisaidia sana timu hiyo.

Ni Ajibu huyu huyu ambaye ameshakuwapo kwenye kikosi hiki hiki, akiwa Simba na pia akiwa Yanga na hakuna kitu chochote kilichofanyika.

Ajibu si mchezaji mbaya kwa kuwa ana kipaji cha hali ya juu, lakini ni huyu huyu ambaye kwenye mechi za Yanga wakati mwingine hamalizi dakika 90.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera mwenyewe ameshatamka kuwa Ajibu bado ana matatizo mengi ikiwamo kukaba na pia pumzi, hivyo akishaona mechi hii inatakiwa kukaba zaidi, anakuwa hana nafasi.

Wengine wanaona ajabu Mohamed Hussein 'Tshabalala'  hajachaguliwa, wengine Ramadhani Kabwili.

Lakini kwenye hiyo hiyo mitandao ya kijamii, hakuna yeyote anayelalamika kutochaguliwa na straika anayeongoza kwa sasa  kupachika mabao kwenye Ligi Kuu, Salum Aiyee wa Mwadui mwenye mabao 14.

Sijaona anayemshangaa Amunike kutomchagua Salum Kimenya, beki wa kulia wa Prisons wa kupanda na kushuka ambaye pia ana uwezo mkubwa wa kufunga na mpaka sasa ana mabao sita akiwazidi mastraika kibao kwenye Ligi Kuu.

Ila mashabiki wengi wanashangaa tu kwa sababu hajachagua wachezaji wanaocheza kwenye timu kubwa na wanaozishabikia wao.

Huwezi kuniambia leo kuwa eti Kabwili ni bora kuliko Aron Kalambo wa Prisons.

Lakini pia yupo atakayesema kuwa kwa nini asingeitwa Del Makonga wa Ndanda au Mohamed Makaka wa Stand badala ya Kalambo kwa  sababu kwa sasa wote hawa ni makipa bora kabisa kwenye Ligi Kuu?

Kocha yeyote duniani huchagua wachezaji ambao yeye mwenyewe anaona anaweza kuwatumia kutokana na mfumo na falsafa anayoitumia na si vinginevyo.

Na pia hata kocha hawezi kuchagua wachezaji wote ambao wanaoonekana ni wazuri au wanaopendwa na mashabiki.

Timu za Brazil, Hispania, Ufaransa zina wachezaji wengi wenye uwezo, lakini makocha huchagua baadhi tu ya wachezaji na si wote.

Kwa maana hiyo mashabiki wabaki tu kuwa mashabiki na  kukubaliana na kikosi kilichoteuliwa na kumuacha kocha afanye kazi yake.

Wabongo tufanye kama ile hadithi ya wanyama waliokuwa kwenye sherehe halafu kila mmoja akawa anakwenda kwa wapishi na kutaka kitu anachopenda kiwekwe kwenye chakula.

Simba alitaka chumvi iongezwe, sungura akataka pilipili iwe nyingi, tembo yeye akasema chakula ni lazima kiwe na ndimu nyingi, ili mradi tu kila mnyama alitaka kitu anachotaka yeye kiwamo kwa wingi badala ya kuwaacha wapishi ndiyo wafanye kazi yao kwa utaalamu wao.

Matokeo yake chakula kikawa kibaya. Chumvi kibao, pilipili balaa, ndimu kama vile kimechacha ili mradi tu tafrani na hakikulika. Tusifike huko.

Kinachotakiwa ni kuisapoti timu na si kuingilia kazi ya makocha kwa sababu hakuna mtu mwenye utaalamu nayo isipokuwa mwenyewe tu na benchi lake la ufundi.