Kofia 'bodaboda' zinafaa lakini...

05Jan 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Kofia 'bodaboda' zinafaa lakini...

KUWAPO kwa pikipiki nchini maarufu kama 'bodaboda', kumekuja kurahisisha usafiri kwa baadhi ya abiria, ingawa madereva wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za ajali.

Ajali za mara kwa mara, nyingi ikielezwa kuwa zinachangiwa na kutozingatia sheria za usalama barabarani.

Pamoja na hayo, usafiri huu umeongeza ajira kwa vijana ambao wengi wao walikuwa vijiweni.

Hata hivyo, baadhi ya madereva na abiria wao wamekuwa hawazingatii sheria za usalama barabarani ikiwamo kutovaa kofia ngumu (helmet) wanapokuwa kwenye vyombo hivyo vya moto.

Sheria inawataka kuvaa kofia hizo kwa sababu ya usalama wao, lakini ajabu ni kwamba wengi wao wamekuwa wakizifunga nyuma ya pikipiki zao na kubeba abiria kama kawaida.

Polisi wamekuwa wakiwabana madereva wasiovaa kofia kwa lengo la kuhakikisha usalama wao hasa pale wanapopata ajali, lakini bado baadhi wameendelea na mtindo wa kuendesha wakiwa vichwa wazi.

Hii ninaweza kusema inatokana na wengi wao kujifunza kuendesha vyombo hivyo uchochoroni, hivyo hawajui sheria za usalama barabarani.

Na matokeo yake wamekuwa wakiendesha pikipiki ovyo, kiasi cha kusababisha ajali.

Hata hivyo kwa upande mwingine, sina uhakika kama kofia hizo ni salama kiafya iwapo zitatumiwa na abiria zaidi ya mmoja.

Ninadhani kuna haja ya kuliangalia hilo, pamoja na madereva hawa na abiria wao kuhimizwa kuvaa kofia.

Hapa ninagusia zaidi upande wa abiria, kwa sababu dereva hana tatizo, kwani ana kofia yake.

Lakini abiria wanachangia kofia moja, na ndiyo maana ninakuwa na mashaka kama abiria hawawezi kuambukizana maradhi.

Sheria zinaruhusu abiria kuvaa kofia hiyo kwa ajili ya usalama wao, lakini ninadhani kwamba zinaweza kuwa na madhara kiafya kutokana na ukweli kwamba zinatumiwa watu wengi kwa nyakati tofauti na inawezekana wakawamo wenye maradhi.

Binafsi ninadhani kwamba kwa utaratibu huo ni rahisi abiria kuambukizwa magonjwa ya ngozi, ingawa hakuna taarifa yoyote ya kuwapo kwa hali, lakini kwa mazingira yalivyo hilo linaweza kutokea.

Wakati sheria zinawataka madereva na abiria kuvaa kofia hizo, pia kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kuwaepusha abiria na magonjwa ya kuambukiza kwa kuangalia uwezekano wa kuziwekea dawa.

Na ninadhani hilo liwe linafanyika kila inapotumika toka kwa abiria mmoja kwenda kwa mwingine.

Ninasema hivyo kwa sababu kofia nyingi kwa ajili ya abiria ni chafu, lakini abiria wanashurutishwa kuzivaa kwa vile ndivyo sheria inavyotaka.

Kuna daktari mmoja wa magonjwa ya ngozi ambaye niliwahi kuzungumza naye kuhusu hali hiyo akasema ni bora abiria akavaa kofia hizo, hata kama atapata magonjwa ya ngozi, kwani atatibiwa kuliko kupata ajali na akapasuka kichwa.

Hata hivyo, kwa maono yangu ninashauri kwamba pamoja na ukweli huo, afya ya abiria pia ni ya muhimu.

Hivyo mamlaka husika zinaposisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani, ziangalie pia namna ya kuepusha abiria na maradhi ya ngozi.

Najua kwamba kanuni za usafirishaji wa bodaboda na bajaj ni za tangu mwaka 2010, na zilianza kutumika mwaka 2011, lakini afya ya abiria, nayo ni kitu muhimu.

Aidha kanuni hizo pia zinawaelekeza madereva wa bodaboda kutotumia lugha chafu na matusi, kutoleta usumbufu kwa mtoa huduma mwingine, kutoendesha kwa mwendo usioruhusiwa, kutokatisha safari, kutoendesha wakati wakiwa wamelewa pombe na kutowasumbua abiria.

Hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), inaposisitiza kuzingatiwa kwa kanuni hizo, iangalie pia namna ya kuepusha abiria na maradhi ya ngozi.

Kwa hao madereva wasiozingatia sheria na kanuni wabanwe kwani kofia zao hawachangii na mtu mwingine, kwa nini wasizivae kwa ajili ya usalama wao?

Maana yake ni kwamba wanataka watii sheria kwa kushurutishwa.

Kanuni zinabainisha kuwa dereva wa pikipiki atakayekiuka masharti anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na akibainika kukiuka, atatozwa faini kati ya Sh. 50,000 na 100,000 ama kwenda jela kati ya mwaka mmoja na miaka miwili.

Kama hili la kuziwekea dawa kofia haliwezekani ama hakuna njia nyingine ya kufanya kulinda afya ya abiria, basi madereva wa bodaboda walazimishwe kuzifanyia usafi kila mara, kuliko hili la abiria kuchangia kofia moja, kitu ambacho ninadhani ni hatari kiafya.