Komu mbona mapema hivi unakimbilia wapi?

07Apr 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Komu mbona mapema hivi unakimbilia wapi?

MBUNGE wa Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Antony Komu, ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

Pamoja na kutangaza kuachana na chama hicho, mwanasiasa huyo anasema ataondoka Chadema mara atakapomaliza kipindi chake cha ubunge na kwamba atagombea tena kupitia NCCR Mageuzi.

Komu amechukua hatua hiyo huku akidai kwamba ndani ya Chadema kumekuwa hakuna uhuru wa kutoa maoni na kuitwa msaliti hata pale anaposhauri mambo yenye tija ndani ya chama.

Hata hivyo, pamoja na kutangaza kuhama, anaiomba Chadema itumie busara kumwacha amalizie majukumu yake ya ubunge kwa muda uliobaki, kwa vile bado anahitaji kuwatumikia wananchi wake.

Baada ya kauli hiyo, Chadema kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje, John Mrema, kinasema kitakaa vikao na kutoa taarifa rasmi kwa umma juu ya jambo hilo.

Kwamba kauli za mbunge huyo zinaonyesha haamini chama kinasimamia nini na analazimika kubaki ndani ya chama kwa kuwa anasubiri posho zake za bunge na kiinua mgongo.

Nikirudi kwenye jambo ambalo ninataka kulizungumzia, ni kwamba sioni kama kulikuwa na haja ya kuharakisha kutangaza kuhama chama wakati bado anahitaji kuwatumikia wananchi.

Mbunge anatangaza kuhama, halafu anaomba busara itumike kumwacha aendelee kubaki ndani ya chama hadi amalize ubunge wake ndipo aondoke! Haraka ya nini wakati bado upo upo Chadema?

Kwa kawaida mtu anakuwa mbunge kupitia chama kilichompa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo, sasa huyo ametangaza kujiondoa lakini kwa utaratibu ambao anataka aendelee kukumbatia ubunge hadi bunge litakapovunjwa.

Binafsi sioni ni kwa nini amefanya haraka kutangaza kuhama chama wakati bado anataka kuendelea kuwa mbunge na anatambua kuwa akihama atakuwa amepoteza sifa za kuendelea kushika nafasi hiyo.

Hii inatokana na ukweli kwamba nafasi hiyo mwanasiasa anaipata kupitia chama cha siasa, hivyo anapokihama na kwenda kujinga na kingine hawezi kuondoka nayo bali anakuwa siyo mbunge tena.

Kama Chadema watakaa na kuamua kumuondoa kwenye chama, atakuwa ameshindwa kuwatumia wananchi kwa miezi iliyobakia na pia hata posho zake za mwisho nazo atakuwa amezikosa.

Ninadhani kwamba washauri wake waliomwambia atangaze mapema kuhama chama wamefanya vibaya, kwani sasa anasubiri kile alichokiita busara ya Chadema kuendelea kuwa ndani ya chama hicho.

Maana yake ni kwamba chama hicho kikiamua kumfuta uanachama, atakuwa amekwama kutimiza malengo yake ambayo amesema ndiyo yamembakiza kwa muda ndani ya Chadema.

Lakini pia ikumbukwe kwamba suala la mwanachama kuhama chama ni haki ya kidemokrasia, ambayo awe mchanga hata mkomavu, ana haki ya kufanya hivyo pale inapobidi.

Inawezekana wapo baadhi ya wanasiasa wanaohama vyama kwa sababu ya ubinafsi kwa kujiona kuwa wao ndiyo wenye haki ya kuongoza, au kuteuliwa kugombea nafasi fulani za uwakilishi.

Katika hilo, wengine wanahama vyama kwa sababu ya kukimbia migogoro, wapo wanaoenda kutafuta nyadhifa, maslahi na hata kufikia kuviponda vyama wanavyotoka.

Wanasiasa wa aina hiyo wasipochaguliwa au kuteuliwa, huamua kuhama vyama vyao na kujiunga na vingine, lakini pia jambo la kuzingatia ni kwamba suala la kuhama chama ni haki ya kidemokrasia.

Hata hivyo, dhana ya kuhama chama inaweza kuwa inachangiwa na kuvutiwa na sera, ikijumuisha tunu, malengo, falsafa, itikadi zake, hasa kule wanakokwenda, ila kikubwa zaidi ni suala la haki ya kidemokrasia.

Inawezekana wapo baadhi ya wanasiasa wanaohama vyama kwa sababu ya ubinafsi kwa kujiona kuwa wao ndiyo wenye haki ya kuongoza, au kuteuliwa kugombea nafasi fulani za uwakilishi.

Wengine wanahama vyama kwa sababu ya kukimbia migogoro, wapo wanaoenda kutafuta nyadhifa, maslahi na hata kufikia kuviponda vyama wanavyotoka.

Wanasiasa wa aina hiyo wasipochaguliwa au kuteuliwa, huamua kuhama vyama vyao na kujiunga na vingine, lakini pia jambo la kuzingatia ni kwamba suala la kuhama chama ni haki ya kidemokrasia.