Kondakta, abiria daladala jiongezeni na hatari corona

26Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kondakta, abiria daladala jiongezeni na hatari corona

KUTOKANA na tishio la virusi vya corona, hatua mbalimbali za kukabiliana nayo inaendelea kuchukuliwa na serikali, ili kuhakikisha Watanzania wanabaki salama.

Miongoni mwa hatua hizo, ni kuzuia mikusanyiko mikubwa ya watu, tamasha, semina na kufunga shule kwa muda wa siku 30, ikiwa ni njia mojawapo ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Aidha, maelekezo hayo ya serikali yanawataka Watanzania kutosalimiana kwa kushikana mikono au kukumbatiana, ili kujikinga na kusambaa virusi vya corona, ambavyo ni rasmi tayari vimeshaingia nchini.

Serikali, pia haijawaacha nyuma wasafiri wa mabasi, zikiwamo daladala. Wasafirishaji wa mabasi hayo, wanatakiwa kubeba abiria kulingana na idadi ya viti vilivyomo ndani ya gari, ingawa katika sura ya pili ni mtihani, mkubwa.

Lengo la kufanya hivyo, ni kuepusha msongamano wa abiria ndani ya magari, hasa jijini Dar es Salaam, hali inayoweza kusababisha maambukizi ya virusi vya corona.

Kupitia taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) iliyotolewa kwa vyombo vya habari Machi 19 mwaka huu, ni kwamba imefikia hatua hiyo baada ya kukutana na wadau wa usafiri na usafirishaji nchini.

Mbali na hilo, kila daladala inatakiwa kuhakikisha kuwa na dawa ya kuua wadudu mikononi, abiria wapake kabla ya kupanda gari na kunyunyiziwa dawa kila mwisho wa safari, kwa ajili ya usalama wa abiria, kondakta na dereva.

Pamoja na maelekezo hayo, bado tatizo la ujazaji wa abiria kwenye daladala bado lipo palepale, ingawa baadhi ya madereva wameanza kutii maelekezo ya kuwa na dawa za kuua wadudu mikononi mwa abiria, kabla ya kupanda gari.

Ni vyema sasa maelekezo hayo yakatelekezwa, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, kwa sababu tu ya uzembe wa kutozingatia mambo ya muhimu kama hayo kwa ajili ya usalama.

Zipo baadhi ya daladala jijini Dar es Salaam, ambazo kondakta wake hawaruhusu kabisa abiria kuingia ndani kabla hawajanawa dawa ya kuua wadudu na wakilazimisha anashushwa.

Vilevile, ni agizo la kuchukua abiria wachache wa kusimama, ingawa kuna ukaidi wa kuwapo magari ya yasiyo na dawa.

Pia, magari yanajaza abiria kupita kiasi, kana kwamba hakuna maelekezo ya kiserikali kwa ajili ya kuepuka usambazaji virusi vya corona.

Jambo hilo siyo la kufanyia mzaha. Ni vyema makondakta, madereva pamoja na abiria ambao bado hawajaona umuhimu huo, wakajiongeza na kuchukua hatua za haraka badala ya kusubiri kukumbwa na tatizo la mamlaka za kisheria kuwachukulia hatua sahihi.

Ni bayana makondakta wanajaza abiria, ili kupata fedha zaidi. Abiria nao wanalazimika kupanda daladala zilizojaa, ili kuwahi kwenye shughuli zao za kila siku, kutokana na hali halisi.

Ushauri wa bure, ni bora kila upande ukazingatia afya zao kwanza. Ni kweli kwamba kuna changamoto ya uhaba wa daladala kwenye baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, hali inayosababisha abiria kukaa vituoni kwa muda mrefu, wakisubiri usafiri.

Nitamke, hicho kisiwe kigezo cha kuwafanya abiria walazimike kujazana katika daladala moja au makondakta kuwarundika kama mizigo, huku wakijua kuwa kuna tishio la virusi vya corona.

Waige mfano wa mabasi ya mwendokasi, ambayo sasa hayajazi abiria kama siku za nyuma na yana dawa za kuua wadudu mikononi, kwa ajili ya kulinda afya za abiria na madereva kwa ujumla.

Kwa janga hili la virusi vya corona, sidhani kwamba hakuna Mtanzania asiyelielewa. Niende mbali, kuwa pia sidhani kwamba taarifa ya Latra inayolenga usalama wa abiria na wasafirishaji, ni ngeni.

Inawezekana, wapo wasioamini na hata wanadharau, wakidhani kwamba virusi vya corona havipo. Ni vyema wakatambua kuwa hili ni janga la dunia nzima, kwa hiyo suala la kuchukua tahadhari ni muhimu.

Virusi vya corona vimeshakatisha maisha ya watu katika maeneo mbalimbali duniani, lakini kwa kinachofanyika sasa kwenye baadhi ya daladala, ni kama Watanzania hawana habari kuhusu hatari ya virusi hivyo.

Waswahili wana msemo 'Ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji', hivyo wakati nchi mbalimbali zikiendelea kukumbwa na virusi vya corona, Watanzania nao hawana budi kuwa makini.