Kongole Ali Mayai kwa hilo

11Jul 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kongole Ali Mayai kwa hilo

MTU anapofanya jambo zuri anastahiki tuzo/tunzo. Maana ya ‘kongole’ ni shukrani; asante. ‘Tuzo/tunzo’ maana yake ni zawadi anayopewa mtu kwa kufanya jambo jema au kazi nzuri.

Stahiki ni kitendo cha mtu kuwa na haki ya kupata kitu fulani kutokana na ufanisi aliopata. Ali Mayai anastahiki kupewa zawadi kwa kazi nzuri aliyofanya. Imebidi nieleze maana ya neno ‘stahiki’ ili wanaopitia makala na wasomaji wasidhani nimekosea kutumia neno hilo kwamba neno sahihi ni ‘stahili,’ hapana.

‘Stahili’ ni kitendo cha mtu kupata adhabu kulingana na jambo baya alilofanya. Kwa mfano, “mwafulani (jina linalotumika kumtaja mtu ambaye yupo lakini jina lake linafichwa) anastahili adhabu kwa kitendo alilofanya.”

Turudi kwenye mada (jambo linalozungumzwa, kusomeshwa au kuandikwa). Muungwana (mtu mwenye tabia njema), Ali Mayai aliyekuwa mchezaji mahiri wa Yanga kabla ya kustaafu, aliandika makala kwenye gazeti maarufu la michezo nchini iliyopewa kichwa: “Timu zijengwe kisayansi, badala ya kukurupuka.”

Amezitaja zaidi timu za Simba na Yanga na mashabiki ambao wamekuwa na tabia ya kutwaa ubingwa kwa kubadilishana. Kwamba mashabiki wa timu hizo kudhani kuwa ndizo zenye wajibu wa kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa!

Nauliza: Kama Ligi Kuu ina timu 20, kwa nini Simba na Yanga zionekane ndizo zinazofaa kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa? Timu 18 zilizobaki hazitaki kuiwakilisha nchi kwenye michezo ya kimataifa au zimeamua kuwa wasindikizaji?

Mayai anatoa mfano wa baadhi ya mechi ambazo Simba na Yanga hucheza na timu zingine katika ligi na kutawaliwa katika maeneo yote ingawa kuna wakati timu hizo hufanikiwa kupata matokeo tu kwani wachezaji wao huwa na mizigo ya fikra vichwani mwao.

Mfano mzuri ni mechi ya Kagera Sugar na Yanga iliyochezwa Jumatano ya wiki hii na Yanga kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Niliangalia mechi ile mwanzo mpaka mwisho na kusikitishwa mno kwa jinsi Yanga ilivyocheza.

Ingawa Yanga ilishinda, nina kila sababu ya kusifu uchezaji wa Kagera Sugar licha ya kushindwa kwani katika mchezo kuna kushinda na kushindwa. Nathubutu kusema Yanga ilipata bahati ya kuishinda Kagera iliyomiliki mpira kuliko Yanga walioonekana kuwa kama wanafunzi wa kandanda!

Nakubaliana na methali ya wahenga kwamba: “Bahati humwacha wa mbele na kumfuata wa nyuma.” Maana yake bahati huweza kumwendea mtu yeyote. Methali hii hutumiwa hasa pale ambapo bahati imemwangukia mtu ambaye hakutarajiwa.

Kagera Sugar chini ya mwalimu wao Mecky Maxime, iliifunga Yanga jijini, Dar es Salaam mabao 3-0 licha ya mengine kukataliwa na mwamuzi. Uamuzi huo uliwashangaza watazamaji wengi uwanjani, hasa wale wanaoujua mchezo wa kandanda ulivyo!

Kuna wakati kulikuwa na tetesi kuwa kocha Maxime alitakiwa na Yanga naye alikuwa tayari lakini kwa masharti ya mshahara aliotaka. Ghafla akaletwa Mzungu Luc Eymael ambaye ndiye aliyeko sasa.

Ina maana Maxime alitaka mshahara mkubwa kuliko anaolipwa huyo Mzungu aliyeko Yanga sasa ambaye hupiga kelele uwanjani mwanzo mpaka mwisho wa mchezo akiwaelekeza wachezaji jinsi ya kujipanga na kucheza? Hawafundishi wakati wa mazoezi, au wachezaji hawamwelewi?

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Mayai anasema timu hujengwa kwa miongo kadhaa badala ya msimu mmoja kama ilivyo kwa timu zetu za Tanzania! Nakubaliana na Mayai kwani timu zetu za Tanzania zimekuwa na tabia ya kusajili wachezaji wasiopungua 10 kila mwaka na kuwaacha wengi wao baada ya kipindi kifupi!

Ndo yale waliyosema wahenga kuwa: “Haraka haraka haina Baraka.” Maana yake jambo linalofanywa kwa pupa huwa halitengemai au halifani. Methali hii yatufunza umuhimu wa kufanya mambo yetu kwa utaratibu ikiwa twataka yafane.

Tatizo la Simba na Yanga ni kugombea wachezaji. Kama mojawapo imeonyesha nia ya kumsajili mchezaji fulani, ingine huingia kinyemela kutaka kumsajili mchezaji yuleyule. Wachezaji hugombewa lakini baadaye huachwa na kupelekwa kwa timu zingine kwa mkopo!

Kiungo huyo alieleza kwenye makala yake kuwa timu hujengwa kwa miongo kadhaa na sio msimu mmoja kama zifanyavyo timu zetu. Anaipongeza Simba kwamba yaweza kuwa darasa kwa vilabu ambavyo kila msimu hufikiria kufanya usajili ili kuijenga upya timu ilhali kinachotakiwa ni kuendeleza ujenzi wa timu ulioanza misimu kadhaa iliyopita.

Vilevile anasema mabadiliko ya mabenchi ya ufundi ni jambo la kawaida, lakini mabadiliko yanayofanywa na vilabu vingine vya soka, hasa zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, husababisha timu nyingi kuanza msimu kwa kujenga upya vikosi vyao badala ya kuwa na mwendelezo wa kikosi cha msimu uliopita.

Niishie hapa nisije kurushiwa mawe na mashabiki wasiojua mchezo wa kandanda ulivyo! Nawapa pole.

[email protected]
0784 334 096