Kongole Jeshi la Polisi Kigoma kwa ulinzi makini uwanjani

19Oct 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kongole Jeshi la Polisi Kigoma kwa ulinzi makini uwanjani

ZIARA ya Simba mkoani Kigoma imeibua vitu kadhaa vipya ambavyo mashabiki wengi wa soka hasa wa mikoa mingine nchini hawakuwahi kuviona vikitokea hapa nchini.

Simba ilienda Kigoma baada miaka mingi kupita tangu enzi za Mbanga FC ilipokuwa Ligi Kuu na ikacheza na timu za Mashujaa, ikashinda bao 1-0 na mechi nyingine ilikuwa dhidi ya Mabingwa wa Burundi, Aigle Noir na ikatoka nao sare tasa.
Mechi hizo zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Kitu cha kwanza ambacho kilishangaza wengi ni mapokezi makubwa iliyoyapata Simba tangu ilipowasili Uwanja wa Ndege na mitaani ambako kulikuwa na umati mkubwa wa mashabiki, uliowavutia mno wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo.

Kilichofuatia kingine ni jinsi mashabiki wa soka Kigoma walivyojitokeza kwa wingi kwenye mechi hizo mbili. Taarifa zinaeleza kuwa, saa nne asubuhi, tayari uwanja ulikuwa umeshaanza kufurika watu kutoka sehemu mbalimbali mkoani humo.

Halafu wakazi wa Kigoma si tu kwamba walikuwa wamejazana uwanjani, lakini walikuwa wakishangilia mno muda wote kitu ambacho huwashinda hata mashabiki wa soka wa Dar es Salaam.

Kitu kingine kilichowashangaza wengi ni ubovu wa Uwanja wa Lake Tanganyika. Nadhani utakuwa unaongoza kwa ubovu kati ya viwanja vyote Tanzania kama sitokosea.

Udongo mwekundu ndiyo unaoonekana zaidi kuliko nyasi. Nyasi chache zilizobaki uwanjani zimekaukiana kwa kukosa maji na rutuba. Kusema kweli sehemu ya kuchezea uwanjani inasikitisha kweli kweli.

Jinsi mashabiki wa Kigoma walivyojitolea kwenye ziara ya Simba na kama kungekuwa na kiwanja kizuri, basi wangefaidi kandanda safi na pesa yao ingekwenda kihalali.

Cha mwisho ni muundo wa ulinzi kwenye uwanja huo. Haijapata kutokea kuona muundo ule wa ulinzi kwenye viwanja vyote nchini Tanzania. Aina ile ya ulinzi mara nyingi huwa tunaiona nje ya nchi kwenye ligi mbalimbali hususan Ulaya.

Kuna baadhi ya watu walidiriki kusema kuwa huenda hawakuwa askari wa Tanzania wanaolinda uwanja huo. Lakini ukweli ni kwamba walikuwa ni Wabongo.

Muda wote walikuwa wamegeukia mashabiki kama Ulaya vile. Walikuwa wameachiana nafasi na kuzunguka uwanja mzima, huku wakitazamana na mashabiki, tofauti na tulivyozoea askari polisi wakiwa nao ni sehemu ya watazamaji wa soka katika viwanja vingine.

Umati mkubwa wa mashabiki Kigoma ulivyokuwa uwanjani na jinsi askari walivyokuwa wanalinda ilivutia mno, kiasi kwamba wengi waliokuwa wanaangalia kwenye televisheni walisifu na kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, kuagiza askari wake kote nchini wanaopewa jukumu la kulinda usalama viwanjani wakati wa mechi kuiga mfano ule.

Aina ile ya ulinzi hata kama kunatokea tatizo ni rahisi kulitatua kwa muda mfupi na bila madhara makubwa huku mhusika kama anatokea jukwaani kuwa rahisi kujulikana. Kwa sababu mtu wa kwanza kumpiga mwenzake, kurusha chupa au kufanya fujo ataonekana na kudhibitiwa kwa urahisi. Lakini askari wanaoangalia soka wanashtukia fujo imeshakuwa kubwa na kinachofanyika nao wanahamaki na kupiga mabomu ya machozi.

Yeyote aliyetoa mafunzo kwa askari polisi wa Kigoma anastahili sifa. Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma na hata ni makamanda wa vituo vya polisi vilivyotoa askari nao pia wanastahili sifa na kuwa mfano kwa wengine. Nadhani askari polisi na walinzi wa viwanja vingine vya soka nchini wanachakujifunza kutoka kwa wenzao wa Kigoma ambao pamoja na kwamba hawana Ligi Kuu kwa miaka mingi, lakini kiulinzi 'wametisha' zaidi na sina budi kutoa kongole kwao.'