Kongole Simba, heko Namungo

08Aug 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kongole Simba, heko Namungo

NALAZIMIKA kuwapa kongole (shukrani; asante) viongozi wa Simba kwa jinsi walivyoiongoza timu yao na kukamilisha msimu uliomalizika hivi karibuni kwa kutwaa vikombe viwili na ngao mfululizo.

Naam, “Anayejitahidi hufaidi.” Maana yake yeyote anayetia bidii hufaidi kutokana na juhudi zake. Hii ni methali inayowanasihi watu kuwa na bidii katika shughuli yoyote wafanyayo.

Ndivyo walivyofanya viongozi wa klabu ya Simba, wachezaji, wanachama na mashabiki waliojaa uwanjani kuwashajiisha (kuwahamasisha; kuwapa ari) wachezaji wakati timu yao ilipocheza nyumbani na ugenini.

Kwanza Simba ilitwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam mabao 4-2 kisha Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo wakipata alama 88.

Yanga iliambulia nafasi ya pili kwa kupata alama 72 ikipitwa kwa alama 16 na Simba, kisha Azam iliyopata alama 70 ikiachwa na Simba kwa alama 18. Kama haitoshi, Simba wakatwaa Kombe la Shirikisho (ASFC) kwa kuifunga timu ngeni ya Ligi Kuu, Namungo FC kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga. Hii yanikumbusha methali isemayo “Penye nia pana njia.”

Maana yake ikiwa mtu ana dhamira ya kufanya jambo fulani hawezi kukosa njia. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kwamba tuwapo na nia ya kufanya jambo, lazima tufanikiwe.

Viongozi wa Simba wakiongozwa na MO Dewji walikuwa na nia; hivyo wamevuna walichopanda. Najikalifisha (kitendo cha kujilazimisha kutenda jambo), kuwapa Simba kongole kwa mara nyingine, ingawa naumia ndani kwa ndani! Nakiri walivyosema wahenga kuwa:

“Kweli ingawa chungu niambie sinifiche.” Twafunzwa umuhimu wa kuwa na tabia ya kuusema ukweli au kuwa watu wausemao ukweli. Kama kumbukumbu zangu si sahihi, natangulia kuomba radhi, lakini kama ni sahihi, nathubutu kusema Simba imeweka rekodi ya pekee kwa kutwaa vikombe viwili na ngao kwa msimu mmoja. Wahenga walikuwa sahihi waliposema:

“Anayejitahidi hufaidi.” Maana yake anayetia bidii hufaidi kutokana na juhudi zake. Hii ni methali inayowanasihi watu kuwa na bidii katika shughuli wafanyazo.

Mafanikio ya klabu ya Simba yapaswa kuwa mfano kwa timu zingine. Sio zinazoshiriki Ligi Kuu tu, bali timu zote za kandanda nchini.

Mchezo wa kandanda unapendwa sana nchini kama unavyopendwa duniani kote, lakini twashindwa kuwaendeleza wachezaji wetu kwani twawategemea mno wachezaji wa nje wanaokuja kuchuma kwetu na kujinufaisha huko watokako!

Tutazinduka lini? Funzo kubwa kwa klabu nyingine ni kuwa makini, kufanya usajiri wa kimya kimya, kujiepusha na uropokaji wa kuweka hadharani kila kinachokusudiwa kufanywa na klabu husika. Maana yangu ni kusajili wachezaji kimya kimya badala ya kutangaza majina ya wachezaji wanaokusudiwa.

Sitafanya haki kukamilisha makala yangu bila kuipongeza timu ya Namungo iliyoingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu uliopita na kushika nafasi ya nne chini ya Simba, Yanga na Azam kwa mtiririko huo.

Pia imeweza kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho ilipofungwa 2-1 na Simba kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Wachezaji wasajiliwe kwa umahiri wao, si majina. Aidha, wawe wamechunguzwa tabia au mienendo yao nje na ndani ya uwanja. Wasichaguliwe kwa kuwa walizifunga timu za Azam, Simba na Yanga tu.

Kadhalika, wachunguzwe nidhamu, yaani mpangilio maalumu wa kufanya jambo; adabu mbele ya watu wengine.

Pia matendo yao wanapokuwa mitaani kama wana uraibu (wa kuvuta sigara, bangi, dawa za kulevya na uasherati) au la.

Wachezaji wenye tabia hizo hawafai. Baada ya kuchunguza yote hayo na kufanya usajili, klabu zapaswa kuwa na utaratibu wa kulipa mishahara ya wachezaji kila mwezi kama ilivyo sheria.

Mishahara ya wachezaji inapocheleweshwa huwakatisha tamaa hivyo kucheza chini ya viwango na kutowaheshimu viongozi na walimu wao.

Wachezaji wa kigeni wanaocheza nchi za nje hulipwa mishahara mikubwa inayozidi baadhi ya marais wetu wa Afrika na kwingineko duniani.

Mishahara wanayolipwa wachezaji hao, kwa mfano Christiano Ronaldo, Lionel Messi, Mohamed Salah, n.k. ni mikubwa. Hii ndio inayowapa jeuri ya kununua ndege (eropleni) zao binafsi, meli, majumba ya fahari yenye gharama kubwa na msururu (vitu vilivyokaa kimoja baada ya kingine; msogo) wa magari ya aina tofauti.

Hapa Tanzania wachezaji husajiliwa kwa kulipwa milioni kadhaa za fedha na mishahara mikubwa kuliko idadi kubwa ya wafanyakazi! Hata hivyo inasikitisha kwani wanashindwa kutambua umuhimu wao kwa taifa! Sasa mchezo wa kandanda duniani si kama ilivyokuwa zamani kwani unalipa fedha nyingi zaidi.

Ndo maana wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine katika nchi za Ulaya, Marekani na kwingineko huuzwa na kununuliwa kwa milioni kadhaa kwa hela za nchi husika.

Hebu niwazindue wachezaji wa Tanzania. Wengi wao wana uwezo wa kwenda kucheza kandanda nchi za wenzetu zenye maendeleo mazuri ya kandanda katika nchi za Ulaya Magharibi na Mashariki, Marekani ya Kaskazini na Kusini, Canada n.k.

Wakicheza kwa bidii na kufuata kanuni za mchezo huo wanaweza kuwa kama wenzao wanavyofanya katika nchi nilizotaja.

Wachukue mfano wa Mbwana Samatta na wengine wanaocheza kandanda ughaibuni. Hebu niwaulize wachezaji wetu wa timu ya Taifa (Taifa Stars) waliopewa viwanja vya kujenga nyumba na Rais Magufuli jijini Dodoma kama wamejenga. Kama bado wanasubiri nini? Asiyejua chozi amtazame aliaye.

[email protected] 0784 334 096