Kuchamba kwingi mwisho …

14Jun 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Kuchamba kwingi mwisho …

NAHISI mvurugiko mkubwa wa lugha ya Kiswahili huko twendako. ‘Bidii’ inayofanywa sasa na waandishi wa habari za michezo yathibitisha wasiwasi wangu.

Nitaanza na methali mbili za wahenga wetu ili wasomaji waniambie ni ipi inayofaa kuwazindua waharibifu wa lugha yetu azizi (-enye thamani).

Mosi: “Mvunja kwao hakui, ila huwa yeye mbombwe (bombwe).” Bombwe ni funza, buu au gae la chungu. Pia ni kitu duni. Maana yake anayeivunja au kuisaliti nchi yake hakui au hana thamani, hubakia mtu wa kudharauliwa.

Methali hii yaweza kutumiwa kwa mtu anayeisaliti nchi yake. Pia yatufunza umuhimu wa kuzipenda nchi zetu na tamaduni (mila, desturi, asili, jadi, imani na itikadi) zake.

Pili: “Mvunja nchi ni mwananchi (mgeni mzo mpime).” Mzo ni kielezi chenye maana ya kwa wingi au tele ama sana. Maana yake anayeisaliti au kuivunja nchi ni mwananchi wa nchi hiyo.

Hutumiwa kueleza kwamba mtu anayeweza kuleta uharibifu mahali fulani ni anayepafahamu vizuri au mwenyeji wa mahali pale.

Kuna wanaonibeza wakisema: “Ah! Mchaga (kwa mama) tangu lini akajua Kiswahili?” Wengine wasema: “Tangu lini Mmasai (kwa baba) akafundisha Kiswahili?” Yote sawa, ila tutambue elimu ni taa, gizani huzagaa.

Kwa hakika elimu ni kitu muhimu sana kama taa inayotuangazia penye giza/kiza. Methali hiyo yatufunza faida zitokanazo na elimu. Binadamu hawezi kuyamudu mazingira yake vizuri bila ya kuwa na elimu.

Nawaachia wenye meno watafune ubuyu kwani “fumbo mfumbie mjinga mwerevu huling’amua.” Yote haya yajiani? Yahusu tabia ya baadhi ya waandishi wasiothamini lugha yao (yetu) ya taifa – Kiswahili!

Kuna wanaodhani kuchanganya maneno ya Kiswahili na Kiingereza katika uzungumzaji au uandishi ndio maendeleo.
Ewe! (tamko la kutahadharisha linaloonesha kushangazwa na jambo). “Mkataa kwao ni mtumwa.” Methali hii yatukumbusha umuhimu wa kuthamini asili zetu. Twapaswa kuwaonea fahari wazazi wetu na mataifa yetu sawia.

Nadharia kadhaa zimetolewa katika kujaribu kubainisha asili ya lugha ya Kiswahili. Mojawapo ni ile inayotoa hoja kuthibitisha kuwa Kiswahili ni Krioli (lugha ya awali ya wazungumzaji iliyoibuka kutokana na mchanganyiko wa lugha nyingi).

Hata hivyo yapo maneno mengi ya Kiswahili yanayotoa ufafanuzi wa maneno na vitu; hivyo hatuna sababu ya kutumia maneno ya kigeni. Wakati mwingine baadhi ya waandishi hupotosha mno maneno ya Kiswahili kwa kuyapa maana tofauti na maudhui (wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema).

Soma hii: “Kamusoko aleta kiberenge kipya” ni kichwa cha habari kwenye gazeti la michezo. ‘Kiberenge’ lina maana mbili: Ni garimoshi dogo la kukagua reli kabla ya garimoshi kubwa (treni) kupita. Pia hutumika kwenye mashamba ya mkonge.

Maana ya pili ni mwanamke (ashaakum!) malaya, kibiritingoma, kahaba, jamvi la wageni. Majina ni mengi ila kwa haya machache yatosha.

Kumbe Kamusoko atamleta mchezaji. Sasa fikiri mchezaji kuitwa garimoshi dogo! Twajitukana na kujidharaulisha wenyewe kwa dhana ya kupamba lugha kumbe twaonesha uzembe (ufanyaji wa jambo bila uangalifu au hadhari) wetu.
“Mademu wa Dodoma tayari zamani. Dodoma imepata bingwa wa Ligi Mkoa ya Wanawake baada ya mchezo wa mwisho kati ya Baobab Queens dhidi ya Pentagon Queens.”

Ingeandikwa ‘kati ya Baobab Queens na Pentagon Queens’ au ‘Baobab Queens dhidi ya Pentagon Queens.’ Maana ya dhidi ni –enye kupingana, kushindana na, kinyume na.

‘Mademu’ ni wingi wa ‘demu’ na maana yake ni ‘mabwende’ na moja ni ‘bwende’ yaani kitambaa kilichozeeka kinachovaliwa kiunoni wakati wa kazi shambani.

‘Demu’ ni kitambaa kikuukuu kinachovaliwa na mwanamke kufunika maziwa wakati wa kulima; tambara, nguo iliyochakaa. Yashangaza mwanamke kuitwa ‘tambara bovu’ ilhali ni mama, shangazi, dada na wake zetu! Mbona twawadharau kiasi hiki?

Eti nao hufurahia kuitwa hivyo! “Usiku kiza mangazimbwe (madanganyo) mtumbuu (aina ya samaki mdogo) huwa papa.” Hutumiwa kupigia mfano wa jambo asilolifahamu mtu. Jambo dogo laweza kumtatiza mtu ikiwa hana fahamu nalo.

Aidha kuna tatizo ya kuvamia majina bila kujua maana yake. Habari ninayoizungumzia, kuna timu ya dada zetu huko Dodoma inayoitwa Pentagon Queens yaani Malkia wa Pentagon.

Maana ya ‘pentagon’ ni pembe tano. Ni jengo la pembe tano lililojengwa kule Arlington, Virginia, Marekani kuwa makao makuu ya Jeshi la nchi hiyo.

Je, jengo la klabu ya kina dada wanaojiita ‘Pentagon Queens’ limejengwa kwa mtindo wa pembe tatu? Au wao ni ‘malkia wa makao makuu ya Jeshi la Marekani’ wanaoishi Tanzania?