Kuelekea dalili ya kuanza rasmi hospitali iliyojengwa miaka 40

30Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kuelekea dalili ya kuanza rasmi hospitali iliyojengwa miaka 40

HOSPITALI ya Rufani ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, inayojengwa mjini Musoma mkoani Mara, inatarajia kuwa kubwa na kuhudumia mikoa yote katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Uongozi wa mkoa hadi sasa umeamua kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo na umeahidi utahakikisha itakuwa na miundombinu, vifaa tiba na wataalamu wa kutosha, katika utoaji huduma za kibingwa katika fani zote muhimu.

Hivi sasa, hospitali inatarajia kuanza kutoa huduma za awali mwezi ujao, ambazo ni za mama na mtoto pamoja na matibabu ya figo, huku ukamilishaji miundombinu mingine ukiendelea.

Kuanza kutoa huduma hizo kunaelezwa na mkuu wa mkoa huo, Adam Malima, wakati akipokea vifaa vya kisasa kwa ajili ya kitengo cha matibabu ya figo cha hospitali hiyo mwanzoni mwa wiki hii.

Sababu za kuanza huduma hizo kabla ya nyingine, inaelezwa kuwa mkakati wa mkoa ni kuboresha afya ya mama na mtoto, kwa lengo la kuendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Awali, mipango waliojiwekea ilikuwa ni kufikia Julai mwaka huu ujenzi uwe umekamilika na kuanza kutoa huduma, lakini haikuwa hivyo na sasa itaanza kutoa huduma hizo mwezi ujao, huku ukamilishaji ukiendelea.

Historia ya ujenzi wa hospitali hiyo inaanzia miaka ya sabini wakati serikali ya awamu ya kwanza na sasa inatarajia kuanza kutoa huduma mwezi ujao, ndani ya serikali iliyopo.

Kuchelewa kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo kumechangiwa na mengi ambayo simulizi yake ni ndefu, lakini itoshe kusema kwamba, kukamilika kwake kutakuwa ni ukombozi kwa wakazi wa mkoa huo.

Hospitali hiyo inajengwa katika Kitongoji cha Kwangwa kilichopo Kusini mwa mji wa Musoma, ambao uko kando ya Ziwa Victoria, ikiwa ni makao makuu ya mkoa huo.

Ujenzi huo ulianza zaidi ya miaka 40 iliyopita, ili wakazi wa mkoa wa Mara na mikoa ya jirani wapate huduma bora za afya na kwa uhakika, safari hii serikali inataka kuhakikisha inakamilika haraka.

Mwishoni mwa mwaka jana ujenzi wa hospitali hiyo ulianza kwa kishindo baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuidhinisha zaidi ya Sh. bilioni 15 na sasa imefikia hatua ya kutaka kuanza kutoa huduma za awali.

Kuwapo kwa taarifa kwamba, hospitali hiyo itaanza kutoa huduma za awali mwezi ujao, ni habari njema kwa wakazi wa mkoa huo wilaya za Rorya, Tarime, Butiama, Serengeti, Musoma Mjini, Musoma na Serengeti.

Wakazi wa mkoa huo wamelazimika kila mara kwenda kupata huduma kubwa za afya katika Hospitali ya Rufani Bugando, jijini Mwanza, lakini sasa kuna nuru miezi michache ijayo, wataondokana na adha hiyo.

Hayo yapo bayana kwamba kuna kuanza kutoa huduma za awali ni dalili tosha kwamba kuna maendeleo mazuri ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambayo kama nilivyoeleza, ujenzi wake una historia ndefu.

Tayari mkuu huyo wa mkoa, ameshaweka wazi kwamba lengo la serikali kutoa mabilioni ya shilingi ni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo, ili kuhakikisha wakazi wa mkoa wa Mara na jirani wanapata huduma bora za afya na za uhakika.

Kutokana na lengo hilo, anamtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo afanye kazi usiku na mchana, ili kufanikisha kile ambacho kimekusudiwa na serikali hasa kuboresha afya za wakazi wa mkoa wa Mara.

Miongoni mwa vitu mkandarasi anatakiwa kuvikamilisha ni uwekaji wa umeme na barabara kwa kuwa ni muhimu, kuwapo hospitalini hapo ili walengwa ambao ni wananchi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika hospitali hiyo.

Ni sehemu ya utekelezaji kitaifa wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM), ulioasisiwa mwaka 2007 na kuanza kutumika mwaka mmoja baadaye, ambako Mara nayo haikuwa nyuma.