Kufanya kazi kwa mazoea hakufai zama hizi, tuache

08May 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kufanya kazi kwa mazoea hakufai zama hizi, tuache

MOJA ya vikwazo vinavyokwamisha gurudumu la maendeleo ya taifa ni cha watu kufanya kazi kwa mazoea.

Na ndiyo maana kinaendelea kupigwa vita kwa nguvu na serikali ya awamu ya tano, ili kisiwe sehemu ya utamaduni wa Mtanzania.

Kwa miongo sasa, suala la watu kufanya kazi zao kwa mazoea, likijionyesha kwa uwazi upande wa watumishi wa umma, limekuwa ni kama utamaduni wa kawaida.

Wahenga wanasema mazoea hujenga utamaduni na watalaam mbalimbali wanabainisha wazi kuwa mazoea ni adui mkuu wa ufanisi, iwe katika sekta ya umma au binafsi, iwe kwenye biashara mpya au za zamani.

Kwa nini? Kwa sababu katika zama hizi za mabadiliko makubwa ya kimaendeleo, zama za sayansi na teknolojia, zama za utandawazi, kunahitajika nidhamu ya kipekee ya utendaji kazi.

Nidhamu inayoongozwa na sheria, kanuni na taratibu za kitaasisi ili kuweza kufikia maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla.

Na kwa kulitambua hilo, baada ya awamu ya tano kuingia madarakani, Rais John Magufuli aliwaonya watumishi wa umma kuachana na utamaduni huo.

Akachukua hatua madhubuti za kuwatambua wale wote ambao hawakuendana na maelekezo yake ili kuonyesha anamaanisha anachokisema.

Dk. Magufuli akawataka wasaidizi wake kwenye wizara, idara, mashirika na taasisi za umma waongozwe na sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma zinazowataka wawatumikie wananchi kwa mujibu wa miongozo ya ofisi zao.

Hata hivyo, Muungwana anaona kwamba suala la kuchukulia vitu kwa mazoea ni kama imekuwa utamaduni si tu kwa watumishi wa umma, bali hata kwa wananchi wa kawaida.

Na matokeo yake, ndiyo hasara tunazoendelea kuzishuhudia kama nchi karibu kila siku.

Hasara za kupotea kwa maisha ya watu, wengine wakiambulia vilema vya maisha, uharibifu wa mali na hatimaye kuathiri uchumi wa nchi.

Kinachomshangaza Muungwana ni kwamba bado baadhi yetu tunaendelea na utamaduni huo wa kufanya kazi kwa mazoea na hatusikii la Mwadhini wala Mnadi swala na hivyo kuishia kusababisha majanga makubwa.

Na hiyo ni pamoja na maelekezo, maonyo na tahadhari zinazotolewa na viongozi wa serikali, wa dini, wa kimila na taasisi mbalimbali, yanayobainisha madhara ya kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa mfano tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini, zinaonyesha asilimia 75 ya ajali za barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu, huku asilimia 50 ya makosa hayo yakihusiana na mambo ya kibinadamu yanayofanywa na madereva.

Lakini mpaka sasa bado unakuta dereva wa Kitanzania anaendesha gari huku akiongea na simu, ‘akichati’ au akizungumza na mtu wa pembeni.

Bado unakuta dereva wa Kitanzania akipita kwenye taa ambazo hazimruhusu, hasimami kwenye alama za pundamilia ama akipita gari la mbele bila ya kuchukua tahadhari na matokeo yake ni ajali.

Ukimuuliza ana majibu yasiyo na mashiko, kwamba hajaanza leo kuendesha gari akiongea na simu au akichati.

Tunaambiwa kwa mfano tuachane na mazoea ya kuchoma moto misitu au kukata miti ovyo, kwani yanagharama kwa maisha yetu, hatusikii.

Takwimu za uhifadhi wa mazingira zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza takribani hekta 400,000 za misitu kila mwaka kutokana na miti kukatwa kwa sababu ya mazoea.

Matokeo yake ni mabadiliko ya tabianchi ambayo ndiyo chanzo cha mafuriko na vimbunga kama Idai au Kenneth tulivyovishuhudia nchi jirani za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.

Tunaambiwa na wataalamu wa afya tuweke mazingira yetu katika hali ya usafi ili kuepukana na magonjwa kama ya kuharisha na kipindupindu.

Lakini kutokana na mazoea ndio haohao tunaofungulia maji ya chooni na kuyaelekeza kwenye mitaro ya maji na hatimaye magonjwa ya kuambukiza.

Ni wakati sasa kwa Watanzania wa kuachana na utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea, ili kuliepusha taifa na majanga ambayo kimsingi yanaepukika.