Kufungiana miaka 5 si sawa

21May 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kufungiana miaka 5 si sawa

KWA mara nyingine tena tumeona watu wa familia ya soka wakifungiwa miaka mitano kujihusisha na masuala ya mpira wa miguu.

Mara ya mwisho ilikuwa ni mwanzoni mwa Aprili, 2021 wakati Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alipofungiwa miaka mitano, lakini alifunguliwa baadaye baada ya kukata rufaa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa soka nchini.

Tumeona wiki hii, Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Mbwana Makata na meneja wake, David Naftali wakifungiwa kujihusha na masuala ya soka kwa kipindi cha miaka mitano.

Adhabu hiyo ilitolewa na  Kamati ya Utendaji na Usimamizi wa Ligi, ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), baada ya kuwakuta na hatia ya kushawishi/kuamuru wachezaji wasiingie uwanjani kuanza mchezo huo,  tukio lililosababisha mchezo wa timu yao dhidi ya Namungo FC kutofanyika.

Mechi hiyo ilikuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi Mei 13,mwaka huu lakini haikuchezwa kwa sababu hizo.

Kamati ikadai baada ya kupokea taarifa na ilifanya uchunguzi na kubaini gari hilo lenye namba STL 3096 lilifika uwanjani hapo, lakini liliondoka kwa dharura kabla ya muda wa mchezo kuanza.

Ikasema waandaaji wa mchezo, Chama Cha Soka Mkoa wa Lindi (LIREFA), kwa kushirikiana na kamisaa walikubaliana kutafuta gari linaloweza kutumika kubeba majeruhi kabla gari hilo maalum halijarejea, lakini walipinga, pamoja na gari hilo kurejea kabla ya muda.

"Cha msingi nimeiona taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari, nadhani kuna utaratibu wa kupata barua rasmi na mambo mengine yatafuata. Adhabu nimeiona, nitajua la kufanya baada ya kukaa na kutafakari pale nitakapopata barua, kuangalia vifungu ambavyo vimetumika kunifungia, ndiyo nitajua sasa nifanye nini, kwa sasa siwezi kufanya au kuongea chochote, ila baadaye nikakapopata hiyo barua na kuona inaeleza nini, nikiona sijatendewa haki nitakata rufaa, kama nikiona ni sahihi kilichofanyika, basi nitajua la kufanya," alisema Makata siku moja tu baada ya kamati kutoa taarifa hiyo.

Naunga mkono adhabu kwa Makata kwa sababu alichokifanya hakikubaliki kwenye dunia ya sasa ya soka.

Soka kwa sasa ni biashara kubwa, watu wamelipa matangazo kwa ajili ya kuonyesha kwenye televisheni, kuna waliolipia ving'amuzi kwa ajili ya kuonyesha mpira, lakini kuna wale ambao wameshalipa viingilio kwenye mabaa, na vibanda umiza. Wote hawa wamepata hasara baada ya mechi hiyo kutoonyeshwa. Kila mtu analia kivyake.

Haya yote yamesababishwa na mtu mmoja au wawili kwa sababu zake za kutaka mechi isichezwe. Hapa adhabu ni lazima.

Hata hivyo, adhabu hiyo naiona ni kubwa mno. Adhabu kama hizo hutolewa kwa wapanga matokeo na  si vinginevyo.

Makata na mwenzake ni kweli wanastahili adhabu, lakini siyo ya kumfungia miaka mitano.

Nadhani bado Watanzania tunaendelea kuishi kwenye dhana za ujamaa, ambazo kwa sasa kwenye nchi yetu kwenye sehemu nyingi hazifanyi kazi.

Zamani soka lilikuwa ni burudani, kujenga afya, mwili, kudumisha upendo na umoja na si kama kama hivi sasa.

Ndiyo maana wachezaji, makocha walikuwa wako Simba, Yanga au Pan African, lakini walikuwa wanafanya kazi kwenye taasisi na mashirika mbalimbali ya umma.

Wanacheza au kufundisha huku wakifanya kazi. Kwa hiyo hata akifungiwa miaka mitano au kumi, anaendelea na maisha yake kama kawaida. Ni adhabu ambazo zilikuwa hazimuathiri kwenye maisha yake kama binadamu. Ndiyo maana wakati huo wachezaji walikuwa wakifungiwa miezi mitatu, sita au mwaka, lakini kwa sasa huwezi kuliona hilo hata hapa nchini, achilia mbali CAF na FIFA.

Lakini kwa dunia ya sasa soka ni ajira, ambayo mtu anaishi na kuendesha familia yake, ukimfungia kwa miaka hivyo si tu kutomtendea haki, ila unakiuka haki zake kama binadamu.

Mtu mwenye mke, watoto na familia, unapomfungia asifanye kazi anayoiweza, ni kama kumfunga mikono.

Mimi nilidhani kamati hiyo iangalie upya, hizo ni adhabu za kizamani sana, wakati huo soka haikuwa kazi rasmi.

Pia nashangazwa na kanuni hiyo kuwepo hadi leo. Nilitegemea wadau wa soka wanaoitwa ili kuzirekebisha kila msimu wangeipigia kelele iondolewe, lakini kumbe bado ipo.

Labda viongozi wa Simba na Yanga wao wanaona kanuni hiyo haiwezi kuwabana, lakini wa mikoani nao vipi? Wanaendelea kuiachia tu kanuni hii iliyopitwa na wakati na kuikumbuka pale inapowakuta?

Wanapofanyia marekebisho kanuni za kila mwaka nini wanachokifanya? Au wanachokumbuka ni kuitetea tu kanuni ya kuchukua pesa zote za mapato kwenye mechi ambazo Simba na Yanga zinacheza mikoani?.