Kufungua kesi ni hatua moja, tuzingatie maelekezo mengine

10Mar 2016
Beatrice Shayo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kufungua kesi ni hatua moja, tuzingatie maelekezo mengine

KESI za ubakaji hapa nchini zinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za mashahidi kushindwa kujitokeza kutoa ushahidi, hatua ambayo inaifanya mahakama kushindwa kuwatia hatiani watuhumiwa.

Kuna baadhi ya kesi za ubakaji ambazo hufunguliwa mahakamani zimekuwa hazina ushahidi licha ya kwamba kuna ukweli wa tukio husika.

Baada ya mtuhumiwa kuachiwa ndipo wananchi huanza kuilalamikia mahakama bila kufahamu kile ambacho kilikuwa kikiendelea mahakamani.

Imenilazimu kuzungumzia suala hilo, kwa kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakidhani ukishamfungulia mtu kesi basi ni kuiacha bila kuifuatilia.

Mbali na hilo wapo ambao hutakiwa kuwasilisha mashahidi wake mahakamani na kuamua kuingia mitini bila kuifuatili hali ambayo inailazimu hakimu ama jaji kumuachia mtuhumiwa kwa kukosekana ushahidi.

Unapofungua kesi mahakamani unatakiwa kuifuatilia kwa kujua tarehe ya kutajwa kesi pamoja na hatua nyingine zinazofuata mpaka maamuzi ya hukumu yanapofikia.

Kuna mtu mmoja alishtakiwa kwa kesi ya ubakaji baada ya muda kupita aliachiwa huru kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuwasilisha ushahidi ambao ungemtia hatiani mshtakiwa.

Ilielezwa kuwa kila ilipokuwa ikipangwa tarehe ya kesi hiyo, kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi upande wa mashtaka hawakujitokeza mahakamani.

Mahakama iliendelea kusogeza tarehe mbele ili kutoa nafasi kwa wahusika kuwasilisha ushahidi, lakini upande wa mashtaka hawakujitokeza katika suala hilo.

Mshitakiwa huyo alipoachiwa huru kutokana na kesi hiyo kufutwa, watu walianza kuhoji imekuwaje kaachiwa huku wakiitupia lawama mahakama kwamba haitendi haki. Hivi mahakama itende haki gani ambayo wananchi wenyewe hamjataka kuisaidia katika kuwasilisha ushahidi?

Ukisikiliza maelezo ya walalamikaji wanaeleza mtuhumiwa huyo ni kweli alibaka na ushahidi wa tukio hilo upo wazi, lakini wanashangazwa kwa nini mahakama haijatenda haki.

Katika hali ya kawaida, mahakama itawezaja kutenda haki pale ushahidi unapokesekana ni vigumu kujithibitisha yenyewe bila wahusika kutoa msaada katika kuwapeleka mashahidi na vielelezo vinavyotakiwa kumtia hatiani mtuhumiwa.

Haina maana kusema umefungua kesi na kuiachia mahakama itende haki bila ya mhusika kupeleka ushahidi, kwani tukio lilipokuwa linafanyika mahakama haikuwepo.

Mbali ya hilo, kuna baadhi ya kesi hufunguliwa mahakamani na kwenda kumalizana nje ya mahakama bila kuitaarifu Mahakama.

Utakuta mtoto amebakwa na ndugu yake ama jirani yake, familia husika zinakubaliana na kukaa meza ya mazungumzo kwa ajili ya kumalizana kwa kesi ama wengine humalizana kwa mtindo wa kifedha ili kuondoa fedheha mahakamani.

Katika hatua kama hiyo ya kukubali kukaa meza moja na kulimaliza bila kuwa na uchungu wa maumivu ya mtoto aliyoyapata pamoja na kuathiriwa kisaikolojia, naweza kusema ni kukosa utu na kuona ukatili aliofanyiwa mtoto ni sawa na thamani ya kiasi kadhaa cha fedha. Inauma sana.

Mwanao amefanyiwa ukatili halafu unakubali kirahisi kesi imalizike kwa njia ya fedha, tujitahidi unapofungua kesi kama hiyo, ni vizuri ikamalizika mahakamani na siyo kuicha kwa vile tu mnaonea haya.

Je, alivyokuwa akikifanya kitendo hicho kiovu kwa nini hakuona huruma kwa mtoto wako mpaka umkubalie kumsamehe. Tuangalie na uzito wa jambo tusikubali kudanganywa na fedha ambazo haziwezi kurudisha thamani ya utu wa mtu.

Tunaweza kutolea mfano kama mtoto huyo angeambukizwa ugonjwa kama wa ukimwi unawezaje kulinganisha maumivu hayo kwa fedha uliyoipata ama kushindwa kumfunga kwa vile tu ni ndugu yako.

Kiukweli unapofungua kesi yako ni muhimu kuhakikisha unapeleka mashahidi wa kutosha ili kuirahisishia mahakama kazi ya kutoa haki na siyo kuilaumu haijatenda haki wakati hakuna ushahidi uliowasilishwa.