Kufuta ‘Panya road’ iwe moja ya vipaumbele vya polisi wetu

09Jan 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kufuta ‘Panya road’ iwe moja ya vipaumbele vya polisi wetu

MOJA ya kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakati wa sikukuu za Mwaka mpya na Noel, ni kuhakikisha fukwe za wazi za Bahari ya Hindi zinakuwa salama muda wote.

Nyakati za sikukuu, fukwe za bahari hufurika watu ambao huenda kuogelea baharini, kupunga upepo na wengine kutembea katika dhima nzima ya kufurahia sikukuu husika.

Kwenye sikukuu ya mwaka mpya, nilitembelea fukwe mbalimbal za wazi ikiwamo maarufu ya Coco Beach, ambayo ilikuwa imefurika watu wa kila aina wakifurahia kwa kuogelea, kupunga upepo na kutembeatembea.

Wakati watu hao wakiendelea na hayo, kulikuwa na ulinzi wa polisi ambao walihakikisha kuna usalama wa kutosha wa raia na mali zao, ili kufuta historia ya matukio ya mara kwa mara ya uvamizi, vifo, majeruhi na wizi wa mali uliokuwa ukifanyika.

Safari hii ilipofika saa 12 jioni, polisi iliamuru watu wote watawanyike kutoka kwenye fukwe hiyo, isipokuwa waliokuwa wakinunua bidhaa na vyakula kutoka kwa wauzaji waliokuwa kando kando ya fukwe hiyo.

Katika doria hiyo, Polisi ilitumia mbwa, virungu na silaha ambazo kimsingi hazikutumika, lakini zilionyesha mamlaka, ujumbe kwa wananchi ukiwa utii bila shuruti.

Asilimia kubwa ya wananchi walifanya hivyo na baada ya muda fukwe ikawa haina watu kabisa.

Ulinzi na ufuatiliaji wa aina hii ni muhimu kwani umewezesha wananchi hususan watoto kuwa salama, tofauti na siku za nyuma.

Ilikuwa ni kawaida siku za nyuma kuona watoto wakiambatana na watu mbalimbali kwenda kwenye fukwe hizo.

Hata hivyo, kutokana na kukosekana kwa usimamizi kwa baadhi ya nyakati, watoto walikuwa wakiachwa waogelee wenyewe, hali iliyosababisha kupotea au kuzama wakati mwingine.

Kwa ufuatiliaji nilioushuhudia safari hii, nina hakika ni ngumu kusikia matukio ya vifo vya maji kwenye fukwe mbalimbali, uharibifu wa mali, wizi au watu kufanyiwa ukatili mwaka huu, kwa kuwa Polisi waliamua kujipanga vyema.

Miaka ya nyuma kulikuwa na matukio ya watoto wa kike kufanyiwa ukatili na vijana wanaokodisha matairi kwa ajili ya kuogelea au wanaowafundisha watu mbalimbali kuogelea.

Kilichokuwa kinafanyika ni kuwapeleka kwenye kina kirefu cha maji na kutishia kuwadhuru, ndipo vitendo vya ubakaji vilifanyika.

Matukio mengi ya aina hii wametendewa zaidi wasichana wa kazi ambao wengi wao nyakati za sikukuu huruhusiwa na ‘mabosi’ wao kwenda kutembea.

Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi ni ya kuungwa mkono kwa kuwa imesaidia kuepusha uwezekano wa kutokea madhara kwa wananchi.

Muungwana anaona kazi hii nzuri iliyofanyika katika fukwe sasa ielekezwe kudhibiti makundi ya Panya road yanayoibuka kwa baadhi ya nyakati na kufanya matukio ya uhalifu, kama ilivyotokea eneo la Tabata Kisukuru hivi karibuni.

Makundi haya yanaundwa na vijana wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 14 na kuendelea, wakitumia silaha za jadi kama mapanga, visu na mashoka kupora fedha, simu na vitu vingine vinavyoweza kubebeka kirahisi.

Muungwana anaamini kupitia intelejensia ya polisi, jeshi hili litasambaratisha makundi haya ya Panya road.

Ni vizuri polisi jamii katika mitaa mbalimbali kubeba vyema wajibu wake wa kushirikiana na jeshi la polisi kudhibiti matukio haya yanayoacha doa kwa kazi kubwa iliyofanywa na jeshi hili nchini.

Muungwana ana imani kubwa na jeshi hili ambalo limefaulu kusambaratisha uhalifu nchini mfano hai ikiwa ni mauaji yaliyokuwa yakifanyika mkoani Pwani, maeneo ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

Lakini pia limeweza kuangamiza ujambazi wa kutumia silaha na kuteka magari uliokuwa umeshamiri nchini.

Hivyo ni rai ya Muungwana kuwa katika mkondo huohuo uliofuta kabisa uhalifu nilioutaja, basi sasa kufuta makundi ya Panya road, iwe ni moja ya vipaumbele vyake.