Kuifanyia mapitio sera ya misitu kuna tija

10Jan 2018
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mjadala
Kuifanyia mapitio sera ya misitu kuna tija

HAKUNA shaka tena kwamba madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi yameanza kujidhihirisha wazi katika maeneo mengi nchini kwa hivi sasa.

Awali Muungwana alikuwa akisikia madhara yake katika nchi za wenzetu na hasa Ulaya, Marekani na mataifa kadhaa ya Bara la Asia, zaidi nchi za China na India.

Madhara dhahiri ya mabadiliko ya tabianchi ambayo tulikuwa tukiyasikia kwa wenzetu ni pamoja na ongezeko la joto duniani, uchafuzi wa hewa, ongezeko la kina cha maji baharini, ukame na mafuriko.

Hata hivyo, sasa si ya kusikia tu kwa wenzetu bali tumeyaona na tutaendelea kuyashuhudia karibu kila siku.

Mfano hai ni ukame uliokumba baadhi ya maeneo hapa nchini katika kipindi cha kilimo kilichopita ambapo kuna maeneo ambao hayakupata kabisa mazao.

Kwa mfano baadhi ya maeneo katika Kanda ya Ziwa hususani mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida, Mwanza, Geita na Kagera hayakupata kabisa mazao kutokana na ukame ambao ni zao la mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo hivyo, kuna maeneo yaliyokumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha uharibifu wa mazao mashambani, makazi, miundombinu na upotevu wa maisha ya watu.

Kimsingi hayo yote ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi. Jiji la Dar es Salaam ni mfano, kwani lilishuhudia mvua ikinyesha kila siku kipindi chote cha mwezi Mei mpaka ilipoingia Juni mwaka jana, kitu ambacho hakijawahi kuonekana kwa muda mrefu.

Vyanzo mbalimbali vinabainisha kuwa kuna sababu nyingi zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi tunayoyashuhudia, lakini nyingi ya sababu hizo zinaletwa na shughuli za binadamu.

Mojawapo ya sababu hizo ni ile ya ukataji ovyo wa miti ama misitu ambao hata hapa nchini unafanyika pamoja na kuwapo kwa mwongozo wa uvunaji, upatikanaji wa rasilimali na vibali vya uvunaji wa miti.

Mwongozo huo uliandaliwa mwaka 2007, ulitokana na changamoto zilizojitokeza kwenye shughuli nzima za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu kwenye miaka kati ya 1995 na 2000.

Kuna miongozo ya aina mbili iliyoandaliwa mmoja ukiangazia uvunaji endelevu na biashara ya mazao ya misitu yanayovunwa katika misitu ya asili na wa pili ukiangazia uvunaji endelevu wa mazao ya misitu yanayovunwa katika mashamba ya miti na misitu ya mikoko.

Miongozo hiyo ililenga kuweka utaratibu madhubuti wa kuzingatia sheria na utawala katika uvunaji endelevu na biashara ya mazao ya misitu na kuainisha mikakati ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu katika mashamba ya miti na misitu ya mikoko.

Miongozo yote miwili imetokana na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na Sheria ya Misitu Sura 323 ya mwaka 2002, pamoja na Matangazo ya Serikali Namba 69 na 70 ya mwaka 2006.

Lakini pamoja na kuwapo kwa miongozo hiyo bado ukataji miti nchini unaendelea kwa kasi kuliko kiwango cha hekta za kukata miti kinachoruhusiwa kwa mwaka kwa mujibu wa mwongozo.

Takwimu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zinaonyesha kwamba, kila mwaka kuna takribani hekta 372,000 za misitu zinazokatwa, ikiwa ni zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa.

Sasa katika hali kama hii, ni wazi kuwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi, yaani ukame, mafuriko, uchafuzi wa hewa na mengineyo kama tuliyoyashuhudia katika kipindi cha kilimo mwaka jana, hayawezi kuepukika.

Kwa maana nyingine, sera ya misitu ya mwaka 1998 na miongozo yake imeshindwa kumaliza tatizo la ukataji wa misitu ovyo.

Ndiyo maana Mjadala unakubaliana na hatua ya serikali ya kufanya mapitio mapya yanayoendelea sasa ya sera ya misitu, ili kuja na sera mpya itakayosaidia kumaliza tatizo la ukataji wa miti usiokubalika, ambao ni moja ya vyanzo vya mabadiliko ya tabianchi.