Kuisaka AFCON 2023 wachezaji wasichaguliwe kimazoea

25Apr 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kuisaka AFCON 2023 wachezaji wasichaguliwe kimazoea

TAYARI Watanzania wote wanajua kuwa timu yao ya Taifa, Taifa Stars imepangwa Kundi F kuelekea kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Baada ya droo iliyochezeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lenye Makao Makuu yake nchini Misri, Stars iliwekwa kwenye kundi moja na timu za Algeria, Uganda na Niger.

Ni kweli kuwa si kundi jepesi kwa sababu Algeria ni moja kati ya timu vigogo vya soka barani Afrika, huku Uganda ikiwa timu ambayo kwa kawaida inaipa shida sana Tanzania upande wa soka kwenye mechi zote za timu za wakubwa, vijana chini ya miaka 23, 20, 17 na hata timu za wanawake.

Takwimu zinaongea kuwa Uganda ilikuwa mlima rahisi kwenye mechi ambayo Stars ilishinda na kwenda fainali za AFCON 2019 nchini Misri, lakini kabla ya hapo ulikuwa ni mlima mkubwa mno.

Kihistoria tu ni mara chache sana kwa Tanzania kuifunga Uganda kuliko wao kuifunga Stars. Kama ingekuwa ni Kenya, angalau.

Niger ni timu ambayo kwenye makaratasi inaonekana kama ni timu mchekea, lakini sivyo. Kwa sasa soka la Afrika Magharibi limekuwa na kuenea sana. Ni kama wameambukizana. Zamani Afrika Magharibi timu tishio zilikuwa ni Nigeria, Ghana na Cameroon, lakini baadaye zilianza kuja timu kama Ivory Coast na kufuatia na zingine mpaka zile nchi ndogo ndogo nazo kwa sasa zimekuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya, huku nchi za ukanda huo zikiwa zimeendelea kwa kuweka akademi nyingi za michezo.

Ni kwamba wachezaji wa mwanzo wa kulipwa kwenye nchi za Afrika Magharibi wengi wametengeneza akademi zao kwa kuzisambaza kwenye nchi mbalimbali jirani, hivyo nchi kama Niger si ya kubeza kwani ina wachezaji wenye vipaji vikubwa.

Hata hivyo, hakuna cha kuhofia kwa Stars kama itaanza maandalizi mapema na ya uhakika. Pamoja nayo, ni kwamba ili Watanzania tufuzu ni lazima uchaguzi wa wachezaji ufanywe kwa makini.

Simfundishi Kocha Mkuu, Kim Paulsen kazi, kwa sababu ndiyo kazi yake, lakini ni kwamba wachezaji wasichaguliwe kimazoea.

Tumeaona huko nyuma baadhi ya wachezaji ambao wamefanya vema na sasa hata kwenye timu zao hawapangwi, lakini wamekuwa wakiitwa.

Ili tufuze kwa sasa, umakini unatakiwa kwa kuita wachezaji ambao wanafanya vema kwa sasa na si kwenye klabu kubwa, hata zile ndogo. Hatupaswi kung'ang'ania wachezaji kutokana na majina yao kwa yale waliyoyafanya zamani.

Mfano mchezaji George Mpole, anaichezea Geita Gold, amechaguliwa kwa mara ya kwanza tu, lakini vitu alivyovifanya ni hatari na mfano wa kuigwa. Wala huwezi kuamini bado ni mchanga kwenye kikosi hicho.

Aziz Andambwile wa Mbeya City, ilifika wakati kwenye mechi za Stars zilizo kwenye Kalenda ya FIFA zilizocheza hivi karibuni alikuwa akishangiliwa na mashabiki uwanja mzima, kila anapogusa mpira.

Tumeona pia kuna baadhi ya wachezaji wapya kutoka nje ya nchi, ambao nao kama taratibu zitafanyika wanaweza pia kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.

Paulsen ameonekana kubadilika kwa sasa kwenye kuchagua wachezaji katika mechi hizi, lakini isiwe kwenye mechi za kirafiki na kwenye mashindano halisi akachukua wachezaji kwa majina yao au klabu zao.

Kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa ukitazama, ukiondoa washambuliaji, kuna timu zina wachezaji wazuri sana, ambao wanachokosa ni mafunzo kidogo tu ili viwango vyao viwe wazi zaidi.

Nina uhakika, kwa kikosi nilichokiona kwenye mechi dhidi ya Afrika ya Kati na Sudan na kiwango kile, kama wataongezwa baadhi ya wachezaji wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu, fainali za AFCON 2023, Stars inaweza kuwamo.