Kuizoea rushwa ni hatari kwa ustawi wa jamii

09Aug 2016
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Kuizoea rushwa ni hatari kwa ustawi wa jamii

RUSHWA inaua uchumi wa nchi. Rushwa inafanya fedha chache au hata nyingi tunazozalisha zisifanye maendeleo ya umma ila kutajirisha wachache ambao hawana uchungu.

Lakini sioni uchungu tena kwa sababu licha ya hasara zote hizo ambazo rushwa inasababisha, tulifikia wakati ikawa kama hakuna anayeona kuwa ni hasara.

Wale wanaotakiwa kuchukua hatua wakawa wanayamaza kimya. Wanaotakiwa kuchukua hatua hawachukui, mimi nikiona uchungu zaidi ya kujitafutia ugonjwa wa moyo nataka nini tena jamani!

Katika maisha yangu nimeona faida ya kuishi bila rushwa, na hasara ya kuishi kwa rushwa.

Rushwa inasababisha kutokuwepo kwa uwajibikaji. Watu hawaishi kwa kuogopa kuwa wananchi wenzao wataathirika kutokana na ufisadi wanaoshiriki, bali kwa kujaribu kuwa wajanja wasikamatwe wakati wa kutimiza haja zao za wizi na kadhalika, hata kama watajulikana baadaye kuwa utajiri wao una asili mbovu. Nani anajali.

Mfumo wa maadili ukawa umepuuzwa na hakuna aliyejali kama maadili ni kitu chema. Tunapoingia katika mfumo wa ujasiriamali wa wizi na rushwa, hakuna anayejali maadili, ukijali maadili ni kama utabaki peke yako ukiwa maskini.

Lakini naangali sasa, jinsi ambavyo dawa hazifiki hospitali; fedha za miradi hazifiki kwa walengwa; vitabu vya kiada vilivyopitishwa ni vile visivyofaa kabisa; achilia mbali habari tunazozisikia kuwa Idara za serikali zikaajiri watu wasiofaa, na wanapokuja kutimuliwa wameshaitia nchi hasara ya fedha.

Lakini hata wale waliofaa kuajiriwa kwa sifa zao nao wakata tamaa na kuchanganyikiwa kabisa kiasi kwamba hawakuweza kufanya kitu tena.

Uwezo wao wa kuchangia taifa ukatelekezwa na nchi ikawakosa. Kisa, kuna watu ambao ajira zinapotokea hufikiria ndugu zao ambao wengi hawana uwezo wa kuzifanya kazi hizo.

Naambiwa nchi hii kupitia idara zake mbalimbali hupata nafasi za kusomesha watoto wa Taifa hili nje.

Lakini baadhi ya wakubwa wanaopata taarifa hizo za masomo (scholarship), huzikalia na kusababisha kupoteza nafasi hizo kwa makumi kila mwaka, na kama zinajazwa basi na watoto wa wanaojulikana ambao wengine uwezo wao ni mdogo wa kuzifanya kwa ufanisi.

Ufisadi ni ujanja, na tunaambiwa ujanja ni kuwahi na kupata hata kama huna uwezo wa kufanikisha jambo unaloambiwa ulifanye; hata kama kupata huko kunaumiza wananchi wengine; kupata kwa siku hizi ni kufumba macho unapowatemea mate wenzako; unahisi umekanyaga jiwe unapowatimba wenzako kwa mabuti yako; unahisi kuwa wanaobugia dawa za kulevya unazoziuza walijitakia wewe unayezileta nchini hukuwaambia waje wanunue.

Kwa wale waliokupigia kura walikuwa wajinga kukubali rushwa ya ubwabwa, kofia, khanga na soda wakati wa uchaguzi na kukupatia kura zao; Rushwa haijali kuumia kwa wananchi, hakujali kuharibika kwa miundo mbinu.

Wenye kupenda ufisadi wanatambua kabisa kuwa, wanachokifanya kinaharibu barabara zetu, malori yao makubwa yanaua uchumi na ingekuwa vizuri wakasafirisha mizigo yao mikubwa kwa meli au treni.

Lakini nani anajali kuwa kuna reli ambayo pato lake lingekuza taifa, ni chanzo kikubwa cha ajira kwa wananchi na pato kwa serikali?. Nchi inaendeshwa kwa kitu gani kama sio kuhakikisha kuwa pato linaingia ndani ya serikali.

Sasa wale walioko jikoni ndio wakawa wanafanya makusudi chakula kisipikwe, sisi tulio nje tunakula nini?

Siku moja nilikuwa nazungumza na dereva wa bodaboda baada ya kumuona akilipa ushuru kwa mtu ili aruhusiwe kupandisha abiria wanaoshuka kwenye basi eneo hilo.

Akasema hawezi kushitaki kokote kwa sababu anajua hata akiipeleka kesi polisi hatashinda; ukweli wake hautaweza kushinda uwongo wa mtoza ushuru anayekuja na fedha. Yeye ukweli wake utakuwa kweli kama akiufunganisha na fedha na ziwe zaidi ya yule anayemshitaki.

Hapa ndipo tulipofikishwa; ukiangalia hata magari yanavyoendeshwa utaona jinsi haki inavyominywa, kuvuja sheria, kutothamini wengine, baadhi ya askari kupokea rushwa. Nchi ikaenda mrama, lakini nani aliona uchungu, na kwa nini nione uchungu?

[email protected], 0766959349