Kukabiliana na wanaouza mali shauri likiwa kortini

07Dec 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Kukabiliana na wanaouza mali shauri likiwa kortini

INAWEZEKANA umefungua shauri la ndoa, au una maombi ya talaka, mgawanyo wa mali ,malezi ya watoto au vyote.

Wakati huo ambao kesi haijaanza, au imeanza kusikilizwa lakini haijaisha, unahisi au unaona mali za ndoa ambazo pengine zinatakiwa kugawanywa zikiwa katika hatari ya kuuzwa, kugawiwa, kuharibiwa au kubadilishwa umiliki. Unaona bayana kuwa shauri litakapomalizika patakuwa hakuna kitu au kitakacho kuwepo ni kidogo.

Unajihoji nini ufanye kisheria katika mazingira kama haya ili kuokoa mali hizi, ili usije kukosa haki yako kesi itakapokwisha? Hiki ndicho kitakachozungumzwa hapa na safu hii ya mionzi ya sheria.

Kitu unachotakiwa kufanya kimeelezwa katika kifungu cha 138( 1 ) cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Kifungu kinasema pale ambapo mtu ataona kuna hatari ya mali kuuzwa, kuharibiwa au kupotezwa kwa namna yoyote ile basi atakuwa na haki ya kuomba mahakama itoe zuio la muda kumzuia mtu yeyote kuiuza, kuibadili umiliki, kuiharibu, kutoa zawadi au kufanya kitu kingine chochote chenye lengo la kuathiri mali hizo.

Kitu hiki pia kimeelezwa mara nyingi na Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Rufani katika kesi mbalimbali mojawapo ikiwa ni hii ya Elizabeth Gikene Vs John Zakharia Gikene shauri la Ndoa Namba 5/2004.

Kwa hiyo utakachofanya, kwanza kama kesi iko mahakama ya wilaya, ya hakimu mkazi, au mahakama kuu na unaye wakili anayekuwakilisha cha kwanza ni kumwambia kuhusu huo wasiwasi wako wa dalili za kupotezwa kwa mali lakini pia muombe mfanye utaratibu wa zuio hili. Bila shaka mtakubaliana kuhusu hilo.

Pili, kama shauri liko katika mahakama zilizotajwa hapo juu lakini hauna wakili anayekuwakilisha ni muhimu kumtafuta wakili yeyote umweleze wasiwasi wako na kumuomba akuandalie maombi ya zuio hili ili uzuie mali wakati shauri la msingi likisubiriwa kuisha. Mtaelewana kuhusu hili na mtafanya kama mlivyoelewana.

Maombi haya ni lazima kumtafuta wakili hata wa kukuandikia tu halafu wewe ukaenda mwenyewe mahakamani, kwasababu mtu ambaye sio Wakili sio rahisi kuandaa maombi haya.

Zaidi, kama kesi iko mahakama ya mwanzo hapo hukuna haja ya wakili kuandaliwa maombi rasmi bali ni kumweleza hakimu anayesikiliza shauri lako kwa mdomo kuhusu wasiwasi wako wa mali kuharibiwa na utamuomba atoe zuio la muda mali zisiguswe mpaka shauri la msingi liishe.

Kama utaweza kumtajia hata kifungu cha sheria kilichoelezwa na Makala hii au pamoja na hiyo kesi iliyotajwa ya Gikene ambavyo kwa pamoja vinaruhusu maombi haya ya zuio.

Kama utashindwa kufanya hivyo ni vyema kumwabia hakimu bila kumtajia kifungu, atatoa msaada.

Mara nyingi tatizo hili la kuharibiwa mali wakati shauri likiendelea mahakamani limekuwa likiwakumba zaidi kinamama.

Anapofungua shauri kuomba talaka au mgawanyo wa mali basi mwanaume huanza kuuza baadhi ya mali au kuzibadilisha umiliki ili wakati shauri linaisha mali ziwe zimeisha ili mwanamke asiambulie kitu, au kwa lengo kuwa ikifikia ushahidi kila mali itakayotajwa na mwanamke kuwa ni ya ndoa akatae kuwa sio yake au ilishauzwa.

Hata wanaume nao hukumbwa na tatizo hili lakini zaidi ni wanawake. Basi hili lisikupe tabu tena kwa kuwa dawa yake ndiyo hiyo.

Na kwa taarifa tu, mali ikizuiliwa na mahakama isiuzwe na mtu akaendelea na uuzaji au kuiharibu adhabu yake ni kifungo cha miezi sita jela kwa kuidharau mahakama.

Lakini pia yule aliyenunua anakuwa amepoteza hela yake kwakuwa amenunua mali ambayo imezuiwa na mahakama na hivyo ni batili. Basi ni vyema kuchukua hatua na kulinda haki na mali kwa mujibu wa sheria.