Kulikoni biashara ya mifuko plastiki nchini?

21Feb 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kulikoni biashara ya mifuko plastiki nchini?

MIFUKO ya plastiki ilipata umaarufu mkubwa nchini, kutokana na unafuu wa bei yake, hali ambayo ilisababisha watu wengi kupenda kutumia kubebea bidhaa mbalimbali madukani na sokoni.

Kulikuwapo kundi kubwa la vijana waliokuwa wafanyabiashara wa mifuko hiyo, iliyopatikana kwa wingi karibu maeneo yote ya mijini; sokoni, madukani na wapo wauzaji walioufuata, huku baadhi yao wakitafutia wateja mitaani.

Hata hivyo, Juni Mosi mwaka jana, serikali ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya mifuko hiyo, ikiwa tayari imeandaa mbadala wake, kwa lengo la kulinda na kutunza mazingira.

Tangu wakati huo mifuko mbadala inayotengenezwa nchini, ndiyo imekuwa ikitumiwa na Watanzania kwa kubeba vitu mbalimbali na hasa wanapokwenda kununua mahitaji dukani au sokoni.

Wakati mifuko hiyo inayotengenezwa nchini, ikiendelea kutumiwa na wananchi, imebainishwa kuwa kuna mifuko ya plastiki inayoingizwa sokoni kinyemela, kutoka nchi za jirani na kuanza kutumiwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Zungu, anaonya wananchi kuchukuliwa hatua kwa kuhujumu uchumi.

Zungu anasema, mifuko hiyo siyo salama wala imara anawataka Watanzania kuipenda mifuko ya kwao ya asili, kuchangia kodi kwa ajili ya maendeleo yao.

Anasema, wamebaini mifuko ya plastiki, imeshaanza kurudi na msisitizo wake ni kwamba wananchi waiache, badala yake wajikite kutumia mbadala wake, ambayo inatengenezwa na viwanda vya chini.

Kutokana na maelezo ya waziri, ni kwamba kuna haja ya kuziba njia zote za panya ambazo zinatumika kuingiza bidhaa kinyemela ili kulinda bidhaa za hapa nchini pamoja na afya za Watanzania.

Bidhaa ambazo zimepigwa marufuku nchini, haziwezi kuingizwa kihalali, badala yake wahusika watatumia njia za panya, ambazo wanaamini kwamba hakuna mtu wa kuwakagua.

Hivyo, waziri aweke mtego kila eneo ambalo anadhani kwamba linaweza kuwa ni uchochoro wa kupitishia bidhaa au biashara isiyofaa na kuingizwa nchini, ili iwe rahisi kuwanasa wahusika na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Watanzania nao kwa upande wao wanatakiwa kushiriki katika vita hii ya biashara kwa kuwafichua wahusika wa uhalifu huu ili kuhakikisha mifuko inayotengezwa nchini inaendelea kupata soko.

Inashangaza kusikia mifuko ya plastiki imeanza kuingizwa kutoka nchi jirani na kuuzwa sokoni kana kwamba hakuna marufuku, wanaofanya hivyo wanataka kuirudisha nyuma Tanzania.

Inawezekana mifuko hiyo imepata soko kutokana na Watanzania wenyewe kuichangamkia, labda kwa unafuu wa bei, ila bado watambue ni hatari, hivyo wasiangalie unafuu tu bali usalama wa afya zao.

Serikali iliondoa biashara ya mifuko hiyo sokoni na kuleta mbadala wake, kutokana na ukweli kwamba ina madhara, sasa wanapojitokeza baadhi ya watu na kuiingiza kinyemela, hawawatakii mema Watanzania.

Biashara ya mifuko ya plastiki inapigwa vita katika nchini mbalimbali duniani ingawa ina fursa za kiuchumi kutokana na watu wengi kuiuza, lakini inalazimu kuachana nayo kutokana na madhara yake.

Kimsingi, wataalamu wa mazingira wanasema, mifuko mingi ya plastiki haiozi hata inapofukiwa ardhini na kuifanya ardhi ikose rutuba na wakati mwingine, inasababisha ardhi hiyo isifae kwa kilimo.

Aidha, mifuko hiyo inaweza kuanza kuoza baada ya miaka 20 au zaidi na kwamba, hata wanyama kama ng'ombe, kondoo, mbuzi na wengine wa aina hiyo wanaweza kufa wanapokula mifuko hiyo.

Wanyama hao wanaweza kula kutokana na ukweli kwamba wapo watu wanaoitupa ikiwa na mabaki ya chakula, hivyo wanaweza kuimeza pamoja na hicho chakula na mwisho wa siku wakafa.

Kikubwa, Watanzania walioachana na mifuko hiyo, wasikubali kurudishwa nyuma na wachache wanaotaka kujinuifaisha, bali waendelee kutumia mbadala, katika ambavyo serikali inaelekeza.

Ni muhimu kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa nchini ni zile zinazotakiwa kwa manufaa ya afya za Watanzania, pia kulinda na kutunza mazingira. Hivyo ni vyema kuwafichua wahusika, ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Tukumbuke onyo la waziri, hivyo wanaoingiza mifuko na wanaootumia, watambue kuwa wanajiweka katika mazingira ya kwenye hatia. Watafakari, kisha wachukue hatua za kuachana na biashara hiyo.