Kulikoni uchafu huu bucha za Tandale?

07Dec 2017
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kulikoni uchafu huu bucha za Tandale?

USAFI wa mazingira katika sehemu ya biashara ni kitu muhimu sana kwa afya ya walaji.

Kama sehemu ya kufanyia biashara inakuwa chafu ni hali hiyo inayoweza kuhatarisha afya ya mlaji.

Inasikitisha sana kuona baadhi ya bucha za nyama za barabarani na maeneo mengine ya  Tandale, jijini Dar es Salaam yanafanya biashara katika mazingira machafu bila ya kujali afya ya mlaji.

Kuna bucha zinauza nyama katika hali ya kushangaza, zikiwa mbele ya mitaro yenye maji machafu na zinaendelea kutoa huduma bila ya kujali afya za walaji.

Ukiangalia maji ni machafu, halafu kuna harufu kali, lakini hawalioni hilo na wanaendelea kuuza nyama katika maeneo hayo ambayo sio rafiki hata kidogo.

Maji hayo ni machafu na yananuka, lakini bucha zilizopo hapo zinaendelea kutoa huduma kwa wateja bila ya kufunga milango, wakati wanajua wako katika maeneo hatarishi kiafya.

Hivi mamlaka husika zipo wapi kuwachukulia hatua wenye bucha hizo, ambao wanafanyabiashara katika maeneo hatarishi kwa afya ya mlaji?

Kinachotakiwa hapa ni kuhakikisha biashara zinafanyika katika maeneo mazuri na yasiyo na uchafu kwa ajili ya kulinda afya ya mlaji.

Kama hatua hazitachukuliwa kwa bucha hizo, hali ya kuendelea kuwalisha wananchi nyama chafu itaendelea kila siku.

Ni vyema tupende kujali afya za walaji kwanza, ambao ndio tunawafanya wao wawe na kipato. Inatakiwa mamlaka husika zinazosimamia miradi hiyo, ziache kukaa ofisini na badala yake kutembelea maeneo ya biashara kuona kama huduma inayotolewa kwa wateja ni sahihi au la.

Kama wahusika wenye mamlaka wataendelea kukaa tu ofisini, daima hatuwezi kujua mambo yanayoendelea huko nje.

Jamii pia katika nafasi yao ina wajibu wa kutoa taarifa katika maeneo husika, kwamba hawaridhiki na huduma zinazotolewa na wafanyabiashara katika maeneo hayo.

Kama jamii nayo itaendelea kuona na kupuuzia suala hilo, litazidi kuendelea siku hadi siku kwa kutoa huduma zisizo na ubora kwa jamii.

Iwapo kuna bucha zinazotoa huduma katika maeneo ya usafi, kwa nini jamii wanajamii msiende kufuata huduma huko na mnaendelea kununua nyama katika hizo bucha ambazo zimezungukwa na mitaro iliyo na maji machafu?Kama jamii mkafikia uamuzi wa kukataa kununua nyama katika maeneo na mkasema biashara ifanyike katika maeneo mazuri, hata hao wauzaji hawataendelea kuuza nyama na bidhaa zingine katika sehemu hizo.

Nasema, kama jamii mtaendelea kuwaunga mkono katika hiyo biashara inayofanyika maeneo machafu, daima mtaendelea kula uchafu na siku msishangae kuna siku mtajikuta nanyi mnatumbukia katika ulingo wa magonjwa.

Kwanza, katika kata zetu kuna ofisi za wanaohusika na afya katika ngazi ya serikali za mitaa karibu, wakiwa na wajibu wa kuwachukulia hatua wanaofanya biashara, katika maeneo yasiyokuwa na sifa au vigezo stahiki, hata kuwachukulia hatua wanaoatiririsha maji majumbani.

Ikumbukwe kuwa, kuzembea kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaowalisha vyakula vichafu wananchi inahitajika kuwa kazi endelevu na si kuungoja ugonjwa unapoingia, ndipo hatua inachukuliwa kwa kuyafungia maeneo hayo ya biashara ambayo yamefungiwa macho kwa muda mrefu.

Suala la usafi linatakiwa kuangaliwa kila siku na kila wakati, ili ikibainika kasoro au mtu anafanya biashara katika maeneo yasiyofaa, ichukuliwe hatua mara moja bila ya kusubiri mlipuko wa magonjwa.

Serikali imekuwa ikipambana na suala la utunzaji mazingira kwa ajili ya kuwanusuru watu wasipate magonjwa, hivyo hili ni suala muhimu la kuchukuliwa hatua.

Nasema, ni jukumu letu kuhakikisha tunaiunga mkono katika kupambana na hali hiyo na sio kusubiri milipuko ya magonjwa inavyoanza, nasi tuanze kupambana.