Kulikoni wimbi hili ubunge, udiwani CCM?

15Jul 2020
Mary Geofrey
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kulikoni wimbi hili ubunge, udiwani CCM?

UCHAGUZI mkuu wa mwaka huu unashuhudia wanachama wengi kuanzia wasanii wa muziki, waigizaji na viongozi mbalimbali kujitokeza kutaka nafasi za ubunge na udiwani.

Ni haki ya kila raia na mwanachama mwenye sifa za kuwania nafasi hizo kufanya hivyo, lakini swali tunalojiuliza ni sababu zipi zimefanya msululu wa wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi huo?

Je, ni demkorasia iliyopo ndani ya chama, kuondolowa kwa mfumo wa miungu watu ndani ya chama kulikokuwa kunawafanya wenye nacho ndio wanapata na wasiyo nacho hawapati hata kama wana sifa zinazokubalika ndani na nje ya chama?

Yote haya yanaweza kuwa ni maswali yenye majibu sahihi ndani yake kwa sababu siku moja kabla ya kuanza mchakato wa uchukuaji fomu ulioanza jana na utakaomalizika Ijumaa ya wiki hii.

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Hamphrey Polepole, anaeleza kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa kumpata mgombea urais Tanzania na Zanzibar uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, wamefanya mabadiliko katika katiba ya CCM ili kupanua wigo wa demokrasia.

Anasema mkutano mkuu wa kata ambao awali ulijumuisha watu wachache kwa sasa utakuwa na wajumbe wapya wanaoingia katika kikao hicho ambao pia ni wenyeviti wa mashina yote katika kata husika ambao wanajulikana, pia mabalozi nao watapiga kura za maoni.

Kwa upande wa ngazi ya jimbo au uwakilishi, wataanza na Mkutano Mkuu wa Jimbo ambao wagombea wote wataingia na wataeleza kwa nini wanataka kupewa dhamana ya uwakilishi na CCM kisha kamati za siasa za ngazi mbalimbali zitafuata utaratibu kwa kuweka mapendekezo mpaka kufikia Halmashauri Kuu ya Taifa itakayoamua jina moja.

Polepole anaeleza kuwa wamejifunza kutoka katika mchakato wa kupata ugombea wa urais walioufanya hivi karibuni. Anaeleza kuwa mchakato wa upigaji kura katika chama hicho utakuwa wa wazi ili kuepusha malalamiko. Hivyo, wanataka uchaguzi ndani ya chama hicho kuwa huru na haki.

Sambamba na hilo, Polepole anaeleza utaratibu wa mawasiliano ndani ya chama na kubainisha kuwa hivi karibuni wataeleza sehemu ambayo taarifa za uchaguzi zitapatikana.

Suala hili na kuweka wazi mchakato wa upigaji kura ni wazi kuwa utaondoa makundi ndani ya chama na kuwaleta pamoja wanachama mara baada ya kumpata mgombea ambaye atawakilisha jimbo au kata.

Tofauti na awali watiania waliokatwa walibaki na vinyongo vinavyowagawanya na mwisho kumalizia hasira zao kwa kuwapigia kura wagombea wa upinzani. “Bora tukose wote ndiyo ilikuwa kauli ya waliokosa. Ni wazi kuwa utaratibu wa mwaka huu, hautawaga wana-CCM.” Anasema.

Akisoma kipengele cha kanuni ya uongozi wa maadili ya chama kwa upande wa haki za wanachama, Polepole anasema mwanachama atakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi endapo kugombea nafasi nyingi kuitasababisha kuzorota kwa uhai wa chama, hatateuliwa.

Aidha, anatahadharisha wagombea na watiania kuepuka vitendo vinavyokatazwa na chama kama kuweka mabango na kutumia vipeperushi kuwa haviruhusiwi kwa sababu ni sawa na kuanza kampeni kabla ya wakati.

Licha ya CCM kuweka wazi kanuni na taratibu za kuwapata wagombea hawa ni muhimu kila aliyechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kuwa sehemu ya ushindani kuwa atambue kuna kukosa na kupata.

Kadhalika wanaopata watambue wazi kuwa ilikuwa ni lazima apatikane mmoja na wengine wajipange kwa ajili ya kukitafutia chama ushindi kwa maslahi ya wote.