Kunahitajika elimu zaidi ya matumizi ‘zebra’ barabarani

16Oct 2020
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kunahitajika elimu zaidi ya matumizi ‘zebra’ barabarani

KIVUKO cha watembea kwa miguu (zebra crossing), maarufu pundamilia, ni alama maalumu inayochorwa kwa rangi nyeupe barabarani kwa watu kuvuka.

Katika barabara zote zilizo na lami na kuwa na alama hiyo, wanalindwa na Sheria ya Usalama Barabarani.

Pamoja na hilo, kuna baadhi ya wenye vyombo vya moto kutoheshimu vivuko hivi na kusababisha ajali.

Madereva wa magari na bodaboda, ingawa kwa kiasi kikubwa nawaingiza katika kundi kubwa la wanaoendesha vizuri, wapo wachache kati yao wasioheshimu nidhamu na sheria za barabarani na katika nafasi ya pekee, penye alama za pundamilia.

Ukiwa mtumiaji wa barabara unapoenda kwenye shughuli zako za kila siku, hasa maeneo ya mijini utashuhudia hili, licha ya kuwapo nadharia ya madereva wengi wa magari hivi sasa wameelimika na kuheshimu maeneo haya.

Shida kubwa huwa naishuhudia kwa waendeshaji bodaboda, ambao ni wazito penye alama hizo za kiusalama. Baadhi hawasimami, ilhali wamekuta magari yamesimama mahali hapo, kuruhusu watu kuvuka.

Ndugu hawa wa bodaboda, wana miongozo pori ya kwao hata usishangae, taa za kuongoza magari ikiwaka nyekundu wao wanaona maana yake ‘vuka’ na kijani au njano anaweza akasimama.

Licha ya bodaboda kuajiri vijana wapatao milioni 1.5 nchini, huku usafiri huo ukitegemewa na watu wengi hususan makazi ya mijini ili kurahisisha safari, elimu ya kuziheshimu zebra zinapaswa ziendelee kutolewa.

Ajira hii kubwa kwa vijana, wanapaswa waelimishwe kuhusu matumizi na kanuni bora za barabarani, ili isiwe na madhara kwa jamii, kwa kuwa ajali zina madhara makubwa ya kiafya katika jamii.

Hapo kuna hesabu ya ulemavu, vifo na hata kuongeza idadi ya wategemezi, katika hali ambayo huenda ingezuilika.

Ajira hii isiyo rasmi, inakadiriwa iwapo bodaboda mmoja akifanyakazi ya Sh. 5,000 kwa siku ikizidishwa mara idadi yao milioni moja na nusu, kuna makusanyo ya fedha wastani wa shilingi bilioni 7.5 kila siku.

Ni hesabu kubwa ya mapato na kwa maana hiyo, ni shughuli serikali inapaswa kuendelea kudumisha, kuptoa maboresho ya usalama barabarani.

Utamaduni wa zebra haukuanza miaka ya karibuni, kwani historia inaonyesha takribani miongo sita tangu kuanzishwa huko nchini Uingereza.

Takwimu za taasisi hiyo zinaonyesha kati ya majeruhi 2,223 waliolazwa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Muhimbili (MOI), mwaka 2016, zaidi ya majeruhi 1,100 wa barabarani waliumizwa kupitia bodaboda.

Jiji la Dar es Salaam, lina wakazi takribani milioni tano na kuna matumizi ya usafiri wa aina tofauti, ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, linasema nusu ya ajali zote zilizotokea nchini, asilimia 53 zilitokea jijini Dar es Salaam kati ya Januari na Machi mwaka 2019.

Linasema kati ya ajali hizo 776 zilizotokea nchini kwa kipindi hicho, ajali 416 zilitokea Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2016 zinasema kuwa watu milioni 1.4 walipoteza maisha katika ajali za magari duniani.

Hapo inajenga ujumbe wa kiusalama kwamba, wakati watembea kwa miguu wakizingatia kuvuka katika alama ya zebra, barabarani, ni wajibu wa madereva kuheshimu kila waonapo dalili ya anayetaka kuvuka, ili wampishe avuke.

Wataalamu wa masuala ya barabarani, wanaeleza kuwa kila aliye jirani na zebra au anayetarajia kuvuka aheshimiwe kwani amefuata sheria.

Hatari za ajali barabarani katika nchi zinazoendelea, ziko kiwango cha juu kwa mara tatu zaidi, huku WHO ikisema kwamba kuna vifo 27 kwa kila watu 1000.

Vifo vya barabarani katika nchi za Afrika ni mara tatu zaidi ya ajali zinazotokea barani Ulaya, ambako kuna ajali chache zaidi.

Ripoti ya WHO iliyotolewa mwaka 2018, inabainisha kuwa Sheria za Tanzania kwa upande wa usalama barabarani zina upungufu katika kudhibiti usalama barabarani, katika baadhi ya maeneo.

Kuna shida kuhusiana na tabia ya kuruhusu ulevi mkubwa kwa madereva, jambo ambalo ni hatarishi.

Tanzania imeweka ukomo wa kilevi kuwa ni wastani kitaalamu gramu 0.8 kwa kila desimali lita (0.08g/dl), lakini WHO inaeleza dereva mwenye kiwango hicho cha ulevi anakuwa hatarini kupata ajali mara nne zaidi ya yule ambaye hajatumia pombe kabisa.

WHO pia inashauri ni vizuri ukomo wa ulevi ukawa ni wastani wanaoutaka gramu 0.05 kwa kila desimali lita (0.05g/dl) kwa madereva wazoefu na wasio na uzoefu ni gramu 0.02g/dl kwa madereva wapya.

Kutokana na ajali hizo, ni wakati wa madereva na watembeaji kwa miguu, kuheshimu sheria za usalama barabarani kupunguza vifo vitokanavyo na ajali.