Kunahitajika vituo vya mabasi ili kuwanusuru abiria jua kali, mvua

25Nov 2021
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kunahitajika vituo vya mabasi ili kuwanusuru abiria jua kali, mvua

USAFIRI wa umma unatumiwa na wengi, kutoka eneo moja hadi lingine. Hivyo, kunahitajika usalama wa abiria wa maeneo ya kupandia na kushuka vituoni.

Kuwapo vituo vya kupumzika iko wazi ni muhimu kwenye kila sehemu iliyotengwa mahsusi kwa huduma hiyo. Hiyo inawaepusha abiria kupigwa na jua, hususan majira ya mchana ikizingatiwa kipindi hiki ni cha jua kali.

Ni kila mahali mijini na vijijini, watu wanalalamikia kuwapo ongezeko la joto pamoja na ukame. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuona ongezeko la joto kwenye mikoa mingi mwaka huu, hali inafikia nyuzi joto 36.

Hiyo ni ongezeko la zaidi ya nyuzi 3.5 juu ya wastani wa kawaida imetawala miaka mingi na wataalamu wa afya wanaeleza athari za jua kali kwenye mwili wa binadamu, inajumuisha vipele vya muwasho, ngozi kuungua au hata kusababisha magonjwa ya ngozi ikiwamo saratani.

Kwa usafiri wa jijini Dar es Salaam, wakati abiria anaposubiri usafiri wa umma ni kawaida humchukua hata wastani wa nusu saa kabla ya kufika muda anaoutarajia kuwasili kituoni hapo. Anapokuwa mahali hapo anahitaji kupumzika.

Jambo zuri limefanywa na mamlaka husika kwa kuwa na maeneo mengi ya mwisho wa safari jijini Dar es Salaam, kama vile Makumbusho, Kijitonyama na Ubungo Mawasiliano, kuna vituo vya kupumzika abiria. Katika ujenzi wa barabara mpya, suala la vituo vya kupumzika limezingatiwa.

Kwingineko nako, vituo vya abiria havipo. Hilo linawafanya abiria wasimame juani hapo katika msimu huu mvua hazijaanza na zikianza, kuna suala la kunyeshewa.

Nasema, ulikuwa muda mwafaka kwa sehemu ambazo wameondolewa wajasiriamali, kungejengwa vituo kwa ajili ya abiria, kwa kuwa ni kati ya haki za usafiri wa umma. Huko nyuma huduma hiyo haikuwapo, ila walijitahidi kujibanza katika sehemu hizo.

Nitoe mifano michache, kama vile barabara za Mandela na Uhuru ambako hakuna pa abiria kujihifadhi kituoni, mbadala wao wanaangalia mahali penye mti wajisiriamali au panapokuwapo nyumba jirani.

Si njia hizo tu, barabara za nje ya mji ndio ‘usiseme’ kukutana na kituo cha abiria ni nadra sana na hata kuwa kama vile imehalalishwa kwa staili yake.

Barabara ya Morogoro, ni mfano mwingime ambako vituo vipo kwenye njia ya mwendokasi pekee. Hapo kunanifanya niendelee kusistiza kwamba, eneo la kupumzika abiria ni muhimu sana. Katika usafiri huu watumiaji wako wa kada tofauti; wazee, watoto, wajawazito na wenye ulemavu.

Vituo vinapokuwapo, vinasaidia kupunguzia abiria hali nyingine inayoonekana kututesa abiria, kupanda na kushuka popote tunapoona kunafaa, hasa gari linapokuwa majonzi panamfaa na kusababisha foleni.

Daktari wa Magonjwa ya Binadamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili - Mloganzila, Dk. Milagilo Malombe, anasema hali ya sasa ya joto kali lina athari kubwa kwa afya ya mwanadamu, kama hakuna hatua za haraka zinazochukuliwa.

Anataja kubwa ni kuwataka watu kuzingatia kuupoza mwili kwa maji na kuepuka kukaa muda mrefu kwenye jua kali, ikiwamo kutembea juani muda mrefu bila kujifunika.

Dk. Malombe anasema, katika kipindi kilichopo mtu anapoteza maji mengi mwilini kwa njia ya jasho inayosababishwa na kiwango cha juu cha joto pamoja na maji yanayotoka kwa njia ya mvuke.

Anashauri pia watu waepuke kukaa muda mrefu juani ili kuepusha uwezekano wa kutokwa na jasho jingi hivyo kupoteza maji zaidi na kuumia ngozi.