Kupanda bei ya mafuta mtaani kumebadili ghafla mkao wetu  

12May 2022
Halfani Chusi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kupanda bei ya mafuta mtaani kumebadili ghafla mkao wetu  

BEI ya mafuta kwa sasa ipo juu na sasa imeongeza gharama kwa wananchi kwa kuongezeka kasi ya ugumu wa maisha, kwa kiwango kikubwa kutokana na bei za bidhaa au kwa lugha rahisi mfumuko wa bei.

Watanzania wengi wamejiajiri katika kuendesha vyombo vya moto kama vile Bajaji na Bodaboda, ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.

Kwa hiyo, kupanda bei ya mafuta kumewaathiri wengi, lakini kikubwa zaidi ni hilo la kuongezeka kwa bei kwa baadhi ya vyombo vya usafiri kama vile daladala, Bajaji na Bodaboda.

Kwa mtazamo wangu, suala la kupanda bei za nauli kwa vyombo vya usafiri kupitia ongezeko la bei ya mafuta limeongeza kwa kasi, ugumu wa maisha huko mitaani tuliko na kwingineko.

Kupitia gharama za usafiri kuwa juu, bei ya vitu navyo imekuwa juu hasa sokoni kunakopatikana vyakula, ukweli ni kwamba hata unapododosa nini shida, mrejesho kutoka kwa wauzaji ni kwamba wanasafirisha bidhaa hizo kwa gharama kubwa sana, ikichagizwa na kupanda gharama za mafuta ya vyombo vya usafiri.

Maumivu ni makubwa mno kwa watu wenye vipato vidogo na Waswahili wanasema, kipato kwa sasa hakikidhi mahitaji, kwa maana ya kuwa kinachopatikana hakimudu gharama za matumizi.

Lakini, linaloleta faraja ni pale timu ya kiserikali kwa kuanzia na mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua, ipo mbioni kutupunguzia makali hayo.

Katika hili nasema, ni jambo la heri na muhimu, kwani litawasaidia Watanzania wote na hasa wenye vipato vidogo katika jitihada za kumudu mahitaji na kurejesha tumaini jipya la mtaani ambako kuna kundi kubwa la umma.

Rai yangu kwa serikali ni kuharakia kushuka kwa bei ya mafuta, kwa kuwa hali ni mbaya mtaani kwa kufanya hivyo kutapunguza gharama za maisha na kuongeza mzunguko wa pesa mtaani.

Angalau niwarejeshee tena lugha ya ahsante, kwa kile kinachotajwa kutekelezwa kuanzia wiki tatu zijazo.

Mbali na ongezeko la nauli katika vyombo vya usafiri kutokana na kupanda kwa bei, pia katika pembejeo za kilimo, kwa sasa hali nayo ni mbaya zaidi kulinganisha na miaka ya nyuma, huku baadhi ya wafanyabiashara wa pembejeo hizo wakisingizia kupanda kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa hizo.

Ukiangalia hapo kuna kundi kubwa la wakulima linashindwa kukabiliana na gharama za pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu, mbolea na dawa kwa ajili yake.

Ni hali inayowafanya wakulima washindwe kulima na wengine hawawezi kuzalisha mazao bora yatakayoleta changamoto ya ushindani  kutunadi katika soko la kimataifa na kwingineko.

Kwa ujumla, tukiangalia suala hilo la kupanda kwa gharama za mafuta kwa mapana yake, limewaathiri wengi na mambo yamekuwa magumu zaidi kila sekta, kutokana na maeneo mengi ya uzalishaji nchini kwetu kutegemea usafirishaji kwa asilimia kubwa.