Kupigwa kwa Mbowe kunavyoacha maswali

10Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kupigwa kwa Mbowe kunavyoacha maswali

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema Freeman Mbowe, amevamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake akiwa jijini Dodoma.

Mashambulizi hayo yaliyofanyika Jumatatu usiku eneo la Area D licha ya kwamba hayajafahamika alishambuliwa kwa namna gani , yamesababisha Mbowe kuendelea na matibabu katika hospitali iliyoko huko Dodoma.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amevieleza vyombo vya habari kuwa shambulio hilo lina sura ya kisiasa, lakini hakueleza zaidi , ila kinachoambatana na uvamizi huo ni maswali kama hivi Mbowe hana walinzi? Iwapo wapo ni wa namna gani?

Msukosuko wa Mbowe unakuja saa chache baada ya kutangazwa kwa taarifa kuwa Tundu Lissu, ana nia ya kuwania urais kupitia Chadema Oktoba mwaka huu,

Nia si kujiingiza kwenye suala la Lisu na Mbowe bali ni kutaka kuwakumbusha viongozi, wanasiasa na Watanzania kuwa wanasiasa wote wanawajibika kuwatumikia Watanzania hivyo hakuna sababu za uadui.

Kwa hivyo, tunategemea kuona kuwa hakuna sababu ya malumbano bali waliomshambulia Mbowe wanafikishwa mbele ya sheria.

Hakuna sababu ya kuendelea kutupiana mpira na kulaumiana kutoka pande zinazohusika na ulinzi na usalama wa kiongozi huyo.

Ni ukweli kuwa pamoja na kufahamu yaliyotokea wananchi wengi wanategemea kuwa eneo analoishi kiongozi huyo ni sehemu salama na kuna ulinzi hivyo yanaibuka maswali mengi kuhusu kilichosababisha tukio hilo.

Ukosefu wa usalama eneo analoishi kiongozi wa kambi ya upinzani na mwenyekiti wa chama kikubwa cha upinzani ni jambo ambalo huenda linawashangaza pia.

Halikadhalika watu watajiuliza ni nani anayemshambulia Mbowe? Sababu ni zipi? Lakini, pamoja na maswali hayo watataka kujua ilikuwaje tukio kama hilo linaripotiwa baada ya Lissu kushambuliwa mwaka 2017 na pia kutangaza nia ya kugombea urais 2020?

Wapo wanaoweza kuwaza kuwa lengo ni kuudhoofisha na kuuyumbisha upinzani hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu miezi mine kuanzia sasa.

Japo, inaonekana kuwa ni masuala ya kisiasa zaidi kwa mujibu wa Mnyika ukweli, tukio hilo unaichafua sifa ya nchi hii ambayo haikustahili kuhusishwa na masuala ya kushambulia na kusulubu kwa risasi wanasiasa huko Dodoma.

Ikunbukwe kuwa Tanzania ilichafuka na mauaji ya albino na udhalilishwaji uliohusika kuuza sehemu za miili yao na kwa madai ya kusaka utajiri, umaarufu, nguvu za kujamiiana na mengine yanayofanana na hayo.

Kushambulia na kujeruhi viongozi wa kisiasa ni chanzo cha kupewa jina baya na nchi kuonekana kama ni eneo lisilo salama duniani ambalo si jina jema kwa Tanzania ambayo ni kisiwa cha amani.

Mathalani, tukirejea mashambulio dhidi ya mwanachama na aliyekuwa mbunge Tundu Lissu, kupigwa kwake kulikofanyika Dodoma mwaka 2017 hadi leo hakuna majibu wala aliyekamatwa au kuchukuliwa hatua.

Kipigo cha Lissu na mlolongo mzima wa kushughulikia kisa chake unaonyesha jinsi ambavyo baadhi ya watu wanakosa uvumilivu wa kisiasa.

Kupigwa Mbowe na Lissu huenda ni matokeo ya kukosekana uvumilivu wa kisiasa na madhara yake yanaweza kusababisha Tanzania kudharauliwa duniani hasa kwa mataifa wapenda demokrasia.

Tanzania imekuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu na kuwa msuluhishi wa mauji ya kimbari yaliyofanyika kwa mataifa jirani. Kwa ujumla ni mhimili wa amani barani Afrika, chonde hakuna haja ya kuharibu sifa hiyo.

Kwa ujumla kushambuliwa Mbowe kunaumiza si familia yake bali Watanzania wengi wakiwamo wapinzani na wasio wafuasi wake ni kwa sababu ni kiongozi anayetetea maslahi ya taifa na pia ni mmoja wa wanaotimiza majukumu ya kikatiba ya kuikosoa, kuisimamia na kuishauri serikali ambayo ni kazi kuu ya upinzani katika kudumisha demokrasia.

Tanzania ni nchi yenye viongozi majasiri, ina wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wasio na woga na ni taifa linalojisimamia lenyewe kwenye ajenda za maendeleo, kulinda na kudumisha demokrasia hivyo ndiyo wakati wa kusimama na kukemea ili kuliepusha taifa na vitisho na mashambulio ya kudhoofisha wanasiasa.