Kushughulikiana huku kutaleta kujidhoofisha

13May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kushughulikiana huku kutaleta kujidhoofisha

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewafukuza uanachama wabunge wanne, huku wengine 11 wakitakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu.

Hiyo, inatokana na wabunge hao kuhudhuria vikao vya bunge badala ya kujiweka eneo la kujitenga kwa siku 14 kama ambavyo chama kiliagiza, lakini wao wakakiuka maelekezo hayo.

Wabunge waliofukuzwa katika chama hicho ni Antony Komu (Moshi Vijijini), Joseph Selasini (Rombo), wote kutoka mkoani Kilimanjaro, Wilfred Rwakatare (Bukoba Mjini), Kagera na David Silinde(Mbozi) mkoani Songwe.

Aidha, wanaotakiwa kujieleza ni wabunge wa Viti Maalum Suzan Masele, Joyce Sokombi, Rose Kamili, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Sware Semesi, Sabrina Sungura na Anne Gideria.

Mbali na hao, pia mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael, wa Kilombero, Peter Lijualikali na Karatu, William Kambalo, hali ambayo inaonyesha mpasuko ndani ya chama hicho.

Chama hicho kimewafukuza uanachama wabunge wanne, huku wengine 11 wakitakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu, kufuatia hatua yao ya kuhudhuria vikao vya bunge badala ya kujitenga.

Huenda hatua hiyo ya Chadema inaweza kusababisha sintofahamu hasa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu, na chama hicho nacho kinajiandaa kushiriki.

Ninasema hivyo, kwa sababu suala la msamaha na maelewano katika chama ni la muhimu kwa ajili ya kuimarisha kuliko kuchukua hatua za kufukuzana kipindi hiki ambacho umoja unahitajika zaidi.

Nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu, hivyo hatua zozote zinatakiwa kuchukuliwa kwa umakini kwa lengo la kujenga chama kuliko kukifanya watu wakione siyo sehemu ya sahihi ya kuendesha siasa.

Vinginevyo Chadema inaweza kuingia kwenye uchaguzi mkuu ikiwa vipande vipande, hali ambayo si salama kwa uhai wa kisiasa wa chama hicho kikubwa cha upinzani nchini.

Waswahili wanasema kwamba, 'umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu', hivyo Chadema kufukuza wanachama wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ni kujiongezea udhaifu.

Kipindi hiki kilikuwa ni nafasi nzuri kwa chama kujipanga na kujiimarisha zaidi badala ya kufukuzana, hali ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kusababisha kiyumbe, kwani chama ni wanachama.

Ndiyo, chama kina katiba, kanuni na miongozo yake, lakini uamuzi uliochukuliwa kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi unaweza kukidhoofisha, kwani waweza kuwa faida kwa vyama vingine.

Umoja imara ndani ya chama ndiyo unaoweza kufanya vyama vikaungana kama ilivyotokea vikaanzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao ulichangia kuvifanya vipate wabunge na madiwani wengi mwaka 2015.

Kwa hiyo mtazamo wa vyama vya upinzani ungekuwa ni kutafuta jinsi ya kujiimarisha zaidi hata kama vinakutana na changamoto kama hizo ambazo zingeweza kuvumiliwa wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Siyo siri kwamba kwenye msafara wa mamba, kenge huwa pia wamo, hivyo hata katika chama, wasaliti pia huwa wamo, lakini zinahitajika mbinu zaidi za kuwashughulikia kwa lengo la kuimarisha umoja katika chama.

Ikumbukwe kwamba Januari mwaka huu, chama hicho kilifunga pazia kwa wanachama wake wanaotaka kuwania ubunge na udiwani kuandika barua za maombi katika maeneo yao ili wajadiliwe na vikao maalum.

Mchakato huo umefanyika kwa lengo la kuhakikisha chama hicho kinapata wanachama ambao kinaamini hawawezi kukiangusha kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, zaidi ya wanachama 70 walijitokeza kuomba kuwania na ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini.

Hatua hiyo ya kujitokeza wanachama wengi kuomba kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi ujao, inaelezwa na Mrema kwamba chama hicho kinazidi kupendwa, na kwamba chama hicho kinafanya mambo kwa uwazi.

Kwamba kilitangaza mchakato huo wanachama wakajitokeza na sasa kimeshafunga rasmi pazi, na kilichobaki ni taratibu nyingine za kufanikisha mchakato huo, ili kupata wanachama sahihi wa kukiwakilisha.

Hivyo nguvu kubwa zingeelekezwa katika mchakato huo na kufikia mengine yanayojitokeza hadi kuhakikisha uchaguzi mkuu unapita kwanza, kwa kutambua kwamba kwenye msafara wa 'mamba, kenge hawakosekani'.