Kusomeana meseji kwenye daladala vipi?

14May 2017
Jenifer Julius
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Kusomeana meseji kwenye daladala vipi?

ASILIMIA kubwa ya wakazi wa miji wanategemea usafiri wa umma na wanapokuwa ndani ya daladala ndiko wanapopata fursa ya kutumia simu iwe kusoma ujumbe, kuandika ama kutongoa-kuchati.

Usafiri huu una watu kutoka sehemu mbalimbali wenye tabia tofauti hivyo hata mienendo yao hutofautiana, kuna wengi wamezoea kupiga chabo, kudokoa na baadhi maneno machafu.

Kati ya yanayojiri ndani ya magari haya kupiga chabo na kusoma ujumbe kwenye simu, ukiwa kwenye daladala mara simu yako inapokea ujumbe unaitoa na kuanza kuusoma, cha ajabu utakuta na jirani yako naye ambaye hata hamjuani anajitahidi kuisoma.

Wakati mwingine unakuta watu wawili au zaidi wamekodolea macho kwenye simu ya mtu wanaangalia kila anachokifanya, tena wamezubaa kana kwamba wako sinema au wanaangalia kipindi kizuri kwenye luninga.

Tabia hii si nzuri , wakati mwingine mtu anakuwa anasoma meseji za siri ambazo asingependa mtu mwingine afahamu, hivyo akija kugundua kuwa kuna mtu pembeni yake alikuwa anasoma anakosa amani .

Kuna msemo kuwa, usichopenda kutendewa usimtendee mwenzako, hivyo wewe mwenye tabia ya kusoma ujumbe za simu za watu kwenye daladala, au kwenye kusanyiko kabla ya kuanza kusoma jiulize kama ingelikuwa ni wewe ndiye unasomewa ungejisikiaje?.

Hakuna faida yoyote unayopata pale unapokodoa macho yako na kuanza kuchunguza simu ya mwenzako na kusoma mambo yake ,acha tabia hiyo kwani unawakera wenzako.

Wakati mwingine utakuta mtu na rafiki yake wanaonyeshana kilichoandikwa kwenye simu ya abiria jirani kisha wanasengenya pembeni na kucheka, haipendezi!

Acheni kuchunguza mambo ya watu kwa kiasi hicho. Imefika wakati ambapo mtu kabla ya kusoma kilichoko kwenye ujumbe wa simu unapoingia aangalie huku na kule kama kuna usalama, si vizuri abiria kuongezeana hofu.

Msafiri awaze kuchunga fedha zake ndani ya mfuko lakini tena awaze kuficha anachosoma kwenye simu yake jamani mnawachosha wenzenu.

Hata kama macho hayana pazia, ila si kwa vitu binafsi kama simu, iwapo umevutiwa jirani yako alipotoa simu yake na wewe toa yako kuliko kuangalia ya mwenzako kama vile ni yako.

Tena tabia hii haipo kwa watu wa rika moja tu , unaweza kumkuta baba au mama na heshima zake anajitahidi kusoma ujumbe wa jirani , anafuatilia anachoandika kisha anacheka au anatingisha kichwa, tena anasubiri yule ashuke ili ahadiithie jirani yake .

Mambo kama haya wakati mwingine yanaibua ugomvi unaosababisha watu kupigana na kutoleana lugha chafu, kwa sababu ni tabia ambayo haivumiliki hivyo kama mtu ana hasira za karibu lazima pachimbike .

Si hilo tu ,ukiendelea na tabia hizi siku utakuja kuona ujumbe wa ajabu kwenye simu ya mtu ukakukosesha amani hata kukuharibia siku yako .

Watanzania elimikeni na kustaarabika na kuwa na mipaka hasa mnapokutana na watu wengine sehemu zenye mikusanyiko kama kwenye daladala, ukumbini, kwenye vituo vya mabasi au mikutanoni kila mtu anakuwa na mambo yake na sehemu kuu ya mawasiliano ni simu kwa hivyo tupeane nafasi ili kila mmoja awe na uhuru wa kuitumia vile apendavyo.

Lakini na nyie wenye simu msiwakwaze wenzenu epuka kufungua picha za ngono na mambo machafu ambayo yanaweza kuwavutia wasio na maadili lakini pia kuwakera abiria jirani wenye heshima na wasiopenda uchafu kama huo.

Kadhalika unaposoma ujumbe wako isiwe ni matangazo mfano unanyanyua simu juu au kuiweka iIi ionekane na kila mmoja aliye jirani nawe. Huo ni uchokozi.