Kusubiri tamko kuu ni kuchelewa kuchukua tahadhari maradhi haya

25Feb 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kusubiri tamko kuu ni kuchelewa kuchukua tahadhari maradhi haya

KATIKA siku za karibuni kumekuwapo mjadala kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wakitaka serikali itoe tamko kuhusu tatizo la upumuaji, huku wengine wakitaka jamii ichukue tahadhari badala ya kusubiri tamko.

Wote kama Watanzania wana haki kutoa maoni, lakini maoni yasichangie kupotosha jamii, badala yake yaisaidie kuchukua hatua zinazoshauriwa na watalaamu wa afya ili kukabiliana na tatizo hilo.

Binafsi, ninaamini Watanzania wengi wanajua kila kitu kuhusu ugonjwa huo tangu dalili zake hadi njia za kujikinga. Kama mtu unajua tatizo na njia zake za kujikinga, kuna haja gani ya kusubiri tamko?

Watu kukaa na kuendelea kuhoji au kuitaka serikali itamke kuhusu kuwapo kwa ugonjwa huo nchini ni matumizi mabaya ya muda, ambao ungetumika kufanya mambo mengine ya muhimu.

Kwanini mtu asichukue hatua zinazotakiwa kama anaona kuna tatizo mbele yake na kubaki akisubiri tamko? Tamko litasaidia nini zaidi ya kuzingatia masharti ya kuepuka ugonjwa huo?

Hata kama hakuna tamko la serikali, kila Mtanzania anatakiwa kufanya sehemu yake kwa kuchukua tahadhari za kiafya ili kujikinga na maambukizo, kwa kuzingatia kwamba, Tanzania siyo kisiwa.

Watu kuendelea kuhoji na kutaka tamko, ni sawa na kuchelewa kuchukua hatua zinazoelekezwa na wataalamu wa afya na mwisho wake ni matatizo ya kujitakia.

Tayari serikali imeshasema haijamzuia mtu yeyote kuvaa barakoa na taratibu nyingine zinazoshauriwa na wataalam wa afya, lakini ikashauri kutumia barakoa zilizotengenezwa nchini.

Kukaa na kuendelea kusubiri tamko ni kupoteza muda. Badala yake, kila mmoja anapaswa kutumia tamko kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo, kama ambavyo wataalamu wa afya wanaelekeza kwa ajili ya kukabiliana nao.

Ni vyema kila mkazi nchini afanye sehemu yake, kwa kuzingatia maelekezo ya watu wa afya, ambayo kimsingi yameshawekwa wazi na kuendelea kuhoji au kutaka tamko bila kujikinga ni sawa na kujitafutia matatizo.

Mwaka jana, Tanzania ilipitia tatizo hilo na kulazimika kufungwa baadhi ya huduma kama shule, huku watu wakitakiwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, ikiwamo kunawa kwa maji tiririka, vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko.

Vilevile, hatua nyingine zinazotakiwa kuchukuliwa ni pamoja na kufunika mdomo na pua pale mtu anapopiga chafya na kukohoa, lengo ni kusaidia kujikinga au ueneaji maradhi hayo au ya namna hiyo yanayoendelea kuisumbua dunia.  

Aidha, kuna tiba na kinga mbadala wa kukabiliana na ugonjwa huo, ni upigaji nyungu kujihakikishia usalama kiafya ingawa bado baadhi ya watu wanaendelea kuhoji kitu ambacho wanakijua.

Tahadhari hizo zilienda sambamba na kuagiza madereva wa daladala kutojaza abiria kupita kiasi na badala yake wakawa ni wale waliokaa kwenye viti tu. Lakini ni ajabu kushuhudia, kuna wanahoji mambo ambayo wanayajua.

Hayo yote ni wazi kwamba yanajulikana, lakini cha ajabu ni watu kuanza kuhoji na kutaka tamko ili kujikinga na tatizo la kupumua kana kwamba hawajui lolote kuhusu mbinu za kukabiliana na ugonjwa huo au maradhi yanayoenea kwa namna hiyo.

Inawezekanaje mtu ukaona tatizo mbele yake, badala ya kuchukua hatua za kulikwepa au kukabiliana nalo. Anasubiri kwanza hadi asikie tamko. Sidhani kama itakuwa sahihi kufanya hivyo.

kunapaswa tamko lisiwe kikwazo cha kushindwa kuchukua tahadhari, badala yake jamii yenyewe ihamasishane, ili kila mtu azingatie kwa vitendo maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Wakati hayo yakifanyika, madereva na makondakta wa daladala zinazotawala hasa mijini nao wasisubiri tamko ndipo waache mtindo wa kujaza abiria kupita kiasi katika magari yao.

Ikumbukwe kuwa kwenye tatizo la upumuaji, watu wanatakiwa kupeana nafasi katika kukaa, ili kuepuka kuambukizana, hivyo hata kwenye usafiri ni muhimu hali hiyo irudi kama ilivyokuwa mwaka jana.

Kwa Jiji la Dar es, siyo vibaya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), ikaruhusu magari binafsi yakaingia katika ya jiji kusaidiana na daladala kubeba abiria, ili kupunguza msongamano ndani ya daladala.

Mwaka jana LATRA ilichukua hatua kama hizo, kama inawezekana, ichukue tena kama sehemu ya kuzingatia kile ambacho kinashauriwa na wataalamu wa afya kwa ajili ya kujikinga na maradhi hayo.