Kutambua wadudu sugu kwa dawa ni elimu tosha

10Jan 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kutambua wadudu sugu kwa dawa ni elimu tosha

MAANA ya usugu kwa antibaiotiki inaelezwa na wataalamu wa afya, ni hali ya vimelea vya magonjwa kutokufa kwa dawa iliyothibitika na inayotumika kuua vimelea hivyo.

Dawa za antibaiotiki zinatajwa kuwa katika kundi la dawa linalojulikana kitaalamu ‘antimicrobials’ ambazo hutumika kuua au kuzuia ukuaji vimelea vinavyosababisha magonjwa ya kuambukiza binadamu na wanyama.

Aidha, inakadiriwa watu 700,000 hufariki duniani kila mwaka, kutokana na usugu wa wadudu na kwamba asilimia 89 ya vifo vyote hutokea barani Afrika na Asia.

Hiyo ni kwa mujibu wa ofisa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Dk. Boniface Marwa, alipofungua mafunzo ya namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi kwa kufuata miongozo wakati wa kumuhudumia mgonjwa mkoani Kigoma.

Ni mwezi Oktoba mwaka jana, alikaririwa na vyombo vya habari, akisisitiza kuwa jitihada za makusudi ni lazima zichukuliwe kila mtaalamu katika sekta ya afya, apambane na tatizo hilo.

Dk. Marwa anasema, tatizo hilo linazidi kuwa tishio duniani na haja ya kufanyika utafiti kupata dawa mpya zitakazoweza kupambana na wadudu sugu.

Wakati serikali ikielekeza hayo, ipo haja kwa jamii nayo kuchukua hatua, ikiwamo kuzingatia elimu, ambayo imekuwa ikitolea kila mara kuhusu madhara ya usugu wa wadudu dhidi ya dawa.

Ikumbukwe, usugu wa dawa umekuwa moja ya tishio kubwa kwa afya ya wananchi katika jamii, hivyo ni muhimu kuzingatia maelekezo au elimu kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.

Wadudu sugu dhidi ya dawa ni tatizo linaloendelea kusumbua jamii, hivyo jamii izingatie elimu inayotolewa kuhusu madhara yanayoweza kutokea na pia watumishi wa sekta ya afya, wafuate miongozo na taratibu za utoaji huduma za afya wakati wa kutoa huduma kwa mgonjwa.

Kwa kuzingatia hilo, Watanzania wenye mtindo wa kutumia dawa zisizo na ulazima yanaweza kupungua kama siyo kumalizika kabisa ili yasiendelee kusababisha tatizo la usugu wa wadudu dhidi ya dawa.

Hivyo, elimu kwa umma ni muhimu izingatiwe na kutambua usugu wa dawa ni hali, ambayo dawa husika inashindwa kuua wadudu mbalimbali kama bakteria.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linaweka wazi kwamba usugu wa dawa ni janga la kidunia kwa vile karibia kila nchi imeripoti kushindwa kwa baadhi ya dawa kufanya kazi.

Linafafanua kuwa kushindwa kutibu magonjwa mbalimbali ya kuambukiza mwisho wa siku kupelekea ugonjwa kukaa muda mrefu, mgonjwa kushindwa kufanya shughuli mbalimbali na hatimaye kusababisha kifo.

Umma unatakiwa kupata elimu ya kutosha ya kujua visababishi vya usugu wa dawa ambavyo vimekuwa vikitajwa na wataalamu wa afya na kuvizingatia, kwani hiyo ni njia mojawapo kuwa salama.

Kiuhalisia dawa inapotumika muda mrefu, vijidudu huishia kuwa sugu kwa dawa hiyo, ingawa kuna baadhi ya tabia za kibinadamu, ambazo huchangia kwa uharaka zaidi kwa usugu huo kutokea.

Kupitia elimu tena ya kutosha, jamii itajua kuwa kuishi katika mazingira yasiyo masafi kama vile kunywa maji yasiyochemshwa, kula vyakula visivyoandaliwa katika mazingira yanayotakiwa huchangia kusambaza vijidudu sugu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Mbali na hilo, jamii pia itajua kwamba kutokumaliza dozi ya dawa za kuua vijidudu, na kuishia njiani pale mtu anapoona amepata nafuu, husababisha kuzalishwa kwa vijidudu sugu.

Suala la kufuata maelekezo ya wataalamu wa dawa (wafamasi), katika matumizi ya dawa ikiwamo kuhakikisha mgonjwa anamaliza dozi na kutokusahau kunywa dawa kwa muda elekezi ni jambo la msingi.

Kwa kuzingatia elimu, kutamfanya mtu aepuke kwenda katika duka la dawa na kununua dawa bila kupata ushauri wa daktari au kufanyiwa uchuguzi ili kufahamu ni mdudu yupi aliyesababisha ugonjwa husika.