Kutokana lililoanikwa, Polisi tujitakatishe

21Mar 2019
Beatrice Shayo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kutokana lililoanikwa, Polisi tujitakatishe

JESHI la Polisi lina wajibu wa kuwachukulia hatua askari wake wanaoenda kinyume na maadili ya kazi yao, pia kuwapongeza watiifu, kujenga uaminifu kwa raia na kuongeza nidhamu ya jeshi.

Kumekuwapo na malalamiko ya kila mara katika vituo vyetu vya polisi, kuwa baadhi ya washtakiwa wanapofikishwa katika vituo, wanabambikwa kesi wasizozifahamu na wanapotaka kuhoji, hawapewi nafasi, baadhi wakati mwingine hata kupigwa, ili asihoji jambo lolote.

Polisi limekuwa likiwahimiza raia kufuata sheria au kutii pasipo shuruti. Hili ni jambo la msingi na sote tunalipigia makofi.

Lakini, raia tunapata kigugumizi, hasa inapotokea mikasa tena yanathibitishwa na mamlaka za kisheria za serikali, askari kuwabambikia wananchi kesi, je, kuna sheria gani inafuatwa hapo?

Je, maadili yenu ya kazi yako wapi, ambayo mnasisitizwa sana hata na viongozi wenu wa juu waliopitia awamu mbalimbali?

Najiuliza, ni sahihi mnataka raia wawakumbushe kiapo cha majukumu yenu ya kila siku, au ndiyo kwa matendo haya matuambia, baadhi mmeshayatelekeza kule chuoni?

Maswali yananielemea, Polisi unapata faida gani unapombambika kesi mshtakiwa? Au ni ulevi wa madaraka ya kazi, kwa nyie mnayoyafanya hayo?

Je, nani anayekupa jeuri ya kumbadilishia mtu makosa yake ama ni nguvu ya fedha inakufanya unasahau kiapo cha kazi yako?

Wapo ambao wana fedha hushirikiana na askari, ili kumkamata mtu kwa chuki zake na kutaka kumuweka kituo cha polisi, ili mradi kumtesa na kama hujui haki zake, anashindwa kutoa malalamiko kama ameonewa.

Suala la askari kubambika kesi kwa watuhumiwa sio jambo geni, limekuwa likilalamikiwa kila wakati na haitashangaza ama kuwashuhudia au kusikia kuwapo kwa mtu gerezani kabambikwa kesi.

Hivi karibuni tumemsikia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, akiianika hadharani polisi kwa kueleza askari wake walivyombambikiza kesi ya mauaji, mfanyabiashara Mussa Sadiki.

Mshtakiwa huyo aliandika barua kwa Rais Dk. John Magufuli, kupitia katika gazeti moja la kila siku, akilalamikia kubambikiwa kesi ya mauaji ambayo DPP alitaja namba yake kutokea mkoani Tabora.

Ilielezwa kuwa, mfanyabiashara huyo baada ya kukamatwa na polisi, walimnyang'anya fedha taslimu, simu ya mkononi na mali alipokuwa amenunua kwa ajili ya wakulima wakati anakwenda kufanya ununuzi.

DPP Biswalo alisema kwamba, walifuatilia malalamiko hayo na kubaini mfanyabiashara huyo alibambikwa kesi, kwa kuwa kitabu cha kuzuia wahalifu kilichopo katika kituo cha polisi, kinaonyesha mtuhumiwa alikamatwa Juni 21, mwaka jana, kwa kosa la kuvunja nyumba usiku.

Kitabu hicho kinaonyesha mlalamikaji alitolewa mahabusu Juni 29, mwaka jana na kupelekwa mahakamani na tarehe hiyo hiyo, alikofunguliwa kesi ya mauaji Namba 8/2018 ikionyesha Mei 6, 2018, akiwa barabara ya Kazima, Tabora Mjini alimuua Jackson Thomas.

Ni tukio lililoibua simanzi kwa watu, jinsi ambavyo sinema ilivyotumika katika kubadilisha mashtaka mpaka anavyokwenda mahakamani na kusomewa kesi, ambayo haipo katika maelezo ya awali.

Kupitia ukweli huo umma ambao tulipewa na DPP, dai ambalo polisi walikiri makosa, ni zaidi ya unyama uliopitiliza.

Leo hii, ni swali la kujuliza sote ni vipi kwa anayekutwa na kama haya, mhusika anaweza kujisafisha. Kimsingi na hata familia ya mhusika inapata wakati mgumu wa kujua mwelekeo na hatima ya ndugu yao, aliyekuwa gerezani.

Katika tukio hilo, kumeonyeshwa uonevu uliopitiliza mtu kuwekwa katika kituo cha polisi wiki nzima kwa kesi ya kuvunja nyumba, alistahili kupatiwa dhamana matokeo yake hakupatiwa.

Niseme kwamba, ufike wakati askari polisi wafanye kazi zao kwa kufuata kiapo na sio kuwaonea wananchi huko vituoni.
Kunapokuwapo matukio ya uonevu yanayofanywa na askari, inasababisha wananchi kukosa imani na Jeshi la Polisi, picha ambayo haistahili kuonekana hata chembe.

Huko huko ndani ya polisi, tujiulize kunapokuwapo na ukakasi wa namna hii, mnamuweka katika sura na nafasi ipi Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro, kuanzia kikazi na hasa kwa umma?

Ni vyema na wakati mwafaka wa ndugu zangu wa polisi, kujisafisha na mambo machafu ya vituoni, tusimbebeshe IGP na wasaidizi wake wa ngazi ya juu, lawama zisizostahili. Dawa kuu ni kubadilika, tukianza na msingi wa kiapo mwisho wa mafunzo, miongozo, kanuni na sheria zinazosimamia majukumu.